DIMBA: Mkenya anayetamba Uswidi kwa ueledi wake katika mashambulizi

DIMBA: Mkenya anayetamba Uswidi kwa ueledi wake katika mashambulizi

Na GEOFFREY ANENE

JOSEPH Stanley Okumu ni mmoja wa mabeki klabu ya IF Elfsborg itatagemea kwenye kampeni zake za Ligi Kuu ya Uswidi (Allsvenskan) na Ligi ya Uropa mwaka huu.

Mkenya huyo mwenye umri wa miaka 23, alichangia pakubwa katika timu hiyo kurejea kwenye Uropa baada ya misimu mitano nje. Alisuka pasi nyingi nzuri na pia kuzima mashambulizi akishirikiana na mabeki wengine timu hiyo ikikamilisha Allsvenskan katika nafasi ya pili.

Okumu, ambaye alishinda tuzo ya mchezaji aliyetia fora wa Elfsborg mwaka 2020, alianza kuinuka kama mchezaji akiwa katika Shule ya Upili ya Wavulana ya Kakamega. Shule hiyo, ambayo timu yake ya soka inafahamika kama Green Commandos, imetoa wachezaji wengi walioingia katika timu ya taifa ya Harambee Stars akiwemo mshambuliaji wa zamani wa Nantes nchini Ufaransa Dennis ‘Menace’ Oliech, winga wa Gor Mahia Clifton Miheso na Eric ‘Marcelo’ Ouma anayechezea klabu ya AIK kwenye Allsvenskan.

Okumu, ambaye jina lake la utani ni ‘Crouch’ kutokana na kuwa mrefu kama mshambuliaji mstaafu wa Uingereza Peter Crouch, alichezea Green Commandos katika michezo ya kitaifa ya Shule za Upili mwaka 2014 ambapo timu hiyo iliibuka bingwa.

Alipiga hatua katika soka yake aliponyakuliwa na Chemilil Sugar mwaka huo na kuichezea kwa muda mfupi kabla ya kuyoyomea ughaibuni katika klabu ya Free State Stars nchini Afrika Kusini mwaka 2016.

Mchezaji huyo, ambaye tetesi zinadai kuwa yuko kwenye rada ya Glasgow Rangers nchini Scotland, alikuwa na Marcelo katika kikosi cha Green Commandos kilichoingia Ligi ya Daraja ya Pili (NSL) mwaka 2018. Kisha, alipata makao mapya nchini Amerika alipojiunga na AFC Ann Arbor mwaka 2018 na kisha, Real Monarchs katika Ligi ya Daraja ya Pili nchini humo.

Wakati huo wote akiwa Amerika, Elfsborg ilikuwa ikifuatilia uchezaji wake kabla ya kuamua ‘anatosha mboga’ baada ya kumuona akichezea Harambee Stars chini ya Mfaransa Sebastien Migne kwenye Kombe la Bara Afrika (AFCON) nchini Misri mwaka 2019. Alijiunga na klabu hiyo bila ada ya uhamisho wiki chache baada ya dimba hilo kukamilika kwa kandarasi ya miaka mitatu itakayofikia tamati Julai 15, 2022.

Umaarufu wake umeongezeka ugani Boras Arena ambapo mchezo wake wa msimu uliopita ulishuhudia akimiminiwa sifa.

Ripoti ya Wyscout ilimtaja Okumu kama mchezaji aliye na uwezo wote wa kunawiri, ingawa bado hajaufikia. “Ana nguvu, na kujumuishwa kwake katika orodha hii ya talanta 11 ya hali ya juu nchini Uswidi wakati huu si utani. Alikuwa muhimu katika Elfsborg kuingia Ligi ya Uropa. Wengi hawakutarajia kabisa kuwa Elfsborg itashiriki Ligi ya Uropa msimu ujao.

Okumu ni ushuhuda kuwa maskauti wa Elfsborg wanafanya kazi nzuri. Walianza kumfuatilia akiwa Monarchs na pia baada ya AFCON. Hawajutii kutafuta huduma zake. Kwenye Allsvenskan 2020, Okumu alikuwa nambari tatu katika kushinda makabiliano ya mipira ya hewani (asilimia 72.32), nambari sita katika kuzima mashambulizi (asilimia 70.54) na alikuwa juu katika kusambaratisha mashambulizi katika kila dakika 90. Bado hajakomaa kabisa, lakini yuko mbioni. Utafurahia ukimuona akiwa na mpira. Pasi zake ni ndefu halafu nzuri. Mara nyingi alianzisha mashambulizi ya Elfsborg kwa njia hiyo. Ana uwezo wa kucheza katika kiwango cha juu zaidi,” ripoti hiyo ya maskauti inasema.

Okumu, ambaye tovuti maarufu ya uhamisho wa wanasoka na masuala yao ya kifedha Transfermarkt inasema ana thamani ya Sh154 milioni, amechezea Elfsborg mechi nzima katika Kombe la Uswidi dhidi ya Degefors, Utsikten na Falkenberg msimu huu. Amehusishwa na Rangers ya kocha Steven Gerrard ambayo inaaminika inajipanga kwa maisha bila Filip Helander anayemezewa mate na Aston Villa na Leicester kwenye Ligi Kuu ya Uingereza. Ili kumuachilia katika kipindi kijacho cha uhamisho, inasemekana Elfsborg itaridhika na Sh300 milioni. Elfsborg itaanza kampeni yake ya ligi dhidi ya waajiri wa zamani wa mshambuliaji Michael Olunga, Djurgarden mnamo April 11.

Okumu, ambaye anaaminika kula mshahara wa Sh7.7 milioni kila mwezi katika klabu ya Elfsborg, alikosa michuano miwili ya Kenya ya kufuzu kushiriki AFCON2022 dhidi ya Misri na Togo mwezi Machi akiuguza jeraha. Alirejea ulingoni Aprili 2 katika mechi ya kirafiki dhidi ya Halmstad ambayo alicheza dakika 45 za kwanza. Elfsborg ilipoteza 1-0.

Nje ya uchezaji, Okumu pia anasaidia katika kuwapa wanafunzi wa Shule ya Upili ya Kakamega motisha kuhusu michezo, hasa soka, pia Januari mwaka huu alifichua kuwa ndoto yake ni kuona vita dhidi ya uhaba wa chakula vinafaulu. Aliunga mkono mradi wa wa ‘Mea Na Mimea’ ulioanzishwa chipukizi wa Kahawa Sportive unaotoa changamoto kwa wakazi wa mijini kutumia nafasi ndogo mitaani mwao kupanda vyakula.

You can share this post!

Mke azima polo kuoa wa pembeni

Utawala bora wa chama cha CPC ni mfano wa kuigwa na Afrika