Michezo

DIMBA PWANI: Ghaib wanalenga soka kuu ya kaunti Kwale ikiwa ni nje ya maskani yao Samburu

August 10th, 2020 2 min read

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

INGAWA imetimiza mwaka wake wa 28 tangu kuundwa, Ghaib FC ya mjini Samburu, ni hadi msimu utakaoanza baadaye ndipo inapotarajia kujiunga na Ligi ya Kaunti ya Kwale inayosimamiwa na Shirikisho la Soka la Kenya (FKF).

Kocha Mkuu wa timu hiyo, Shaban Omar amesema timu hiyo imekuwa haishiriki kwenye ligi yoyote kwa miaka yote hiyo sababu si eti ni dhaifu, haina wachezaji wa kutosha wenye vipaji vya kusakata soka. Anasema kuwa hayo yote yanatokana na ukosefu wa udhamini.

“Timu yetu ina sifa zote zinazohitajika timu kuwa nazo kushiriki kwenye ligi yoyote ile ila imebakia kucheza mechi za kirafiki na mashindano ya sehemu hiyo kwa kuwa haijawahi kupata udhamini,” amesema Omar.

Ghaib FC imepania msimu utakaoanza baadaye mwaka huu, kushiriki kwenye ligi hiyo ya Kaunti ya Kwale kwani maofisa wake wanakwenda mbio kuhakikisha mara hii wamefanikiwa kupata wadhamini wa kuiwezesha kutimiza hilo.

Omar anasema tangu Patrick Rocky aiunde timu hiyo, imekuwa ikijitahidi kupata udhamini ili ishiriki kwenye ligi ya FKF lakini ukosefu wa fedha umeikosesha fursa ya kupata wahisani.

“Tumejitahidi tuwezavyo kuona tumeweza kupata udhamini ili tuweze kutoka nje ya sehemu yetu hii ya Samburu lakini tumeshindwa kufanikiwa kupata wahisani wa kutuonea huruma na kutusaidia ili vijana wetu waonyeshe talanta zao,” akasema mkufunzi huyo.

Akiongea katika uwanja wao wa Kasarani wa hapo Samburu akiwa na Naibu Kocha Hamisi Karungwa, Omar anasema hawajakata tamaa na wangali wanajitahidi kusaka atakayewadhamini ili wafanikiwe kushiriki kwenye ligi hiyo ya kaunti msimu utakaoanza.

Kocha huyo anasema watajitahidi wawezavyo kuhakikisha juhudi zilizofanywa na Rocky za kuianzisha timu hiyo hazipotei bure na akatoa ombi kwa viongozi na wafanyabiashara wa sehemu hiyo wajitolee kuisaidia timu ili iweze kushiriki ligini msimu utakapoanza.

“Tunajitahidi sana kuhakikisha vijana wetu wanashiriki kucheza soka na kuendeleza vipaji vyao na njia mojawapo ya kuwasaidia vijana kufanikisha ndoto zao za kuwa wanasoka wa majina makubwa, ni muhimu kushiriki ligini,” anasema Mwenyekiti wa klabu hiyo, Jira Karungwa.

Karungwa anasema watawafuata viongozi wao kuwaomba wawapatie udhamini ili timu iweze kusafiri sehemu mbalimbali za kaunti hiyo itakaposhiriki kwenye ligi.

“Naamini mara hii tutafanikiwa kwani tunayo nia na tunaona mwangaza uko,” akasema.

Meneja Imran Kadzeni anaiambia Dimba kuwa wana kikosi imara kinachoweza kupambana na timu yoyote ile na akatoa ombi kwa timu ya Ligi Kuu ya Kenya (KPL) ya jimbo la Pwani ya Bandari FC ifike hapo kuchea mechi za kirafiki.

Kikosi hicho cha cha Ghaib FC kina Ibrahim Kombo, Leli Ali, Fadhili Jira (Nahodha), Salim Mboja, Ndurya Rashid, Barnaba Bati, Amar Katili, Iddi Nyerere, Ismail Mkalla, Ahmed Ngati, Beja Chumvi na Mwachizi Hamisi.

Wengine ni Zakaria Jira, Hassan Jira, Iddi Mwanzije, Hamisi Mbuja, Jay Tungwa, Hassan mwarua, Chaka Morris, Mwangale Mboga, Rama Tungwa, Ayub Ndegwa, Ndzai Ndega, Mohamed Karui na Saddam Rashid. Nahodha Fadhili Jira amesema wanawashukuru viongozi wa timu yao kwa juhudi wanazofanya za kutaka timu hiyo ishiriki kwenye ligi ili na wao wachezaji wapate fursa ya kuonekana kuonyesha vipaji vyao na pia kuinua talanta zao.

“Si vizuri kujisifu lakini nikiwa nahodha wa Ghaib FC, ninaamini pamoja na wachezaji wenzangu kuwa tuko wazuri ni vile tu hatujapata fursa ya kushiriki kwenye ligi.

“Tuna matarajio makubwa msimu huu utakaoanza, tutapata udhamini ili nasi tutambe viwanjani na wala sivyo vya hapa Samburu pekee,” akasema Jira huku akishangiliwa na wachezaji wenzake.

Ghaib imepania kuonyesha ubora wao msimu unaokuja kwani wachezaji wanasema watafanya bidii kuhakikisha wakishiriki kwenye ligi hiyo, wanashinda na kupanda Ligi ya Taifa Daraja la Pili.