DIMBA PWANI: Ilianza kama Action Boys FC, sasa ni Beach Bay FC

DIMBA PWANI: Ilianza kama Action Boys FC, sasa ni Beach Bay FC

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

BEACH Bay FC ya Mjanaheri, Kaunti ya Kilifi ni miongoni mwa timu ambazo zinaendelea kufanya vizuri kwenye Ligi ya Kitaifa Daraja la Pili, ikipania kutaka kupanda ngazi hadi Ligi ya Kitaifa Daraja la Kwanza ama msimu ujao wa 2021-2022 au wa 2022-2023.

Klabu hiyo ilifanya juhudi kubwa mwanzoni mwa ligi hiyo na hivi karibuni ilipata msiba wa ghafla alipofariki golikipa wao Jeremiah Karema na kutokana na majonzi ya kumpoteza mchezaji wao huyo, timu hiyo ilipoteza mechi tatu mfululizo na ikawarudisha nyuma kidogo.

“Tulikuwa kwenye nafasi tatu bora lakini tulipoondokewa na Karema, tulirudi nyuma na tuko nafasi ya tano. Tutajitahidi kuhakikisha tunarudi tulipotoka kwani bado tuko na nafasi nzuri ya kuibuka washindi kwenye ligi na kupanda ngazi,” amesema kocha wa timu hiyo, James Mkutano.

Alizitaja mechi tatu hizo kuwa za huzuni kubwa kwao kwani mechi zote tatu dhidi ya Mariakani, Borrusia Dortmund na Samburu Lions FC walipoteza kwa kufungwa bao 1-0.

“Hakika ulikuwa wakati wetu mbaya lakini tulitulizana na sasa tuko sawa,” akasema Mkutano.

Mkufunzi huyo anasema wanasubiri kwa hamu kufunguliwa kwa michezo na serikali ya Kaunti ya Kilifi wapate kucheza mechi zao zilizobakia.

“Tunashindwa kucheza mechi zetu za nyumbani katika viwanja vya kaunti nyingine sababu hatuna pesa za kugharimia safari,” akasema.

Ilikuwa mwaka 1992, vijana wanne wa kijiji cha Mjanaheri kilichoko kaunti ndogo ya Magarini waliokuwa wakipenda soka walipoamua kuanzisha klabu yao kwa ajili ya kuwafanya wawe na timu kali na ya kutambulika kote Pwani.

Stephen Haji Matole, Konde Matole, Stephen Tunde na Bruno Tunde walianzisha klabu kwa jina la Action Boys FC wakiwa na nia ya kuifikisha mbali.

Mkutano anasema waanzilishi hao walikuwa wachezaji wa kwanza wa timu hiyo ambayo baadaye iligeuzwa jina na kuitwa Beach Bay FC.

“Klabu yetu hiyo iligeuzwa na kuitwa Beach Bay FC kwa sababu aliyekuwa mmiliki wa hoteli ya Beach Bay aliidhamini kwa kila kitu. Pia ilitubidi tubadilishe jina kwa sababu tulipojiunga na ligi ya FKF, kulikuwako na klabu nyingine yenye jina la Action Boys FC,” akasema Mkutano.

Alisema waanzilishi wa klabu hiyo walistaafu kucheza vijana wengine wakachukua nafasi zao. “Kiuhakika timu yetu ya Beach Bay FC ni ya vijana wetu wa Mjanaheri pekee hakuna hata mmoja kutoka eneo lingine,” akasema mkufunzi huyo.

Mkutano anasema ingawa haina tena udhamini wa hoteli hiyo, wakazi wa sehemu hiyo wanaihami timu wakisaidiwa na Mbunge wa Magarini, Michael Thoya Kingi pamoja na Mwakilishi wa Wadi ya Magarini, Elinah Stephen Mbaru ambao anawashukuru.

Alisema katika kikosi chake kuna wachezaji ambao wanaweza kuzichezea klabu zozote kubwa hapa nchini wakipewa nafasi ya kufanya majaribio. Mmoja wao ni Baraka Kazungu aliyetakiwa na klabu mbili za ligi wanayoshiriki, Samburu Lions ya Samburu na Maji Bombers FC ya Malindi.

Mwingine ni Amani Kiponda aliyetakiwa na Young Bulls FC ya Magarini inayoshiriki kwenye Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza. Wengine ni Kasena Sulubu, Andrea Hali na Erick Thoya anayemezewa mate na Omax FC.

Wachezaji wengine katika kikosi cha timu hiyo ya Beach Bay ni Ballack Charo (Nahodha), Karisa Kahindi, Samuel Sulubu, Rogers Gona, Elia Hali, Charo Ali na Elisha Mruu.

Nahodha wa Beach Bay FC Ballack Charo. Picha/ Abdulrahman Sheriff

Pia wako James Mbogo, Emmaneu Kazungu, Derrick Gunga, Bahati Sulubu, Furaha Chemu, Omari Mwanyumba, Stanley Chea, Elisha Sulubu, Ibrahim Mwamu,Paulo Chome, Joseph safari na Furaha Safari Kahindi.

You can share this post!

Machifu kuaga afisi za kikoloni

Vijana waliofariki mikononi mwa polisi Embu kuzikwa kwenye...