DIMBA: Ramsdale ‘nyani’ mpya asiyecheka na mtu Emirates

DIMBA: Ramsdale ‘nyani’ mpya asiyecheka na mtu Emirates

Na GEOFFREY ANENE

AARON Christopher Ramsdale ni mmoja wa makipa wanaojizolea umaarufu kwenye ulimwengu wa soka.

Amejitokeza kuwa shujaa mpya kambini mwa Arsenal msimu huu wa 2021-2022 ambao ungali mbichi, baada ya kushinda mechi zake nne za kwanza tangu awasili mwezi Agosti.

Alikuwa michumani wanabunduki wa Arsenal wakimiminia West Bromwich Albion mabao 6-0 katika kipute cha Carabao Cup mnamo Agosti 25; pia katika ushindi wa 1-0 dhidi ya Norwich (Septemba 11) na Burnley (Septemba 18) ligini.

Kipa Aaron Ramsdale asherehekea ushindi wa kwanza wa Arsenal msimu huu, dhidi ya Norwich City katika uwanja wa nyumbani Emirates jijini London, Uingereza, Septemba 2021. Picha/ Maktaba

Umaarufu wake ulipanda zaidi alipowakatisha tamaa majirani Tottenham Hotspur katika gozi la London kaskazini ambalo Arsenal ilitawala 3-1 Septemba 26.

Kipa huyu chipukizi alizaliwa Mei 14, 1998.

Alivutiwa kufanya majukumu ya kulinda lango na Mwingereza mwenzake Ben Foster, ambaye ni shujaa wake. Foster, 38, anachezea Watford.

Yeye ni mmoja wa makipa waliovuma nchini Uingereza.Ramsdale si wa kwanza kuwa mchezaji katika familia yake.

Amefuata nyayo za babake Nick aliyekuwa mtimkaji wa mbio za mita 400 kuruka viunzi, naye mamake Caroline alikuwa mchezaji wa netiboli.Safari ya Ramsdale katika ulingo wa soka ilianza akiwa na umri wa miaka saba.

Kipa huyo, kwa jina la utani Ramsy, alipata kunoa talanta yake katika shule ya makipa ya Fred Barber, shule ya upili ya Sir Thomas Boughey na akademia ya Marsh Town na pia Bolton Wanderers.

Alikuwa Bolton kwa kipindi kirefu cha miaka mitano. Hata hivyo, kimo chake hakikuridhisha Bolton na ikamuachilia.Klabu nyingine kadhaa pia zilimkataa kwa sababu ya kukosa kuwa na urefu mzuri.

Alitiwa moyo na wazazi wake pamoja na nduguze Oliver na Edwards kuendelea kutafuta kuwa kipa.

Vyakula maalum vilimsaidia kuongeza umbo lake. Muda si muda Sheffield ilipiku Huddersfield katika kuwania huduma zake. Ilimpa udhamini wa kusoma na kuendeleza talanta yake ya ukipa.

Kandarasi ya kwanza ya soka ya malipo aliyotia saini ilikuwa Julai 2016 akijiunga na timu ya watu wazima ya Sheffield United, kutoka ile ya wachezaji wasiozidi miaka 18.

Alikaa ugani Bramall Lane kwa miezi sita, ikiwemo kuanza maisha katika timu ya watu wazima kwa ushindi wa 6-0 dhidi ya Leyton Orient mnamo Novemba 2016.

Sheffield, ambayo wakati huo ilikuwa katika ligi ya daraja ya tatu, iliuzia Bournemouth mnyakaji huyo kwa Sh150 milioni pekee mnamo Januari 2017. Bournemouth ilikuwa Ligi Kuu (EPL) wakati huo.

Baada ya kuona hachezeshwi ugani Dean Court, Ramsdale aliitisha waajiri wake ruhusa ya kutafuta klabu ya daraja ya chini ili apate uzoefu. Alipelekwa Chesterfield kwa mkopo wa miezi mitano msimu 2017-2018.

Miezi saba iliyofuata, alikuwa kambini Bournemouth kabla kujiunga na AFC Wimbledon kwa mkopo wa miezi mitano msimu 2018-2019.Ramsdale alirejea ugani Dean Court msimu 2019-2020 na kuwa kipa nambari moja wa Bournemouth.

Alinyakuliwa na Sheffield kwa Sh2.6 bilioni baada ya msimu mgumu na Bournemouth, aliyoichezea michuano 37 ikishushwa ngazi kwa kumaliza EPL ndani ya mduara hatari.

Mambo pia hayakuwa mazuri kwake msimu 2020-2021 wakati Sheffield ilitemwa kutoka EPL.

Wachanganuzi wa soka pamoja na mashabiki walikosoa Arsenal vikali ilipoamua kumsaini kwa karibu Sh3.6 bilioni mwezi Agosti, kwa kandarasi itakayokatika Juni 2025.

Hata hivyo, wengi wamelazimika kufyata ndimi zao ugani Emirates baada ya Ramsdale kuandikisha ushindi mara nne mfululizo.

Kocha Mikel Arteta aliamua kumpa fursa ya kuanza mechi baada ya Mjerumani Bernd Leno kupoteza michuano ya kwanza ya ligi dhidi ya Brentford, Chelsea na mabingwa watetezi Manchester City kwa jumla ya magoli 9-0.

Matunda ya kuamua kutupa Leno kitini na kumtumia Ramsdale yamekuwa yakionekana.

Mabao ya Emile Smith Rowe, Pierre-Emerick Aubameyang na Bukayo Saka pamoja na kazi safi michumani ilishuhudia Arsenal ikizima maadui wao Tottenham 3-1 katika Debi ya North London wikendi ya Septemba 26.

Vijana wa kocha Nuno Espirito Santo walikuwa wamepigiwa upatu kulemea Arsenal.Kwa sasa, vita vya kipa nambari moja ugani Emirates kati ya Ramsdale na Leno vinaonekana kuegemea upande wa Mwingereza huyo.

Kimataifa, Ramsdale anawakilisha Uingereza. Alikuwa katika kikosi cha Kombe la Euro 2020 kujaza nafasi ya majeruhi Dean Henderson, lakini sasa anabisha kuonja mechi yake ya kwanza.

Hii ni baada ya kocha Gareth Southgate kumjumuisha katika kikosi kitakachovaana na Andorra (Oktoba 9) na Hungary (Oktoba 12) kwenye kampeni za kufuzu kwa Kombe la Dunia nchini Qatar 2022.

Inakisiwa yeye hula mshahara wa Sh6.4 milioni kila wiki (Sh335 milioni kila mwaka) ugani Emirates.

You can share this post!

UDAKU: Jicho kali la nje laponza kocha mwenye tamaa ya fisi

DIMBA NYANJANI: Huyu ‘Mbappe’ wa Young Bulls atisha...