DIMBA: Ruby: Beki mtulivu akiwa na boli na mkali wa kupangua wapinzani

DIMBA: Ruby: Beki mtulivu akiwa na boli na mkali wa kupangua wapinzani

Na GEOFFREY ANENE

RUBEN dos Santos Gato Alves Dias ni mmoja wa wachezaji matata wanaotarajiwa kung’ara katika Ligi Kuu ya Uingereza msimu 2021-2022 itakayong’oa nanga Agosti 13.

Raia huyo Ureno ni beki wa kati wa Manchester City. Yeye ni mmoja wa mabeki walionunuliwa na City miaka ya hivi majuzi ikisaka kujaza pengo kubwa lililoachwa katika idara ya ulinzi baada ya gunge Vincent Kompany kuondoka Mei 2019.

Beki huyo wa kati, ambaye alianza uchezaji wa soka akiwa mshambuliaji kabla ya kufanya majukumu ya kiungo na kisha kuridhika na kazi ya kuwa beki, alijiunga na Cityzens mwezi Septemba 2020 kutoka Benfica.

Aliridhisha kocha Pep Guardiola katika msimu wake wa kwanza ugani Etihad. Mhispania huyo alimtumia katika michuano 50 katika mashindano yote. Akishirikiana na Mhispania-Mfaransa Aymeric Laporte, Dias alikuwa mwamba katika ngome ya City.

Kazi yake nzuri ilishuhudia akijumuishwa pamoja na mshambuliaji Dominic Calvert-Lewin (Everton), kiungo mvamizi Phil Foden (Manchester City), kipa Ilan Meslier (Leeds), kiungo mshambuliaji Mason Mount (Chelsea), Marcus Rashford (Manchester United), beki Declan Rice (West Ham) na beki wa kupanda na kushuka Bukayo Saka (Arsenal) katika orodha ya wawanizi wa tuzo ya mchezaji bora chipukizi kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu uliopita. Muingereza Foden aliibuka mshindi.

Ruby, ambaye amechezea timu ya taifa ya Ureno mara 32 ikiwemo nne katika Kombe la Euro 2020 lililokamilika karibu mwezi mmoja uliopita, alizaliwa jijini Lisbon mwezi Mei 14 mwaka 1997.

Alianza safari ya kuwa mwanasoka akiwa na umri wa miaka tisa alipojaribiwa na kufuzu kuingia akademia ya Estrela da Amadora mwaka 2006. Miamba wa Ureno Benfica walimnyakua mwaka 2008.

Alichezea timu ya pili ya Benfica (B) mechi ya kwanza mnamo Septemba 2015 akiwa na umri wa miaka 18.

Kisha, alijumuishwa kwa timu ya watu wazima ya Benfica kwa mechi ya Klabu Bingwa Ulaya mnamo Machi 9 mwaka 2016 dhidi wenyeji Zenit Saint-Petersburg ambayo ilikuwa ya raundi ya 16-bora kwa sababu mabeki watatu kati ya wanne hawakuweza kusafiri hadi nchini Urusi.

Alipiga hatua nyingine katika timu ya watu wazima ya Benfica alipoanzishwa kwa mara ya kwanza katika mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Boavista. Kwa miezi miwili ilifuata, Ruby alisakata soka ya kupendeza zikiwemo dhidi ya Manchester United kwenye Klabu Bingwa Ulaya mnamo Oktoba 2017. Alichezea Benfica zaidi ya mechi 100 katika mashindano yote ikiwemo kushinda nayo Ligi Kuu kabla ya kunyakuliwa na City kwa ada ya Sh9.2 bilioni.

Ruby amejitokeza kuwa mchezaji muhimu uwanjani Etihad. Amehusika katika kuzima mashambulizi ya wapinzani na pia kuunganisha mashambulizi ya timu yake. Ameonekana mtulivu akiwa na mpira na pia ni mzuri katika kusoma wapinzani wanavyopanga mashambulizi yao. Nguvu zake pia zimejitokeza wakati timu imewekewa presha.

Vilevile, ni mwerevu katika anavyojipanga uwanjani na kufanya kazi yake. Akiwa Benfica alikuwa akisababisha ikabu nyingi. Hata hivyo, ameshughulikia suala hilo ilivyoshuhudiwa ikabu zikipungua ugani Etihad kwa kumakinika zaidi.

Katika kandarasi yake itakayokatika Juni 2026, Ruby anaaminika kupokea mshahara wa Sh14.8 milioni kila juma (Sh771.9 milioni kila mwaka).

Mchezaji huyo anachumbia mwanamuziki kutoka Ureno, April Ivy, ambaye majina yake kamili ni Marianna Goncalvez. Ruby ni mtoto wa tatu katika familia ya watoto wanne.

You can share this post!

Siku 365 za kufa kupona

UDAKU: Huyu Neymar hapoi, amedakia Bruna kabla Natalia...