DIMBA: Sambi Lokonga: kizibo tosha cha safu ya kati ya The Gunners!

DIMBA: Sambi Lokonga: kizibo tosha cha safu ya kati ya The Gunners!

Na GEOFFREY ANENE

CHIPUKIZI Albert-Mboyo Sambi Lokonga ni kiungo anayeinuka kimchezo kwa haraka katika ulimwengu wa soka ambaye sasa ni mali ya wanabunduki wa Arsenal.

Kocha Roberto Martinez amelinganisha kinda huyo kimchezo na nyota wa Borussia Dortmund Axel Witsel.

Sambi alizaliwa Oktoba 22, 1999 jijini Brusseles. Amekuza uanasoka wake katika klabu mbili.

Alianzia uchezaji wake katika kituo cha kukuza talanta cha Verviers kabla ya kujiunga na akademia inayosifika nchini Ubelgiji ya Anderlecht mwaka 2010.

Anatoka katika familia ya wachezaji. Ndugu yake Paul-Jose M’Poku,29, ni mshambuliaji katika klabu ya Konyaspor nchini Uturuki.

Binamu yake Eliezer Mpoku, 19, ni kiungo mkabaji wa Uswizi.

Ana asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambako wazazi wake Josee na Desire Lokonga walitoka.

Sambi alisaini kandarasi yake ya kwanza ya soka ya malipo na Anderlecht mnamo Novemba 2017.

Alisakatia timu ya watu kwa mara ya kwanza mwezi mmoja baadaye ikichapa Eupen 1-0 Desemba 22.

Alichezea Anderlecht jumla ya michuano 85 kutoka msimu 2017-2018 na kuchangia magoli manne na pasi nane zilizozlisha mabao kabla ya Arsenal kumnunua kwa Sh2.2 bilioni juma lililopita (Julai 19).

Kandarasi yake ni miaka mitano ugani Emirates. Itakatika Juni 30, 2026.

Sababu kubwa ya Arsenal kusaini Mbelgiji huyo ni kuwa klabu hiyo kutoka jijini London inalenga kuimarisha safu ya kati. Hii ni baada ya Matteo Guendouzi kuelekea Marseille, Dani Ceballos na Martin Odeggaard kurejea Real Madrid nao Lucas Torreira na Granit Xhaka wanataka kuyoyomea Italia.

Sambi anaingia katika safu iliyo na viungo wakabaji Thomas Partey, Xhaka, Torreira, Mohamed Elneny na kiungo wa kati Joe Willock.

Anatarajiwa kutumiwa zaidi kumpa ushindani kiungo mkabaji Partey ama pia kushirikiana na raia huyo wa Ghana.

Baadhi ya vyombo vya habari Uingereza vinaamini alinunuliwa kuwa kizibo cha Xhaka.

Hata hivyo, Sambi atakuwa na kibarua kigumu kufikia kiwango cha Mswizi huyo anayemezewa mate na Roma ya kocha Jose Mourinho.

Kabla ya kuwa mali ya Arsenal, Sambi alitumiwa zaidi katika misimu miwili iliyopita na hata kufanywa nahodha.

Alichezeshwa mara 26 msimu 2019-2020 kabla ya msimu huo kufutiliwa mbali kutokana na kuvurugwa kabisa na mkurupuko wa virusi vya corona. Mchango wake ulikuwa mkubwa zaidi msimu 2020-2021 alipotumiwa katika michuano 37, ikiwemo 27 ya Ligi Kuu, katika mashindano yote na kufunga mabao matatu pamoja na kumega pasi mbili zilizozalisha magoli.

Alipata bao lake la kwanza akichezea timu ya watu wazima ya Anderlecht lilipatikana katika sare ya 1-1 dhidi ya Eupen mnamo Septemba 27, 2020.

Sambi anawakilisha Ubelgiji kimataifa. Amechezea timu ya taifa ya Ubelgiji ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 17 hadi 21.

Aliitwa kwa mara ya kwanza kuchezea timu ya watu wazima ya Ubelgiji kwa mechi ya kirafiki dhidi ya Ugiriki mnamo Juni 3. Hakutumiwa katika mchuano huo uliotamatika 1-1.

Pia, alijumuishwa katika kikosi cha Martinez cha Kombe la Euro 2020, lakini hakutumiwa. Albert anatumia zaidi mguu wake wa kulia.

Nguvu zake ni katika kusuka pasi, chenga, makombora ya kutoka mbali na kuiba pasi za wapinzani.

Ulegevu wake uko katika kusababisha ikabu nyingi pamoja na kuchelewa katika kufanya uamuzi.

Kocha wake wa zamani Vincent Kompany pia anasema Sambi, ambaye pia amesifiwa sana na nyota wa zamani wa Arsenal Thierry Henry, anafaa kuimarisha ulinzi na kushinda makabiliano.

Albert atavalia jezi nambari 23 iliyovaliwa na beki raia wa Brazil David Luiz kabla ya kandarasi yake ikatike msimu uliopita. Sambi anasemekana alipokea mshahara wa Sh2.9 milioni kila wiki kambini Anderlecht.

Baada ya kujiunga na Arsenal, kitita kinaaminika kimeongezeka kufikia karibu maeneo ya Sh5.0 milioni kwa juma. Kocha Mikel Arteta alisifu Sambi alipomnunua ikiwemo kusema ni mchezaji “mwerevu aliyeonyesha ukomavu mkubwa katika ukuaji wake”.

You can share this post!

Peaty aweka historia ya kuwa Mwingereza wa kwanza kuhifadhi...

GUMZO: Wanasema Werner amechoka kusugua benchi ya Chelsea