Michezo

DIMBA: Si siri tena! Neymar ala bata na Natalia

March 2nd, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

FOWADI mahiri wa Paris Saint-Germain (PSG) na timu ya taifa ya Brazil, Neymar Jr, hachoki kupenda!

Nyota huyo, 28, ambaye pia amewahi kuvalia jezi za Barcelona, sasa amejinasia penzi la mwanamitindo mzawa wa Cuba, Natalia Barulich, 28.

Neymar na Natalia wanaanza kutoka kimapenzi mwaka mmoja baada ya kipusa huyo raia wa Croatia, kutemana na mumewe Maluma.

Maluma ni mwanamuziki maarufu mzawa wa Colombia, aliyewahi kunogesha hafla ya Neymar wakati akiadhimisha miaka 27 ya kuzaliwa.

Wiki iliyopita staa huyo alionekana akiponda raha na Natalia, ambaye duru zinasema pia anawaniwa na mwanasoka wa zamani wa Chelsea, John Terry, 39.

Tangu atemane na Maluma, Natalia amekuwa mwepesi wa kupakia picha za Neymar mtandaoni, akiambatisha jumbe zinazoashiria kuwepo kwa mapenzi kati yao.

“Kila mtu anafahamu ustadi wa kipaji chako uwanjani, ila wangejua ulivyo mtamu na ndani pia. Unazo heshima zangu zote mpenzi!” akaandika Natalia huku akitia alama za kuashiria mabusu motomoto mwishoni mwa ujumbe huo.

Katika picha nyingine, Natalia alikuwa amevalia rinda jeupe ambalo alifichua kwamba lilinunuliwa na straika huyo mahiri mwishoni mwa mwaka jana walipokutana katika hafla moja jijini Rio, Brazil.

“Rinda hili ni zawadi tosha kutoka kwa Neymar, dume ambalo nalistahi sana kwa pendo la kweli,” akasema demu huyo.

Aidha, kidosho huyo amemtaka Neymar kukomesha kabisa mawasiliano ya mara kwa mara na wanamitindo Izabel Goulart na Alsessandra Ambrosio, waliowahi kumgawia tunda mwanzoni mwa 2019 jijini Dusseldorf, Ujerumani.

Neymar anaanza kumtambalia Natalia kimapenzi miezi michache baada ya kutengana na mwigizaji maarufu mzawa wa Mexico, Danna Paolo, 24.

Danna alikuwa kiini cha kuvurugika kwa uhusiano wa miaka sita kati ya Neymar na kichuna Bruna Marquezine, 24.

Awali, Neymar alikuwa akila bata na mwanamitindo Mari Tavares kabla ya kukiri kuvutiwa na maungo ya Ellen Santana, aliyetawazwa mshindi wa Miss BumBum nchini Brazil mnamo 2018.

Ni miezi sita tu imepita tangu nyota huyo atemane pia na mwanamitindo Noa Saez, aliyekuwa mwenyeji wake wa mara kwa mara katika mkahawa wa Mr Porter jijini Catalonia, Uhispania.

Noa aliingia katika orodha ndefu ya vichuna wa Neymar baada ya sogora huyo kutomasa pia matunda ya warembo Liza Brito kutoka Uswizi na Larissa ‘Anitta’ Macedo wa Brazil.