Makala

'Dimbwi la Clayworks lingali tishio kwa wakazi'

October 31st, 2019 2 min read

Na SAMMY WAWERU

BARABARA kuu ya Thika Superhighway kwa kawaida huwa ni yenye shughuli nyingi, hasa za usafiri na uchukuzi.

Pembezoni mwa barabara hiyo eneo la Clayworks, Kaunti ya Nairobi na kati ya mtaa wa Kasarani na Githurai, kuna dimbwi ambalo si la kilimo, uvuvi wala kujivinjari kwa kuogelea.

Duru zinaarifu kuwa awali halikuwepo na kwamba lilijiri kupitia uchimbaji na uundaji wa matofali, eneo hilo ‘Clayworks’ likipata jina kupitia shughuli hizo.

Licha ya kuwa matofali yanatumika katika ujenzi na kupunguza gharama, timbo hilo sasa limekuwa kitekeo cha maji yasiyokauka msimu wa kiangazi. Limeunda kidimbwi, ambacho kwa wakazi wa eneo la Clayworks na mitaa jirani ni kiini cha mauti.

Taswira ya mandhari eneo la Clayworks pembezoni mwa Thika Superhighway. Picha/ Sammy Waweru

Hata ingawa kimo chake hakijulikana, Antony Wa Wanjiru mkazi wa Githurai anasema si kisa kimoja au viwili watu wameripotiwa kuuawa humo. “Ni dimbwi la mauti, ni hatari kwa wapitanjia. Watu hupigwa ngeta na kurushwa humo,” asema Antony.

Miili hutolewa katika kidimbwi hicho mara kwa mara, kisa cha hivi karibuni kikiwa cha mwezi Juni mwaka huu.

Mwaka 2018 matatu iliyodaiwa kuwa na abiria 18 iliripotiwa kutumbukia humo.

Shughuli za kuokoa manusura ziligonga mwamba kwani tukio hilo lilifanyika mwendo wa saa mbili za jioni.

Aidha, wakazi waliandamana wakilalamikia kujikokota kwa serikali kuingilia kati suala hilo.

Licha ya kuwa matatu yenyewe ilitolewa angalau si miili yote iliyoopolewa.

Ni shughuli iliyohusisha maafisa wa kijeshi, KDF, wa kupiga mbizi kuokoa manusura majini.

Kufuatia tukio hilo, mengi yaliibuka baadhi ya watu wakijitokeza na kufichua kwamba wamepoteza wapendwa wao katika kidimbwi hicho.

Mbunge wa Ruiru Simon King’ara aliagiza nguzo kando mwa barabara – guard rails – ziwekwe katika sehemu hiyo. Na hilo bila shaka liliafikiwa.

Taswira ya mandhari eneo la Clayworks pembezoni mwa Thika Superhighway. Picha/ Sammy Waweru

Isitoshe, Agosti 2019 kilizingirwa kwa ua wenye nyaya za nguvu za umeme.

Baadhi ya wakazi wanakosoa hatua hiyo wakisema si suluhu la maafa yanayoshuhudiwa humo.

“Halina manufaa yoyote kwetu kwa kuwa hata halitumiki kufanya kilimo. Tunaomba kifunikwe,” mkazi akaambia Taifa Leo.

Inadaiwa ardhi ambako kuna kidimbwi hicho inazozaniwa. Wakati wa kuweka ua, makundi mawili hasimu yalikabiliana vikali.

Ililazimu maafisa wa polisi kusimamia shughuli hiyo.

Kidimbwi hicho pia kinadaiwa kuwa na joka.

Kwa wapita njia, si salama saa za jioni na usiku ambapo wengi wamejipata kuandamwa na wahalifu na kurushwa humo.

Ili kizikwe, halmashauri ya kitaifa ya mazingira Nema, na wadau husika wanapaswa kutathmini faida na madhara yake. Pia, Nema ndiyo yenye mamlaka kuagiza kizikwe ili kuondoa hali ya kiwewe eneo hilo.

Taswira ya mandhari eneo la Clayworks pembezoni mwa Thika Superhighway. Picha/ Sammy Waweru