DINI: Akili yako itawaliwe na mawazo mema usiwe adui wa nafsi yako

DINI: Akili yako itawaliwe na mawazo mema usiwe adui wa nafsi yako

NA PADRE FAUSTIN KAMUGISHA

Tumezoea kusema, “nipishe nipite,” kama kuna watu wameziba njia au wanakuzuia kupita. Lakini wakati mwingine unaweza kujizuia mwenyewe kupiga hatua maishani.

Unaweza kuwa mchawi wa maendeleo yako mwenyewe. Adui wa mtu ni mtu mwenyewe. Unaweza kujiharibia mambo mazuri, nafasi ya kazi, fursa ya mafanikio, ndoa yako mwenyewe, kutaja machache.

Katika msingi huo tunasema, jipishe, upite. Usijizuie, usijiharibie, usijiripue. Mtu anaweza kujenga nyumba au familia yake mwenyewe, lakini anaweza kuibomoa kwa mikono yake.

“Kila mwanamke mwenye hekima huijenga nyumba yake, kila mpumbavu hubomoa kwa mikono yake” (Mithali 14: 1). “Ushindi wa kwanza na mzuri sana ni kujishinda; nafsi yako kukushinda ni jambo la aibu sana na linalotia kichefuchefu kati ya mambo yote,” alisema mwanafalsafa wa Kigiriki Plato.

Jipishe, jishinde.Mawazo yako mabaya yanakuzuia kwenda mbele. Jipishe, upite. “Mpaka wakati gani mawazo mabaya yatakaa katika kifua chako?” (Yeremia 4: 14).

Jiwazie mazuri na jiwazie mawazo chanya. Jipishe. Mzee Theophilius Siwezi alimtembelea Mzee Musa Mtokambali aliyekuwa na mafanikio makubwa.

Katika kuongea kwake Mzee Theophilius Siwezi alisema,“Kila ninachokifanya sifanikiwi. Kila ninalolianzisha halifanikiwi. Ni kama mgongoni nimeandikwa neno HAPANA kwa herufi kubwa.”

Huyu hakuwaza mazuri. “Mawazo mazuri ni wageni wenye baraka wapokolewe kwa moyo mkunjufu, walishwe vizuri na watafutwe. Kama majani ya mawaridi yanatoa harufu nzuri kama yatawekwa kwenye jagi la kumbukumbu,” alisema mchungaji Charles H Spurgeon.

Yakaribishe vizuri mawazo mazuri kama unavyomkaribisha mgeni mwenye matashi mema. “Wewe ni jumla ya mawazo yanayotawala au yanayoongoza zaidi,” alisema Napoleon Hill.

Mawazo chanya yatawale. Mawazo mwanga yatawale. Mawazo mazuri yatawale.Tuliza akili. “Tumieni akili kama ipasavyo” (2 Wakorintho 15:34).Bwana Musa Mawese alitaka kuweka gia ya kurudi nyuma kwenye gari. Aliteremsha kioo cha gari na kuwaambia waliokuwa nyuma ya gari, “nipishe, nipite.”

Aligeuza shingo na kutazama nyuma na kuchochea moto. Bahati mbaya alikuwa ameweka gia namba moja. Aligonga ukuta. Mawazo yalikuwa mbali. Hakutuliza akili. Kusema kweli baada ya kusema, “Nipishe nipite,” angejiambia, “Jipishe, upite.”Nani amekuzuia kujiamini? Jipishe.

“Kama nimekosa kujiamini nina ulimwengu wote kinyume changu,” alisema Emerson. Nani amekuzuia kujifunza somo kutokana na ulichokipoteza? Jipishe.

“Ukipoteza usipoteze somo,” alisema Dalai Lama. Nani amekuzuia kuchapa kazi? Jipishe. “Akili yenye uvivu ni mahali pa kucheza pa Shetani,” alisema Napoleon Hill. Nani anakuzuia kuwa mkarimu? Jipishe.

“Unavyogawana zaidi ndivyo unapata zaidi,” alisema Napoleon Hill. Nani amekuzuia kutazama mambo vizuri kwa mtazamo chanya? Jipishe. “Kama ukibadili namna ya kutazama mambo, mambo unayoyatazama yanabadilika,” alisema Wayne Dyer.Nani amekuzuia kusimama kama ulianguka jana? Jipishe.

“Kama ulianguka jana, simama leo” (H.G. Wells). Nani amekuzuia kuwa na mpango mkakati wa maisha yako?Jipishe. “Usipopangilia maisha yako, uwezekano ni kuwa utaingia kwenye mipango ya watu wengine. Na unatabiri nini walichokupangia? Sio kikubwa” (Jim Rohn).Nani amekuzuia kukimbia?

Swala akimuona simba anasali, “Mungu okoa maisha yangu.” Anakimbia. Simba akimuona swala anasali, “Mungu nisaidie nipate chakula hiki.” Anakimbia kufukuzia. Jipishe. Kimbia.

Kumbuka anayetubu ni mdhambi anayeikimbia dhambi. Huko ni kukimbia ambako ni kuzuri. Anayetenda dhambi ni mdhambi anayeikimbilia dhambi. Jipishe, ikimbie dhambi.

Nani amekuzuia kutabasamu? Jipishe. Nani amekuzuia kunyenyekea ili ule vya watu na Mungu? Jipishe. Nani amekuzuia kwenda kwenye ibada? Jipishe. Nani amekuzuia kutoa sadaka ya noti badala ya chenji?Jipishe. Nani amekuzuia kupenda watu? Jipishe. Nani amekuzuia kuwatendea watu mema? Jipishe

You can share this post!

Mzee aliyerushwa nje ya SGR apatikana hai siku 4 baadaye

Ruto aonywa asifurahie masaibu ya Rais Uhuru