DINI: Hakuna majira wala hali inayodumu milele, weka matumaini kwa Mungu

DINI: Hakuna majira wala hali inayodumu milele, weka matumaini kwa Mungu

Na WYCLIFF OTIENO

JANE alifanikiwa kupata watoto wawili wa kiume.

Ndoto yake ya kupata mtoto wa tatu, na haswa wa kike ilikatizwa mumewe alipohusika katika ajali ya barabarani na kupoteza maisha yake.

Wakweze hawakumpenda. Walimnyang’anya kila kitu na kumfukuza nyumbani kwa kisingizio kuwa alikuwa mke mwenye kisirani na mshirikina.

Maisha yakawa magumu sana. Alitegemea vibarua kukimu mahitaji yake. Aliishi katika kitongoji duni mjini Nairobi, akifanya kazi ya kuwafulia watu nguo, na pia kazi za nyumba. Alifanya bidii kuwalea wanawe na kuwapeleka shuleni akiwa na matumaini kuwa wangemsaidia siku zijazo.

Mwanawe wa kwanza alikuwa mwerevu sana. Alikuwa na ndoto ya kusoma awe daktari. Lakini mwana wa pili alilemewa na masomo hata akaacha shule katika kidato cha pili. Tumaini la Jane likawa kwa mwana wa kwanza.

Lakini kwa bahati mbaya, siku ya mwisho ya mtihani wa Kidato cha Nne, kijana alizimia shuleni na kuaga dunia.

Jane alikosa matumaini kabisa. Alijiona kweli mwenye laana. Alitamani kujitoa uhai. Alitamani heri Mungu angemchukua mwanawe wa pili, aliyekataa masomo badala ya huyu wa kwanza. Aliyekuwa tumaini lake.

Lakini mipango ya Mungu si kama ya mwanadamu. Yule kijana wa pili, licha ya hali yake, Mungu alimbariki na akafanikiwa sana katika biashara.

Baada ya miaka kadhaa, alimnunulia mamake shamba na kumjengea jumba la kifahari. Hivyo, ukumbuke hata majira marefu na magumu yana mwisho wake.

Biblia Takatifu linasema katika Mhubiri 3:1, “Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu. Kila majira yana mwisho wake.”

Kila majira yana faida zake. Sio kwamba unapopitia hali ngumu ni ishara kuwa umemkosea Mungu. Ni majira tu. Hakika yatapita.

Usikate tamaa kwa sababu ya majira unayoyapitia. Usifanye uamuzi mbaya utakaokufanya usione majira yajayo. Majira magumu yanatufanya tuweke tumaini letu kwa Mungu. Yeye habadiliki na ahadi zake hudumu milele.

Majira magumu yanatuhitaji kuwa na Imani. Unapojua huna uwezo wa kusuluhisha jambo, unamgeukia yeye aliye na uwezo.

Majira unayopitia leo ni uwanja wa matayarisho kwa majira yajayo. Ni muhimu kuangalia majira kwa mtazomo chanya. Wakati wa ukame, liandae shamba lako. Weka mbegu yako tayari maana majira ya mvua yanakaribia.

Kukataliwa ni majira. Watu wanaweza kukukataa wakati utukufu wa Mungu haujadhihirika maishani mwako. Lakini ni majira tu. Usikate tamaa. Hakuna aliyekubalika kabla hajakataliwa.

Mungu atakapobadilisha majira, utaheshimika na kukubalika tu.

Kama umebarikiwa na kazi na unapata mshahara, fikiria kuhusu kuweka akiba. Usitumie kila unachopata. Hiyo si hekima. Wekeza, weka akiba. Wabariki watu. Hayo ni majira na yatapita. Ukijipata katika majira ya kukosa kazi na ukame mfukoni, utafanya nini kama hukutumia fursa yako vizuri?

Ukiwa na afya njema, fanya kazi kwa bidii. Tumia majira hayo vizuri. Wahurumie wale hawana afya njema. Wasaidie wanaohitaji msaada. Hiyo ni mbegu unapanda ili utakapojipata katika majira ya kukosa afya, upate watu wa kusimama nawe. Mungu hadhihakiwi, mtu huvuna anachopanda.

Ukiwa mgonjwa usikate tamaa. Ni majira tu na yatapita. Jiandae kimawazo. Jiulize majira hayo yakipita utamfanyia nini Mungu? Majirani na wanadamu utawafanyia nini? Utahusika vipi kuboresha maisha yako na ya wengine?

Kuna dada rafiki yangu alikuwa mgonjwa karibu kufa. Nilipomtembelea hospitalini, aliniambia anaomba Mungu akimponya atamtumikia milele. Mungu alimponya na sasa ni mchungaji. Anamtumikia Mungu kwa moyo wake wote.

Mefiboshethi alikuwa kiwete na alijiona kama mbwa, lakini Daudi alipotaka kuiheshimu nyumba ya Sauli, ni yeye tu alipatikana. Akainuliwa na kula pamoja na mfalme na kurudishiwa mashamba yote ya Sauli.

Mhubiri 3:11 inasema, Kila kitu amekifanya kizuri kwa wakati wake; tena ameiweka hiyo milele ndani ya mioyo yao; ila kwa jinsi mwanadamu asivyoweza kuivumbua kazi ya Mungu anayoifanya, tangu mwanzo hata mwisho.

Unayoyapitia ni majira. Yatapita tu. Weka tumaini lako kwa Mungu. Jiandae kwa majira yajayo, maana hakika yaja!

You can share this post!

Fidu aahidi makubwa kwa mashabiki wa Changamwe Ladies

Mlima wateleza kwa Ruto, Raila