DINI: Hata kama hatumwoni, Bwana Mchungaji Mwema huwa nasi hata wakati wa mateso

DINI: Hata kama hatumwoni, Bwana Mchungaji Mwema huwa nasi hata wakati wa mateso

NA PADRE FAUSTIN KAMUGISHA

Mungu ni mchungaji mwema. Anajali. Ana huruma. Anakumbuka. Hakuachi. Anakupenda. Yesu ni mchungaji mwema. Lakini huenda hauoni wema wa mchungaji mwema.

Huwezi kuandika bango kwenye ndoa yako kuwa ndoa hii haina matatizo. Mateso yamejipanga foleni. Kazi uliyoipata umesimamishwa. Mchumba uliyetaka kumuoa amechukuliwa.

Vipi kama huoni wema wa mchungaji mwema? Nakubaliana na Peter Marshall, aliyesema, “Mungu hataruhusu matatizo yatupate, isipokuwa kama ana mpango maalumu ambapo neema kubwa itatoka kwenye jambo gumu.” Inasemwa, “Bwana ndiye mchungaji wangu, Sitapungukiwa na kitu” (Zaburi 23:1).

Huenda huoni wema wa mchungaji mwema. Wakati kuna mawingu jua halionekani lakini lipo. Ingawa kuna matatizo, Mungu mchungaji mwema yupo.Vipi kama mchungaji mwema hazuii mateso?

Mungu hakumzuia Yosefu asitupwe kwenye shimo. Mungu hakumzuia Yosefu asiuzwe kama mtumwa. Mungu hakuzuia mke wa Farao asimsingizie Yosefu. Lakini hao wote walimsogeza Yosefu kwenye wito wake.

Hayo yote yalikuwa sehemu ya mchakato na mpango wa Mungu. Mungu hakumzuia Danieli asitupwe kwenye shimo la simba. Mungu hakuzuia Abednego, Meshaki na Shadraki wasitupwe kwenye tanuru la moto. Lakini Mungu alikuwa pamoja nao. “Kumbuka kuwa hata katikati ya mateso mapenzi ya Mungu yanatimizwa,” alisema Paul Chappell.

Mungu hakuzuia Wamisri wasiwafuate wana wa Israeli walipokuwa wanakimbia kutoka Misri. Mbele yao kulikuwa na bahari na nyuma yao kulikuwa na jeshi la Farao. Musa alimlilia Mungu. “BWANA akamwambia Musa, Mbona unanililia mimi? W

aambie wana wa Israeli waendelee mbele (Kutoka 14:15). Kama kuna mateso, endelea mbele.Vipi kama mchungaji mwema anajibu kinyume cha mategemeo? Unaomba kuwa padre Mungu anakukatalia, unaoa na mtoto wako anakuwa padre.

Unamchumbia msichana anakuacha anaenda kuwa mtawa. Unaomba lifti unanyimwa lifti. Unajibiwa kinyume cha mategemeo na mchungaji mwema. Lakini baadaye unagundua gari ambapo umenyimwa lifti limepinduka. Kuna aliyesema, “Baadhi ya zawadi kubwa sana za Mungu ni sala ambayo haikujibiwa.”

Bwana Felix wa Nola aliwakimbia maadui na kujificha kwenye pango. Akiwa kwenye pango alianza kusali na kumuomba Mungu amsaidie. Aliomba Mungu aweke zege kwenye lango la kuingilia kwenye pango. Ghafla aliona buibui anaweka utandu kwenye mlango. Alisema, “Mungu sikuomba utandu nimeomba zege.”

Baada ya buibui kumaliza kushona vizuri kwa utandu, maadui walifika pale walijiambia, “Hapa hajaingia mtu yeyote, kwa sababu utandu usingekuwepo.”

Wakaenda zao. Pamoja na Mungu utandu ni kama zege, bila Mungu zege ni utandu. Ukweli huu utusaidie, “Maana mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu; asema BWANA. Kwa maana kama vile mbingu zilivyo juu sana kuliko nchi, kadhalika njia zangu zi juu sana kuliko njia zenu, na mawazo yangu kuliko mawazo yenu” (Isaya 55:8-9).

Jibu la sala ambayo haijajibiwa ni Mungu anakulinda na matokeo mabaya. Hapana ya Mungu si kukatataa kwa Mungu bali ni kubadili mwelekeo wako na dira yako.

Vipi kama mchungaji mwema anachelewa kujibu? Kuna msichana peke kwa wazazi aliyesali hivi, “Leo Mungu sijiombei, namuombea mama yangu mpe mkwe mzuri wa sura na tabia. Amina.” Kusema kweli alikuwa anajiombea. Ilichukua miaka mingi kuolewa lakini Mungu alimjibu. “Kuchelewa kwa Mungu si kukataa kwa Mungu,” alisema mchungaji Robert Schuller.

Mungu anachelewa kwa lengo kubwa sana. Mungu anachelewa kwa vile unapoelekea kuna dhoruba. Anangoja dhoruba lipite. “Kuchelewa kwa Mungu si kukataa kwa Mungu. Kama jambo linachukua muda mrefu kuliko ulivyotegemea, amini kuwa Mungu anakuandaa,” alisema Victoria Osteen.

Ni kweli, “Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, kama wengine wanavyodhani anakawia, bali huwavumilia, maana hapendi mtu yeyote apotee, bali wote wafikie toba” (2 Petro 3:9).

You can share this post!

JAMVI: Mtihani wa IEBC 2022 vigogo wa siasa nchini...

Washukiwa 11 wa kundi la MRC waliokamatwa wachunguzwa