Habari Mseto

Dini kuondoa hitaji la mabinti kueleza iwapo ni mabikira

February 3rd, 2020 1 min read

FARHIYA HUSSEIN NA WINNIE ATIENO

WANAWAKE Waislamu sasa hawatahitajika tena kueleza kama wao ni bikira wanapojaza cheti cha ndoa.

Kadhi Mkuu Shariff Ahmed Muhdhar alieleza jana kuwa hitaji hilo katika cheti cha ndoa kati ya waumini Waislamu litaondolewa katika muda wa miezi sita ijayo.

Sheikh Muhdhar alisema hatua hiyo ni kufuatia malalamiko ya wanawake kuwa hitaji hilo lina ubaguzi kwani wanaume hawahitajiki kusema kama wao ni bikira.

“Kamati inayosimamia masuala ya ndoa miongoni mwa waislamu ilipata maoni ya waumini na kupendekeza hitaji hilo liondolewe. Wanawake wengi walisema si vizuri kutaja ubikira wao ilhali wanaume hawatajiki kufanya hivyo,” alieleza Sheikh Muhdhar.

Alisema kuwa wanawake walitaka swala la ubikira liwe kati ya wanandoa.

Kwa sasa tamaduni za kiislamu huwataka wanawake kutangaza ubikira wao kwenye cheti cha ndoa. Hii ni kwa mujibu wa itikadi ya dini ya kiislamu inayohimiza waumini kujizuia kushiriki ngono hadi ndoa.

Lakini uamuzi wa kuondoa hitaji la kufichua kama wewe ni bikira kwenye cheti cha ndoa umepingwa na baadhi ya waumini na viongozi.

Msomi wa dini ya Kiislamu, Bi Sofia Omar alisema kuwa kuwepo kwa sehemu hiyo kwenye hati za ndoa ni muhimu: “Ikiwa imetaja kama mwanamke ni bikira kwenye hati za ndoa basi itabidi mwanamke ajihifadhi na kujitunza mpaka atakapoolewa,” alisema Bi Omar.

Hata hivyo alipendekeza kuwa hati za ndoa pia ziwe na sehemu ya wanaume kusema kama wao ni bikira.

Kwa upande wake, Mratibu Mkuu wa Baraza la Maimamu Nchini (CIPK) Sheikh Mohammed Khalifa alisema kuwa viongozi wa dini wanafaa kuwa na kikao maalum na Kadhi Mkuu kabla ya suala hilo kupitishwa.

Naye Mwenyekiti wa Kitaifa wa Baraza la Ushauri wa Waislamu wa Kenya (Kemnac) Sheikh Juma Ngao alisema kuwa iwapo waumini wenyewe watasema sehemu hiyo iondolewe basi inafaa kufutwa.