DINI: Kupanga ni kuumaliza mwaka kabla hujauanza, panga makuu

DINI: Kupanga ni kuumaliza mwaka kabla hujauanza, panga makuu

Na FAUSTIN KAMUGISHA

KUPANGA ni kuvuka daraja kabla ya kulipita.

Kupanga ni kukata kanzu kabla mtoto hajazaliwa.

Kupanga ni kuhesabu mayai kabla ya kutagwa. Kupanga ni kuweka bati kwenye paa kabla ya mvua kunyesha. Kupanga ni kuchimba kisima kabla ya kuwa na kiu.

Ni kulima mazao ya chakula kabla ya baa la njaa. Kupanga ni kuzuia jambo baya kabla ya kutokea. Heri kuzuia kuliko kuponya. Hadhari kabla ya hatari. Kupanga ni kutabiri.

“Njia nzuri sana ya kutabiri wakati ujao ni kuumba,” alisema Stephen Covey. Kupanga ni kujiandaa.

“Kwa kushindwa kujiandaa, unajiandaa kushindwa,” alisema Benjamin Franklin.

“Ni nani kati yenu ambaye kama anataka kujenga, hatakaa kwanza na kufanya makisio ya gharama aone kama ana fedha za kutosha kukamilisha ujenzi? (Luka 14:28).

Kupanga ni kufikiria mapema jambo. Kupanga ni kufanya mipango. Kupanga ni kutayarisha ramani. Kupanga ni kunuia. Ni kudhamiria kufanya au kufanikisha jambo. Kupanga ni kupania. Kupanga ni kudhamiria.

Kupanga ni kukusudia. Kadiri ya Kamusi Kuu ya Kiswahili “panga” maana yake ni kufanya utaratibu wa jambo. Mpango ni utarartibu wa kufanya jambo kwa hatua ili kufikia lengo linalokusudiwa.

Mpango-dira ni utaratibu wa kina au mapendekezo yanayoonyesha namna kitu fulani kinavyotarajiwa kufanya kazi.

Kupanga ni kumaliza mwaka kabla hujauanza. Usianze mwaka ambao haujaumaliza kwenye karatasi. Usianze mwezi ambao haujaumalizia kwenye karatasi.

Usianze siku ambayo hujaimaliza kwenye karatasi.

“Kila mara panga kabla. Mvua ilikuwa hainyeshi Noa alipojenga safina,” alisema Richard Cushing.

Kesho ni ya watu wale wanaojiandalia kesho.

“Tunaishi chini ya mbingu ile ile, lakini hatuna upeo mmoja,” alisema Konrad Adenauer.

Kuna ambao wanapanga makubwa, na kuna ambao hawapangi.

“Mtu asiyepanga ya mbeleni, atakuta matatizo mlangoni,” alisema Conficius.

Kupanga ni kuishusha kesho na kuiingiza katika leo. Ni kufikiria leo wakati wa kesho.

“Usipofikiria juu ya wakati ujao, huwezi kuwa nao,” alisema John Galsworthy.

Kupanga ni kuifufua jana ikusaidie kupanga ya kesho. Kupanga kunahitaji kuwa na nyuso zaidi ya mbili.

Jina ‘Januari’ linatokana na jina la muungu wa Kirumi ‘Janu’ ambaye alikuwa na nyuso mbili, uso mmoja ukitazama yaliyopita na uso mwingine ukitazama yajayo.

Tunahitaji uso wa tatu wa kutazama ya leo, maana matunda ya kesho yako kwenye mbegu za leo.

Kesho inaanza leo. Kupanga kunahitaji kuitazama jana iliyozikwa kuzimuni, leo iliyo kwenye uso wa nchi na kesho iliyoko mawinguni.

Panga mipango mikubwa. Usifikirie madogo yanayolingana na kichuguu. Fikiria milima mikubwa.

“Usifanye mipango midogo, haina uchawi wa kusisimua damu za watu,” alisema Daniel Burnham.

“Mipango si chochote. Kupanga ni kila kitu,” alisema Dwight D Eisenhower.

Mpango ni jina au nomino dhahania, lakini kupanga ni kitenzi. Kupanga ni kutenda. Kupanga kunahitaji kufanyia kazi mpango.

“Matatizo ni mipango mingi iliyoegemea juu ya mambo yalivyo sasa. Ili kufanikiwa, mipango yako binafsi ifokasi kwenye kile ambacho unataka, si kile ulicho nacho,” alisema Nido Qubein, rais wa Chuo Kikuu cha High Point University.

Kuwa na mpango ‘A’’.

“Kama mpango ‘A’ haufanyi kazi, alfabeti ina bado herufi 25.

Kuwa na Mpango ‘A’, mpango ‘B’, mpango ‘C’ na kuendelea. Kuwa na maandalizi ya kushangaza.

“Mafanikio ya kushangaza yanatanguliwa na maandalizi ya kushangaza,” alisema Robert H Schuller, mwandishi wa vitabu na mhubiri mashuhuri.

Sasa hivi kuna mtu anayekula embe kwa sababu miaka 10 iliyopita, kuna ambaye alipanda mwembe.

Sasa hivi kuna mtu anayekata miti ya kujengea kwa sababu miaka 12 iliyopita kuna mtu aliyepanda msitu.

Tatizo kubwa ni kuwa hatupangi kushindwa, tunashindwa kupanga.

You can share this post!

MWANASIASA NGANGARI: Zacharia Onyonka alifariki kabla ya...

KINAYA: ‘Baba’ bado ni jogoo wa siasa licha ya...

adminleo