DINI: Lisheni akili zenu mawazo mazuri, fikra za tumaini na ndoto za ufanisi

DINI: Lisheni akili zenu mawazo mazuri, fikra za tumaini na ndoto za ufanisi

Na FAUSTIN KAMUGISHA

HERI kuanza umefungwa goli kuliko kumaliza umefungwa mabao kadha.

Mchezo wa maisha una kipindi cha kwanza na kipindi cha pili. Kipindi cha kwanza ni kipindi cha kutafuta na kipindi cha pili ni kile cha kuacha alama.

Heri kuanza na dhiki kuliko kumaliza nayo.

Wahaya wa Tanzania wana methali isemayo, zakuba ibanza eza amehereruka ishasa (heri kuanza na dhiki kuliko kumaliza na dhiki).

Kwa ujumla, ukifikisha miaka arobaini ni hafutaimu.

“Hafutaimu sio kukosekana kwa lile ambalo haukufanya, bali ni kukubali kushindwa kwako na kutambua unaishi kwa neema.” (Bob P. Buford).

Kama umeshindwa kipindi cha kwanza, usikate tamaa.

Mtume Paulo ambaye hakufanya vizuri kipindi cha kwanza cha mchezo wa maisha alisema, “Kwa hiyo, hatukati tamaa. Ingawa miili yetu inachakaa, utu wetu wa ndani unafanywa upya kila siku.” (2 Kor 4:16).

Unaweza kuanza kipindi cha pili cha mchezo wa maisha mwili umechakaa lakini moyoni na akilini wewe ni chipukizi.

“Miaka inaweza kufanya ngozi yako kuwa na mifunyo, lakini kutokuwa na shauku ya kitu chochote kunafanya roho iwe na makunyanzi. Wewe ni mdogo kama imani yako, na mzee kama mashaka yako; ni kijana kama kujiamini kwako, ni mzee kama kutamauka kwako. Katika kitovu cha kila moyo, kuna chumba cha kurekodi. Kikipokea ujumbe wa uzuri, matumaini, furaha na ujasiri unakuwa kijana. Moyo wako ukifunikwa na theluji ya kutazamia mabaya na barafu ya wasiwasi hivyo na hivyo tu unazeeka,” alisema Douglas MacArthur.

Lisha akili yako na mawazo mazuri na fikra ya matumaini, ndoto za maendeleo na mipango yenye kuleta furaha.

Katika Biblia, kuna watu wawili wanaitwa Saulo.

Saulo wa Agano la Kale alifanikiwa kipindi cha kwanza cha maisha. Kipindi cha pili hakufanikiwa. Saulo wa Agano Jipya ambaye anaitwa Paulo hakufanikiwa kipindi cha kwanza.

Kipindi cha pili, Mungu alimpa neema.

Alishirikiana na neema ya Mungu tofauti na mfalme Saulo ambaye hakushirikiana na neema ya Mungu.

Mtume Paulo aliandika, “Namshukuru Mungu kwa sababu ya neema” (1 Kor 1:4).

Kuna wakati niliongoza sala kabla ya kula sikutumia sala ya kawaida tunayotumia nilitunga ya kwangu.

Katika sala hiyo, nilishukuru neema Mungu anazotujalia. Mtoto mdogo wa umri wa miaka mitatu alimwambia mama yake. Padre Kamugisha anamjua rafiki yangu Neema. Suala kubwa si kuijua neema bali kushirikiana na neema ya Mungu. Mfalme Saulo alimaliza vibaya. Tunasoma hivi katika Biblia, “Ndipo neno la Bwana likamjia Samweli, kusema, “Najuta kwa sababu nimemtawaza Sauli awe mfalme; maana amerudi nyuma, asinifuate, wala hakufanya nilivyomwamuru” (1 Samweli 15: 10).

Saulo alianza kujitumikia badala ya kumtumikia Mungu. Alijijengea sanamu. Hakumtii Mungu, akatoa sababu (visingizio) ana mpango wa kumtolea Mungu sadaka tu.

Jibu alilipata, “Kutii ni bora kuliko dhabihu, na kusikia kuliko mafuta ya beberu” (1 Samweli 15: 22).

Kuna watu wanaalikwa kwa mambo ya Mungu, “Njoo kwenye mafungo. Njoo kwenye semina.Njoo kwenye ibada.” Mwingine anadharau na kusema, “Wanahitaji zaka.” “Wanahitaji sadaka wasitusumbue.” Saulo Paulo alimaliza vizuri: “Nimevipiga vita vilivyo vizuri” (2 Tim 4:7).

Kitu kikubwa kilichokosekana kwenye “sanduku” la Mfalme Saulo nacho ni ujasiri. Wakati ulipowadia wa kumfanya mfalme alijificha kwenye mizigo (1 Samweli 10: 22): “Tazama amejificha kwenye mizigo.”

Wachumba wanakuja unajificha. Fursa zinakuja unajificha kwa visingizio:sijavaa vizuri. Siendi kanisani nywele hazijakaa vizuri. Ukijificha fursa zinajificha. Ujasiri na woga vinaambukiza: Goliati alipowatishia watu wa Saulo walikimbilia kwenye mahema yao.

Watu wa Daudi walipambana na wenye nguvu hawakukimbia (2 Samweli 23: 8-12).

Ujasiri unakusaidia kufanya unaloogopa kufanya ( 1 Samweli 10:22).

Bila ujasiri tunakuwa watumwa wa kutojihisi salama. Saulo alimuogopa Daudi. Kila mtu ni kama analo “sanduku” palipo na vipaji vyake, fadhila zake, nguvu zake na uwezo wake.

Kwenye “sanduku” lako kuna nini na unavitumiaje: kipindi cha hafutaimu ya maisha ni kujihoji juu ya mambo hayo.

You can share this post!

De Bruyne, Foden kutochezea Man-City dhidi ya Spurs

Kiongozi wa upinzani nchini Zambia akaribia kuwa Rais