Makala

DINI: Matumaini ni mwanga kwenye giza na suluhu kwa msongo wa matatizo

July 19th, 2020 3 min read

Na FAUSTIN KAMUGISHA

ASKOFU Desmond Tutu wa Afrika Kusini ameelezea maana ya matumaini kwa mtazamo chanya.

Asema: “Matumaini ni kuweza kuona mwanga licha ya giza kote kote.”

Hata ukiwa kwenye matatizo, kuwa na matumaini. Matatizo ni giza la kukusaidia kuona nyota. Katika giza la matatizo unapasa kuwa na matumaini. Katika giza la corona, tuna matumaini ya kupatikana kwa tiba na wagonjwa kupona. Ukitembea usiku wenye giza, unaona nyota. Katika mtazamo huo, Louise Phillipe alisema: “Giza linapokuwa giza nene, nyota inaangaza sana.”

Petro anatutaka tuzungumzie matumaini yaliyo ndani mwetu.

“Muwe tayari kumjibu yeyote atakayewaulizeni juu ya matumaini yaliyo ndani yenu, lakini fanyeni hivyo kwa upole na heshima.” (1 Petro 3: 15-16). Tumaini lililo ndani yetu ni hili: Maisha pamoja na Yesu ni matumaini yasiyo na mwisho, bila yeye, ni mwisho usio na matumaini. Tumaini linaongea mazuri.

Watu wanapokwambia, “Kata tamaa,” matumaini yanasema, “jaribu tena.” Watu wanapokwambia, “nusu glasi haikujaa,” matumaini yanasema, “nusu glasi imejaa.” Watu wanapokwambia, “matatizo ni mengi,” matumaini yanasema, “yana mwisho.”

Watu wanapokwambia, “mlango wa kazi umefungwa,” matumaini yanasema, “Mungu anafungua mlango mwingine.” Watu wanaposema kuna hasi, matumaini yanasema, penye hasi kuna chanya. Watu wanaposema kuna kivuli, matumaini yanasema, penye kivuli kuna mwanga. Watu wanaposema pameinama, matumaini yanasema, painapo ndipo painukapo.

Watu wanaposema la kuvunda halina ubani, matumaini yanasema kwa Mungu la kuvunda lina ubani. Watu wanaposema maji yakimwagika hayazoleki, matumaini yanasema, kwa Mungu maji yakimwagika yanazoleka. Watu wanaposema kuna dhiki matumaini yanasema baada ya dhiki faraja. Watu wanaposema kesho haitabiriki, matumaini yanasema kesho itapendeza.

Watu wanapokusingizia na kusema una shtaka la kujibu, matumini yanasema, palipo na mshtaki kuna Mtetezi.

Kuna methali ya wamaasai isemayo, “matumaini sio sawa na kukata tamaa.” Mtu ambaye amekata tamaa hamlilii Mungu. Yuda hakumlilia Mungu. Mtu aliyekata tamaa hatafuti na haombi msamaha. Maisha yakikosa malengo yanakosa na maana. Namna hiyo ,sababu ya kuishi inaweza kuponyoka kutoka mikononi mwa mtu.

Matumaini ni kinyume cha kukata tamaa.

Matumaini yanaongea juu ya mwanzo mpya. Karakana za kutengenezea vitu za mwanasayansi Thomas Edison ziliungua usiku Desemba 1914 huko West Orange. Thomas Edison alipoteza vifaa vyenye thamani ya dola milioni moja na rekodi ya kazi zake.

Asubuhi iliyofuata, alitembea kwenye majivu ya matumaini yake na ndoto zake, mvumbuzi huyu aliyekuwa na umri wa miaka sitini na saba alisema, “Kuna jambo la thamani katika maafa. Makosa yetu yote yanachomwa. Sasa tunaweza kuanza upya.”

Mwanasayansi huyu aliona makosa ya kisayansi yanachomwa. Aliyatazama matatizo kama namna ya kuanza upya, pakiwepo na njia mpya na mtazamo mpya.

Matumaini yanasema siku mbaya haipitilizi, Jumanne haipitilizi na kuifanya Jumatano kuwa Jumanne. Mtu mmoja aliwahi kuniuliza, “Mbona Padre Kamugisha kila mara unaonekana mwenye furaha?” Nilimjibu:

“Hata kukiwa na tatizo, najua kuwa katika Biblia haikuandikwa siku hii ilikaa zaidi bali kukawa jioni kukawa asubuhi siku ya pili.” Hata kama tunapambana na matatizo kama wafuasi wawili wa Emmaus, tujue kuwa katika Biblia imeandikwa, “It came to pass,” (lilitoweka) na sio “It came to stay” (lilidumu).

Matumaini yanasema maisha pamoja na Yesu ni matumaini yasiyo na mwisho; bila Yesu ni mwisho usio na matumaini. Yesu alisema: “Ulimwengu mna mahangaiko, lakini pigeni moyo konde, mimi nimeushinda ulimwengu” (Yohane 16:33).

Tunaweza kuishinda dunia pamoja na Kristo.

Julian Mfalme wa Kirumi kuanzia mwaka 360 hadi 363 alitoa tamko kwamba, Ukristo uharamishwe na kwa nguvu zake zote alijitahidi kuuangamiza. Akimpitia mkristo mmoja mzee alimuuliza, “Kristo wako yuko wapi sasa? Mzee alijibu, “Anatengeneza jeneza kwa ajili ya Mfalme wa Kirumi.” Mwisho wa siku mauti yalimkabili mfalme alisema, “Ee Mgaliliya umeshinda!” Maisha pamoja na Yesu ni matumaini yasiyo na mwisho ya kushinda ulimwengu; bila yeye ni mwisho usio na matumaini wa kushinda

Matumani yanasema, “mawazo ya Mungu si mawazo yetu na njia za Mungu si njia zetu (Isaya 55: 6-9). Kuna maeneo mbalimbali ambapo mawazo ya Mungu si mawazo yetu. Eneo la kwanza ni ukarimu wa Mungu au majaliwa. Vigezo vyake vya kutoa ni tofauti na binadamu. a kuandika juu yake na wazo fulani.”