DINI: Matunda ya kesho yako kwenye mbegu za leo kwa hivyo basi la leo kalifanye leo

DINI: Matunda ya kesho yako kwenye mbegu za leo kwa hivyo basi la leo kalifanye leo

NA PADRE FAUSTIN KAMUGISHA

MWANADAMU ana siku mbili anazozijua katika maisha yake: jana na leo. Kesho iko mikononi mwa Mungu. Leo ni yako itumie vizuri. Ingekuwa kila asubuhi unawekewa kwenye akaunti yako dola 1,440 na kuhakikisha unazitumia zote, usipofanya hivyo salio linachukuliwa. Bila shaka ungejitahidi kutumia kila dola.

Leo una dakika 1,440. Muda ni mali. Tumia dakika hizo vizuri. Leo moja ni ya thamani sana kuliko kesho mbili. Utakavyokuwa kesho inategemea unavyoitumia leo.

“Nitakavyokuwa, kwa sasa niko kwenye mchakato wa kuwa hivyo,” alisema Benjamin Franklin. Leo fanya mchakato wa utakavyokuwa kesho. Lifanye leo! Labda kesho litakatazwa (methali ya Finland).

Methali hii inabainisha kuwa zuri liwezekano leo lisingoje kesho. Ni kama methali ya Kiswahi isemayo, leo ni kabla ya kesho. Methali ya inatufundisha tusiwe na tabia ya kuyaacha mambo tunayoweza kuyafanya leo yasubiri hadi kesho. Leo huitangulia kesho.

Kuna namna nyingi za kuitendea haki siku iitwayo leo.Kwanza anza siku kwa sala hii: “Utupe leo mkate wetu wa kila siku” (Mathayo 6: 11). “Kumbuka kuwa sala inaomba tu mkate wa leo.

Hailalamikii mkate tuliokula jana ambao ulikuwa umechacha; sala haisemi: “Ee Mungu pamekuwepo na ukame katika ukanda wa ngano na tunaweza kuwa na kipindi kingine cha ukame – na kama ni hivyo nitapataje mkate wa kula kipindi kingine cha majira au ikitokea nikapoteza kazi – ee Mungu, nitapaje mkate? Hapana, sala hii inatufundisha kuomba mkate wa leo tu. Mkate wa leo ni aina ya mkate unaoweza kula,” aliandika Dale Carnegie katika kitabu chake, How to Stop Worrying and Start Living.

Usiombe mkate wa kesho. Unaomba mkate wa leo. Haimaanishi usipange ya kesho. Inamaanisha kuwa matunda ya kesho yamo kwenye mbegu za leo.

“Wakati ujao unaanza leo, si kesho,” alisema Mt Papa Yohane Paulo II. Ombi hili halimaniishi ubweteke na kutegemea kila kitu kutoka kwa Mungu. Shiriki majibu ya sala kwa kutafuta mkate. Mungu anawalisha ndege lakini hawawekei chakula kwenye viota.Pili, usiruhusu leo yako ivamiwe na wasiwasi.

“Wasiwasi hauibi mateso ya kesho, bali unakausha furaha za leo” (Leo Buscaglia). “Msifanye wasiwasi mtakula nini na mtakunywa nini” (Luka 12:29).Tafsiri sisisi ya maneno msifanye wasiwasi ni msining’inie angani. Weka miguu chini. Yafanyie kazi duniani unayoyaomba mbinguni. Vinginevyo unaning’inia angani.

Kumuingiza Mungu katika mahangaiko yako na wakati huo huo hushiriki majibu ya sala ni kuning’inia angani.Tatu, kataa ya jana yasizidi ya leo. Kama ulilolifanya jana linaonekana kubwa, hujafanya kitu kikubwa leo. Leo vunja rekodi ya jana; sali zaidi, wekeza zaidi, panda miti zaidi kutaja machache tu. Jana isimeze sehemu kubwa ya leo.

“Usiache jana ichukue sehemu kubwa ya leo” (Will Rogers). Jana haiwezi kuikamata leo. “Leo haiwezi kuikamata kesho” (methali ya Jamaica)Nne, usilaze viporo.

“Usiliache mpaka kesho unaloweza kufanya leo,” alisema Benjamin Franklin. Kiporo ni chakula kilichobaki na kuliwa siku ya pili yake. Hakuna kulaza viporo. Hakuna kusitasita. Hakuna kubweteka. Hakuna kukumbatia uvivu. Hakuna utepetevu. Hakuna ukunguni. Hakuna ulegevu.Tano, vaa miwani ya kuona mambo chanya.

Methali ya Sanskriti ingawa ni ndefu inasema ukweli mtupu juu ya leo. “Itazame vizuri leo, kwa sababu jana ni ndoto tu na kesho ni maono tu. Leo unayoishi vizuri inaifanya kila jana ndoto ya wakati ujao mzuri na kila asubuhi ni maono ya matumaini. Itazame vizuri leo.”Leo imejaa furaha ya kukua.

Leo ipo fursa za maendeleo, fungua macho uone. Leo ina utukufu wa matendo mazuri, tenda tendo jema, wema hauozi. Leo imejaa uzuri wa neno jema, sifia na tia moyo. Leo imejaa maajabu ya maumbile, yafurahie. Leo imejaa fahari. (H. F. Lyte 1793-1847) katika sala ya usiku sala ya kumaliza siku alisali, “Yameisha fika mwishoni, maisha sasa yaisha, raha za dunia basi, zakoma fahari zake…ee usobadilika ukae pamoja nami.”

Kwa ufupi sala hiyo inabainisha kuwa leo imejaa raha na furaha, fahari na utukufu. Muda ni mali. Leo imejaa mali. Kabla ya jua kuchomoza mvuvi alienda mtoni. Alipokuwa kwenye kingo za mto alihisi kitu chini ya miguu yake.

Kulikuwepo begi dogo limejaa “mawe.” Alichukua begi hilo na kuweka neti yake upandeni na kuchuchumaa kwenye kingo za mto akingoja jua lichomoze. Bila ya kuwa na kitu cha kufanya alichukua “mawe” kutoka kwenye begi na kuanza kuyatupa mtoni.

Wakati jua linachomoza alikuwa ametupa “mawe” yote mtoni. Alibakiwa na “jiwe” moja.Akiwa amelishikilia na akisaidiwa na mwanga wa jua aliona vizuri “jiwe” la mwisho. Alifurahi sana. “Jiwe” hilo lilikuwa ni madini ya thamani kubwa. Alisikitika sana kwa vile alitupa madini mengi kwenye mto.

Muda ni madini ya thamani sana. Usiipoteze leo. Usitupe ovyo madini ya dakika za leo. “Haraka nyingi na kufika ni kesho; chukua muda, fika leo” (methali ya Jamaica). Haraka haraka haina baraka.

You can share this post!

Wanajeshi 23 waliofungwa kwa mauaji ya Kabila waachiliwa...

Yattani apondwa kuhusu ongezeko la deni la kitaifa