Makala

DINI: Mazuri yote unayotenda hakika yatakumbukwa daima dawamu

September 22nd, 2019 3 min read

Na WYCLIFFE OTIENO

KUNA mambo ambayo mtu huyatenda sirini na kuna mengine yanayotendwa waziwazi.

Kuna mambo mazuri ambayo huwa tunatenda tukitarajia kupewa shukrani au kusifiwa.

Mara nyingi huwa tunakereka moyoni tunapokosa kutambuliwa.

Labda kuna watu wengi uliowatendea mambo mema lakini walipofanikiwa wakakusahau au wakakulipa kwa ubaya. Usijali maana jambo lolote unalofanya duniani, kuna kumbukumbu inayowekwa.

Mordekai katika kitabu cha Esther 2:21-23 alimwokoa mfalme Ahasuero ilipopangiwa njama ya kuawa.

“Ikawa siku zile, Mordekai alipokuwa akiketi mlangoni pa mfalme, wawili katika wasimamizi wake mfalme, Bigthana na Tereshi, wangoje mlango, walighadhibika, wakataka kumpelekea mikono mfalme Ahasuero. Basi Mordekai akapata kulijua jambo hilo, naye akamjulisha Esta, malkia; naye Esta akamwambia mfalme habari hiyo kwa jina la Mordekai. Na jambo hilo lilipochunguzwa, na hakika ikapatikana, hao wote wawili wakatundikwa juu ya mti. Hayo pia yakaandikwa katika kitabu cha taarifa mbele ya mfalme.”

Cha ajabu ni kuwa baada ya kutenda mema alisahaulika. Badala yake Hamani Mwagagi, mtu mbaya sana ndiye aliyepandishwa cheo.

Esther 3:1, “Baada ya hayo, mfalme Ahasuero alimwongezea cheo Hamani bin Hamedatha, Mwagagi, akampandisha, akamwekea kiti chake juu ya maakida wote waliokuwapo pamoja naye.”

Lakini Mordekai aliendelea kufanya kazi yake kwa uaminifu.

Kwa muda mrefu mema ya Mordekai yalionekana kama yaliyosahaulika.

Je, mara ngapi umetenda mema na ukaona kuwa yamesahaulika? Ukweli ni kuwa kuna kumbukumbu inayowekwa.

Hakuna jambo unalofanya ambalo litasahaulika. Walioona wanaweza kuandika kwenye vitabu au wataweka akilini mwao.

Waliona na kamera watanasa kwenye mitambo. Hata katika ulimwengu wa kiroho kumbukumbu huwekwa, na Mungu mwenyewe atakulipa wakati ufaao.

Mordekai alikataa kumwinamia Hamani, maana yeye kama Myahudi aliamini kuwa Mungu tu ndiye anayestahili kuinamiwa.

Jambo hilo lilimkera Hamani na akapanga njama ya kumnyonga Mordekai na kuwaua Wayahudi wote. Lakini Mungu alikuwa na mpango mwema.

Waswahili walisema wema hauozi. Usiku wa kuamkia siku iliyopangwa Mordekai afe, mfalme hakupata usingizi.

Esther 6: 1-3, 10, “Usiku ule mfalme hakupata usingizi; akaamuru aletewe kitabu cha maandiko ya taarifa, nayo yakasomwa mbele ya mfalme.

Ikaonekana kuwa imeandikwa ya kwamba Mordekai aliwachongea Bigthana na Tereshi, wasimamizi wawili wa mfalme, katika hao waliolinda mlango, waliotaka kumtia mikono mfalme Ahasuero.

Mfalme akasema, Je! Ni heshima gani au jaha gani Mordekai aliyofanyiziwa kwa ajili ya hayo?

Watumwa wa mfalme waliomhudumu wakamwambia, Hakuna alilofanyiziwa… Basi mfalme akamwambia Hamani, Hima! Twaa mavazi na farasi kama ulivyosema, ukamfanyizie vivyo hivyo Mordekai, Myahudi, aketiye mlangoni pa mfalme; lisipungue neno lolote katika yote uliyoyasema.”

Kumbukumbu ilitolewa na mema aliyotenda Mordekai yakakumbukwa. Badala ya Mordekai kuuawa ni Hamani aliyeangamizwa.

Utalipwa chochote unachotenda. Utavuna unachopanda. Ukipanda mema utavuna mema, ukipanda maovu utavuna maovu.

Uamuzi ni wako. Mavuno mengine huonekama kuchelewa, mavuna mengine huja haraka. Lakini kwa hakika utavuna.

Ni juu yako kuamua kumpenda Mungu na kutii maagizo yake upate baraka, au uamue kukaidi upate laana. Mungu anayeona hata yaliyo sirini, atakujibu kwa wazi.

Waweza kuwadanganya wanadamu, lakini huwezi kumdanganya Mungu. Usijali kuhusu maadui na mipango yao. Mpende Mungu tu.

Wapende wanadamu, hata wale wasiopendeka. Upendo ni mbegu. Panda upendo utavuna upendo.

Waweza kudharauliwa leo, lakini siku moja Mungu akikumbuka mema uliyotenda atakulipa.

Waliokudharau watashangaa. Waliokuita majina na kukukejeli watashangaa.

Mlindalango

Mordekai alikuwa mlindalango. Lakini mema aliyotenda yalipokumbukwa, aliinuliwa hata akawa waziri mkuu katika nchi ya kigeni. Yusufu alidharauliwa, akauzwa na hatimaye akafungwa jela.

Lakini ndoto aliyotabiri ilipokumbukwa, alitolewa gerezani akafanywa waziri mkuu.

Yusufu aliamka akiwa mfungwa, lakini jioni hiyo alilala ikuluni akiwa waziri mkuu. Siku moja Dorkasi alikuwa amekufa, lakini wanawake wajane walipokumbuka ukarimu wake na mavazi aliyowashonea, walilia sana. Petero alipoona hayo, akamfufua Dorkasi.

Mema unayotenda hayataoza. Mungu atakukumbuka wakati ufaao.

Kila mara shetani anapotushtaki, Mungu anakumbuka damu ya Yesu iliyomwagika msalabani kwa sababu yetu. Hukumu inaondolewa na tunahesabiwa haki kwa neema.

Mpende Mungu. Tembea katika utakatifu. Tenda mapenzi yake.

Kuna kumbukumbu inayowekwa. Na siku ya malipo yaja.