DINI: Msalaba ndio siri ya mafanikio; hakuna utukufu bila mahangaiko

DINI: Msalaba ndio siri ya mafanikio; hakuna utukufu bila mahangaiko

Na FAUSTIN KAMUGISHA

UKINYOOSHA mikono yako upandeni unakuwa na sura ya msalaba.

Sura ya binadamu ni sura ya msalaba. Kichwani hadi miguuni ni kama ubao wima wa msalaba.

Mikono iliyonyoshwa ni kama ubao mlalo wa msalaba. Ubao wima wa msalaba unaongea juu ya mausihano kati ya Mungu na binadamu, Yesu Kristu ni mpatanishi.

Magugu huziba njia ambayo haitumiki. Ili kuimarisha uhusiano wako na Mungu, mtembelee kwenye maeneo ya ibada.

Zungumza naye asubuhi katika sala. Mshukuru jioni kabla ya kulala. Anza siku na Mungu. Imalize siku na Mungu. Ubao mlalo unaonyesha uhusiano kati ya binadamu na binadamu Yesu Kristu ni mpatanishi.

Hatuna budi kuishi kindugu. Undugu ni kufaana si kufanana.

Msalaba ni nembo ya ushindi. Kwa kifo cha msalabani Yesu ametukomboa. Nakubaliana na mtume Paulo aliyeandika, “Sisi imetupasa kuona fahari kwa Msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristu” (Gal 6: 14)

Msalaba unaongea juu ya kuwafikiria wengine. Yesu alipokuwa msalabani aliwafikiria wengine. Tunasoma hivi katika Injili ya Yohane, “Karibu na msalaba wa Yesu walisimama mama yake, Maria Mke wa Klopa, na Maria Magdalena.

Basi, Yesu alipomwona mama yake na karibu naye mfuasi aliyempenda, alimwambia mama yake, “Mama, tazama mwanao.” Kisha akamwambia mfuasi, “Tazama mama yako.” Toka saa ile mfuasi huyo alimpokea nyumbani kwake” (Yohane 19: 25- 27).

Baba wa Kanisa Teofilo alisema, “Wakati askari walikuwa wanafanya kazi yao ya ukatili, alikuwa anamfikiria mama yake kwa wasiwasi mkubwa.”

Katika shida wafikirie wengine. Unapopiga makasia ya mtumbwi wa mwingine uende mbele, wa kwako unaenda mbele pia.

Ukiwa mgonjwa umetembelewa waulizie wagonjwa wengine wanaendeleaje. Huko Afrika ya Kusini siku moja Gandhi alikuwa anasafiri katika daraja la kwanza la gari moshi.

Askari wa kizungu alitaka kumtoa nje ya daraja la kwanza. Lakini Gandhi aliona si haki. Alipinga. Askari alimrushia teke Gandhi. Gandhi alimuuliza askari, “Kiatu chako kimepona?” Akiwa na maumivu alifikiria kiatu cha askari.

Pointi ni kuwa wafikirie wengine. Wakina mama wana kanga zimeandikwa, “kula unibakizie.” Usizibe njia wafikirie wengine. Kuna maeneo pembezoni mwa mji watu wanaziba njia.

Hawana imani kuwa watoto wao na wajukuu wao watanunua magari. Wafikirie wengine. Unapojipakulia chakula wafikirie wengine. Isiwe kujihudumia kichoyo bali kujihudumia kiukarimu ukijua wewe kwenye msitari si kitinda mimba.

Wafikirie wengine. Kuku hugawana myonyoo na vifaranga, ni mfano wa kuwafikiria wengine. Niliona picha ya swala anakimbizwa na simba akiwa na watoto wake wawili. Aliamua kusimama watoto wakakimbia.

Wakati simba anamshughulikia watoto wake waliweza kutoroka kwenye makucha ya simba. Wakati simba anamshughulikia swala macho ya swala yalielekezwa kwa watoto wake. Huu ni mfano wa kuwafikiria wengine.

Msalaba unaongea juu ya siri ya mafanikio: hakuna msalaba, hakuna taji la utukufu; hakuna jasho, hakuna matamu; hakuna dhiki, hakuna faraja; hakuna Ijumaa Kuu, hakuna Jumapili ya Pasaka. Mpiga gitaa alijisema, “Pesa haitoki pepesi, gitaa imenichoma vidole.”

Vidole kuumizwa ni msalaba. Mwisho wa siku kuna mafanikio. “Taji la miiba ni sharti la taji la utukufu,” alisema Askofu Fulton Sheen wa Marekani. Msalaba ni vijilia ya utukufu.

Ijumaa Kuu kwanza, Jumapili ya Pasaka baadaye. Baada ya dhiki faraja. Huwezi kutafuta mataji kwa kukwepa misalaba. Huwezi kutafuta kupandishwa cheo kwa kukwepa misalaba. Mchumia juani hulia kivulini.

Mtu anayefanya kazi ngumu (juani, msalabani) huishia kufurahia matunda ya kazi yake kwa raha (kivulini, utukufu). Mtaka cha uvunguni (utukufu) sharti ainame (msalaba). Katika misingi hii hakuna msalaba, hakuna utukufu.

Wahaya wa Tanzania wana methali isemayo: Zuri (utukufu) lina gharama kubwa sana (msalaba) – akarungi kaseza. Kuna kitendawili cha wahaya kisemacho: Limeiva lakini liko miibani (jibu ni senene kwenye miiba). Lililoiva ni utukufu.

Miibani ni msalaba au taji la msalaba. Pointi ni kuwa huwezi kutafuta mataji ya ushindi kwa kukwepa misalaba.

You can share this post!

JAMVI: Raila anajitia hatarini kuhepwa ifikapo 2022

Wanaomezea ‘tosha’ ya Uhuru