Makala

DINI: Mungu hahitaji umati kutimiza kusudi lake

February 4th, 2024 1 min read

NA WYCLIFFE OTIENO

TUKIWA wengi tunaweza kufanya mambo mengi na ni kweli pia kwamba umoja ni nguvu kwani wanadadamu hukamilika kwa kushirikiana.

Lakini Mungu si lazima atumie umati. Mtu mmoja mtiifu akiwa na Mungu ni Umati mkubwa kwa maana hakuna jambo gumu kwake.

Wamidiani waliwahangaisha sana Waisraeli. Waliwaibia vyakula na kuwafanya wateseke. Ilibidi Gideoni atafute watu wa kumsaidia kukomboa Israeli. Maadui walikuwa wengi kuwazidi.

Gideoni alidhani alihitaji watu wengi sana iwezekanavyo ili kuwakabili. Alikusanya watu 32,000. Lakini Mungu akasema hao ni wengi sana.

Waamuzi 7:2 inasema, Bwana akamwambia Gideoni, Watu hawa walio pamoja nawe ni wengi mno hata nikawatie Wamidiani katika mikono yao, wasije Israeli wakajivuna juu yangu wakisema, Mkono wangu mwenyewe ndio ulioniokoa.

Vita vingekuwa vikali na watu majasiri tu ndio walihitajika. Aliwapunguza wakabaki watu elfu kumi. Hata hao waliobaki aliagizwa awapunguze wakabaki 300. Vita vilikuwa kwa utukufu wa Bwana. Kama watu wengi wangeshinda wangejivuna na Mungu asingepokea utukufu.

Katika maisha yako labda umejipata katika hali ngumu kama hii. Mungu anaweza kukuokoa akitumia watu wengi au wachache.
Cha kushangaza ni kuwa hata Gideoni mwenyewe alikuwa mwoga. Malaika alipomtokea na kumwita shujaa, alikuwa amejificha kwenye shinikizo akipura ngano. Sauti ya Mungu ilimbadilisha akawa shujaa na kukomboa Israeli.

Mungu anaweza kukutumia licha ya hofu uliyo nayo ukatenda mambo makuu. Ukisikia sauti yake, amini tu maana alikujua hata kabla hujazaliwa.

Ukiwa na Mungu si lazima utumie silaha za kawaida. Wanajeshi wa Gideoni hawakutumia mikuki, panga na mishale. Walipiga tarumbeta, wakaivunja mitungi, wakaishika mienge kwa mikono yao ya kushoto, na zile tarumbeta katika mikono yao ya kuume; wakapiga kelele, Upanga wa Bwana na wa Gideoni (Waamuzi 7:20). Walishinda kwa kumtukuza Bwana.

Hata Daudi alishindwa kutumia upanga wa Sauli, lakini bado akampiga Goliathi kwa kutumia kombeo. Maana aliamini kuwa ni Bwana anampigania.

Ukimsikia atakuelekeza, ukitembea naye utafika salama, ukimtii wanadamu watakutii, ukimwogopa watu watakuogopa. Ukimtukuza, utatukuzwa.