DINI: Penda kusema ukweli siku zote, njia ya mwongo ni fupi, imejaa aibu na fedheha

DINI: Penda kusema ukweli siku zote, njia ya mwongo ni fupi, imejaa aibu na fedheha

NA PADRE FAUSTIN KAMUGISHA

NYUMBA ya muongo ikiwaka moto hakuna atakayemuamini. Na ukisema uongo Jumamosi utaaibika Jumapili. Ndivyo zisemavyo methali mbili za Uturuki.

Hakuna anayemuamini muongo; na matokeo ya kusema uongo ni aibu.

Kusikiliza uongo ni kazi ngumu zaidi kuliko kusema uongo (methali ya Turkey). Yataka upige moyo konde ili kusikiliza uongo.

Kusema kweli, uongo unafunga lakini haukazi. Ukiwa na mtungi wa gesi ukizima gesi, usipokaza gesi inavuja. Uongo kawaida yake ni “kuvuja.”

Yesu alipofufuka ulisemwa uongo kuzima ukweli huu. Ilitolewa hongo kwa ajili ya kuzima ukweli huu.

Tunasoma hivi katika Biblia. “Walipokuwa bado njiani, baadhi ya walinzi walienda mjini, wakawapasha makuhani wakuu habari za mambo yote yaliyotendeka. Nao wakakusanyika na wazee. Na baada ya kushauriana na kupatana, wakawapa askari fedha nyingi, wakawaagiza, “Semeni, ‘wafuasi wake walikuja usiku, wakamwiba sisi tulipokuwa tunalala usingizi.’ Na kama gavana akisikia neno, sisi tutamshauri, ili msipatwe na matatizo.” Nao wakapokea fedha, wakafanya kama walivyoagizwa.” (Mathayo 28: 11-15).

Huu ni mfano wa uongo unavyofunga lakini haukazi. Kwanza njia ya muongo ni fupi. Ni askari wa namna gani anapewa jukumu la kulinda kisha yeye analala.

Askari ni mtu anayefanya kazi ya kulinda raia, kulinda nchi. Jukumu lake kuu ni kulinda. Kisa hiki kinakumbusha masimulizi ya watu watatu waliomfanyia kazi mtu aliyeitwa Musa.

Alipouliza ni namna gani wanampenda. Mpishi alijibu: “Nakupenda sana ndio maana nakupikia chakula kizuri kila siku.”

Mwenye kufanya usafi wa mazingira alisema: “Nakupenda sana, ndio maana nahakikisha mazingira ni safi na yanavutia.”

Mlinzi wake alisema: “Nakupenda sana ndio maana kila ninapolinda nakuota.” Kumbe huyu husinzia kazini! Pili, mtu huchongewa na ulimi wake. Mtu hutiwa kwenye matatizo kwa sababu ya ulimi wake.

Askari waliagizwa kusema kuwa “wafuasi wake walikuja usiku, wakamwiba sisi tulipokuwa tunalala usingizi.”

Ina maana jicho moja liliona wafuasi wakiiba mwili wa Yesu. Jicho lingine lika limefumbwa kwa sababu ya usingizi.

Namna hii ya kulala inapingana na maumbile ya binadamu. Je, baadaye kwanini hawakutafuta hati ya kufanya upekuzi kila mahali?

Tatu, fedha fedheha. Makuhani wakuu pamoja na wazee walifuata falsafa potofu isemayo, “penye udhia weka rupia,” – yaani penye udhia na shida weka rushwa.

Tumesoma hapo juu kwenye Biblia kwamba, “Na baada ya kushauriana na kupatana, wakawapa askari fedha nyingi, wakawaagiza, “Semeni, ‘wafuasi wake walikuja usiku, wakamwiba sisi tulipokuwa tunalala usingizi’.”

Kitendo cha kutoa rushwa ni ushahidi kuwa Yesu alifufuka. Ukweli ukizikwa una tabia ya kufufuka. Rushwa hutolewa ili kuzima ukweli. Fedha fedheha ina maana kuwa pesa huleta mambo ya aibu baina ya binadamu.

Ukisema uongo lazima uwe ni mtu anayekumbuka mambo sana. Kuna hadithi ya mtu aliyeiba mlango. Mwenye mlango alienda gulioni na kusema, “Aliyeiba mlango ana utando wa buibui kichwani.”

Aliyeiba mlango akagusa kiganja chake kichwani, na kwa namna hiyo alijulikana. Mtunga Zaburi 119:43 anatukumbusha kuwa, “Usiliondoe neno la kweli kinywani.”

Ukweli hauzami unaibuka. Ukweli ukiuzika utafufuka. Yesu alisema: “Mimi ndimi njia na ukweli.” (Yohane 14: 6).

Yesu alipofufuka ni ukweli ulifufuka. Ukweli ukiuzamisha utaelea. Ukweli ukiuzima hauzimiki. Ukweli ukiuziba unazibuka.

Ukweli ni kama mafuta, yataelea juu ya maji. Pia ni kama moshi, huwezi kuuficha kwenye nguo. Ukweli ni sawa na kikohozi, hakifichiki.

Kuna mtu aliyetuhumiwa kumpiga mtu fulani. Mahakamani mshitaki alimwambia mshitakiwa: “Ulinipiga.” Mshtakiwa alijibu: “Sikukupiga.”

Mshtaki alisisitiza: “Ulinipiga!” Mshtakiwa alirudisha jibu: “Sikukupiga!” Kwa hasira mshtaki alisema kwa msisitizo: “Ulinipiga!!!” Kwa hasira mshtakiwa alisema: “Naweza kukupiga tena!!!”

Ukweli ulielea. Ukweli una tabia ya kufufuka. Ukweli ndio unafunga na kukaza. Uongo unafunga lakini haukazi.

You can share this post!

Watu 30 pekee wahudhuria mazishi ya mume wa Malkia

JAMVI: Njama ya Raila kubomoa One Kenya Alliance