DINI: Tunapoishi na wenzetu tuachiane alama za moyoni, yaani tugusane kwa matendo mema

DINI: Tunapoishi na wenzetu tuachiane alama za moyoni, yaani tugusane kwa matendo mema

Na PADRE FAUSTIN KAMUGISHA

UNAPOKUTANA na watu huwa wanakupima kichwa chako lakini unapoondoka wao hupima moyo wako.

Unapokutana na watu ni kama unawaachia alama za vidole (fingerprints) na vilevile kwa namna moja au nyingine huwa unawaachia alama za moyo (heart prints).

Huwa tunaacha alama za vidole kwenye pesa, zawadi zilizofungwa na ambazo hazikufungwa, kwenye vitasa, kuta, vitabu na vijiko japo kwa kutaja vitu vichache tu.

Wahaya wana methali isemayo: “Nyumba zinapakana lakini mioyo haipakani” maana yake ikiwa kwamba majirani hawaachiani alama za mioyo. Ni kama methali ya Tuareg isemayo, “Achanisha mahema kisha weka mioyo pamoja.” Hakikisha mnaachiana alama za mioyo. Kuacha alama ya moyo ni kugusa moyo wa mtu kwa matendo mema.

Alama za moyo ni alama za kuumia kwa ajili ya wengine. Mama Tereza wa Calcutta alisema, “Penda mpaka upendo ukuumize.”

Bwana Yesu Kristu alipofufuka alikuwa na vidonda vya misumari, aliwaambia wafuasi wake, “Tazameni mikono yangu na miguu yangu, ya kuwa ni mimi mwenyewe” (Lk 24:39). Vidonda hivi viliwakilisha alama za moyo wake ulioumia kwa ajili ya wengine.

“Bwana alienda na vidonda vyake kwenye umilele. Ni Mungu aliyeumizwa; alikubali kuumizwa kupitia upendo wake kwetu. Vidonda vyake ni alama kwamba anaelewa na anakubali kuumizwa kutokana na upendo wake kwetu. Vidonda vyake hivi namna gani vinagusika katika historia ya nyakati zetu!

Kusema kweli, mara kwa mara anakubali kuumizwa kwa ajili yetu. Ni uhakika ulioje wa huruma yake, ni faraja ya namna gani vidonda vyake vinamaanisha kwetu!…ni wajibu ulioje vinaotupa, wajibu wa kukubali kuumizwa kwa ajili yake,” alisema Papa Benedict XVI katika homilia ya Jumapili ya Huruma ya Mungu, Aprili 15, 2007.

Weisberg ni mji mmojawapo wa miji ya Ujerumani ambo una mnara ambao uko juu ya ngome na mnara huo unabeba jina, “Imani ya Wanawake.” Inasemekana kuwa Mfalme Conard II alivamia ngome hiyo na askari waliokuwa wanalinda ngome walisalimu amri kwa sharti kuwa wanawake waruhusiwe kubeba wanavyovipenda sana.

Mfalme alitegemea wangebeba mikufu ya thamani na hazina ambazo wanawake hupenda. Kwa mshangao mkubwa alipokuwa anawasubiri wanawake watoke alishangazwa na walichokuwa wamebeba. Wanawake wasio na nguvu na wenye nguvu, wazee kwa vijana walibeba waume zao au watoto wao wa kiume au binti zao. Wengi waliumia sababu ya uzito wa wapendwa wao. Wakati wa dharura wanawake hawakukumbuka pete zao za dhahabu na mikufu yao ya dhahabu walikumbuka wapendwa wao. Hawa hawaitwi tu, “wanawake wa imani” bali “wanawake wa upendo.” Hawa waliacha alama za moyo.

Alama za moyo ni alama za mapenzi mema, ni alama za nia njema. Kuna mtoto aliyekuwa na maembe mawili yaliyoiva. Mama yake alimuomba ampe embe moja. Haraka haraka mtoto huyo alionja kipande cha embe moja na baadaye kipande cha embe la pili. Mama yake alifikiri mtoto wake ni mchoyo. Mtoto huyo alimpa mama yake embe aliloshikilia katika mkono wa kushoto akisema, “Mama chukua hili ndilo tamu.” Mtoto huyo alipoonja embe alikuwa na nia njema.

Alama za moyo ni alama za kutoa. Yesu alitoa uhai wake kwa ajili yetu. Alain Delon alisema, “Nilijua kila kitu na kupokea kila kitu. Lakini furaha ya kweli ni kutoa.” Kwa maneno yaliyotiwa chumvi anasema kujua kunaleta furaha lakini si kamili. Kupokea kunaleta furaha lakini si kamili. Kutoa kunaleta furaha ya kweli. Kumbe kutoa na kupokea kunaleta furaha kamili.

William Barclay alisema, “Zawadi si kamili kama sisi hatumo katika zawadi hiyo.”

Ukitoa zawadi ya suruali iliyochanika ambayo ulitegemea kulitupa, nafsi yako haimo katika zawadi hiyo.

You can share this post!

Olunga akwamilia juu ya jedwali la wafungaji Klabu Bingwa...

Kimbunga Jobo chaishiwa nguvu baada ya kuwasili Tanzania