DINI: Ugumu wa maisha usikufanye upoteze imani au kulaumu wengine, jipe moyo kuna nuru

DINI: Ugumu wa maisha usikufanye upoteze imani au kulaumu wengine, jipe moyo kuna nuru

Na WYCLIFFE OTIENO

KUNA wakati katika maisha mambo yanakuwa magumu mpaka unasikia kukata tamaa.

Unaweza kujikuta umezungukwa na shida mpaka hujui la kufanya. Wakati kama huo, watu wengi hutafuta mtu wa kulaumu. Watu wengi hupoteza mwelekeo na kuchanganyikiwa.

Lakini leo ningependa ujue kwamba ni vigumu kutofautisha chuma iliyopakwa rangi ya dhahabu na dhahabu yenyewe, mpaka zipitishwe kwa moto.

Changamoto tunazozipitia zimekusudiwa kutufanya bora zaidi.

Kufanikiwa au kutofanikiwa kunategemea mtazamo wako. Ukitaka kushinda magumu yote yanayokuja mbele zako, lazima uamue kuwa hutakoma wala kuchoka bali utaendelea kusonga mbele.

Mungu alimtuma Musa kuwakomboa Waisraeli kutoka utumwani Misri, lakini kila mara walipopata shida walimlalamikia Musa na wakapoteza tumaini.

Biblia Takatifu katika kitabu cha Kutoka 14:13-15 inasema, “Musa akawaambia watu, Msiogope, simameni tu, mkauone wokovu wa Bwana atakaowafanyia leo; kwa maana hao Wamisri mliowaona leo hamtawaona tena milele. Bwana atawapigania ninyi, nanyi mtanyamaza kimya.”

Lakini katika mstari wa 15, Bwana anamwambia Musa, “Bwana akamwambia Musa, Mbona unanililia mimi? Waambie wana wa Israeli waendelee mbele.”

Endelea mbele! Usichoke! Usikome! Wakati mambo ni magumu, ichukulie kama ishara ya ushindi mkuu unaotarajiwa.

Kuna mambo lazima ujiepushe nayo ili ufikie hatima yako. Usiruhusu maoni ya watu wengine kuongoza maisha yako. Si kile watu wanachofikiria juu yako bali ni kile unafikiria ndio muhimu. Fanya kilicho cha maana kwako, wala usitake kumpendeza kila mtu, lakini jizatiti kumpendeza Mungu maana bila yeye huwezi lolote.

Usikubali aibu ya kushindwa kwako hapo awali ikuzuie kuendelea. Kila mtu aliyefanikiwa maishani, alianza na kushindwa. Elewa yaliyopita maishani mwako hayawezi kulinganishwa na yajayo. Cha muhimu ni kile unachofanya sasa. Waswahili walisema, yaliyopita si ndwele, ganga yajayo.

Lazima katika maisha yako uamue kile unachotaka. Unataka uhusiano wako na Mungu uwe vipi?

Unataka uhusiano wako na watu wengine uweje? Unataka biashara yako iweje? Unataka familia yako iweje? Unataka masomo yako yawe vipi? Unataka huduma yako iweje? Unataka hatima yako iweje?

Lazima uamue mwenyewe. Huwezi kutoka mahali ulipo mpaka uamue mahali unapotaka kuwa. Amua kile unachotaka, kisha ukifuatilie kwa bidii na utafaulu.

Jambo lingine linalowazuia wengi kufanikiwa ni kuahirisha malengo yaliyo muhimu. Kuna maamuzi mawili ya kimsingi maishani, kukubali hali jinsi ilivyo au kukubali jukumu lako la kubadilisha hali.

Musa angekubali kuendelea kuwa mwana wa binti Firauni na kuwaacha Wayahudi wateseke. Lakini alichagua kuacha maisha ya kifahari na kuamua kufanya mapenzi ya Mungu. Kama unataka kuanzisha biashara, wakati mzuri ni jana, lakini kama hukuanza jana, Mungu amekupa nafasi ya pili uianze leo. Wacha kuahirisha mambo.

Mhubiri Rick Warren anasema kuwa kila siku inakupa fursa mpya ya kuchagua. Kuna watu ambao wameamua kutofanya chochote. Kama hufanyi chochote mbona unatarajia mazuri? Hakuna atakayekuchagulia.

Kila mtu ana mzigo wake mzito. Kila mwamba ngoma huvuta kwake, walisema wahenga. Maisha ni kujizatiti. Biblia inasema katika Mathayo 11:12, “Tangu siku za Yohana Mbatizaji hata sasa ufalme wa mbinguni hupatikana kwa nguvu, nao wenye nguvu wauteka.”

Kama vile ufalme wa mbinguni haupatikani kirahisi, vilevile mazuri unayoyatafuta hapa duniani, hayatakujia kirahisi. Usipoamua kutumia nafasi ambayo Bwana amekupa leo kuchagua kufanya kitu juu ya maisha yako utajipata ukitoa visababu. Mara nyingi kutofanikiwa kwa muda mrefu huwa ni matokeo ya watu wanaotoa visababu badala ya maamuzi.

Mambo yakiwa magumu amua kuendelea mbele. Musa aliwaambia Waisraeli wasimame wima waone ushindi wa Bwana, lakini Bwana akamwambia endelea mbele. Musa alipofuata maagizo ya Mungu, njia ilipatikana baharini. Ukifuata maagizo ya Mungu, njia itapatikana.

Haijalishi kama ni ukuta uko mbele yako. Haijalishi kama ni jangwa. Waisraeli waliona milima upande, bahari mbele yao na majeshi ya Firauni yuma yao, wakawa na hofu na kutamani wangebaki Misri kama watumwa. Lakini walisahau kuangalia juu mahali msaada wao ungetoka. Walisahau hatima yao na ahadi ya Bwana kuwa anawatoa utumwani na kuwapeleka katika nchi iliyo na asali na maziwa.

Bwana ana mpango mzuri nawe. Usikubali ripoti ya wanadamu. Amini ripoti ya Mungu aliyekuumba na kukukomboa kwa damu ya dhamani kuu ya mwanawe Yesu Kristo. Mpango wa Mungu ni ufanikiwe. Mpango wa Mungu ni uendelee mbele!

You can share this post!

JAMVI: Raila kuvizia ziara za Rais Ukambani kwaibua hofu

JAMVI: Dalili mwafaka umepatikana Mlimani kuhusu kura ya...