DINI: Unayojiambia yatakuinua au kukufifisha, tafakari kwanza kuhusu unayoyatamka!

DINI: Unayojiambia yatakuinua au kukufifisha, tafakari kwanza kuhusu unayoyatamka!

NA PADRE FAUSTIN KAMUGISHA

MSOMI mmoja aliwahi kusema hivi: “Unayojiambia kila siku yatakuinua au yatakudidimiza. Uwe mwema kwa nafsi yako kwa kuwa unalojiambia linasikika mbinguni. Unalojiambia Mungu analisikia. Unalojiambia linakurudia. Maisha ni mwangwi. Unalojiambia ni mtazamo chanya au mtazamo hasi.”

“Usisahau kujiambia mambo chanya kila siku! Lazima ujipende kwa ndani ili ukue kwa nje, ” alisema Hannah Bronfman.

Katika Biblia, kuna mwanamke aliyekuwa anafuja damu kwa muda wa miaka kumi na miwili, aliamua kumwendea Yesu ili amponye, “Alijiambia, nikigusa pindo la vazi lake nitapona” (Mk 5:28).

Alijiambia maneno ya matumaini, maneno ya mtazamo chanya, maneno ya kujipenda, maneno ya imani, maneno yatiayo mwanga. Yesu alimwambia, “imani yako imekuponya.”

Alimponya. Swali ni, wewe unajiambia nini?Kwanza, jiambie inawezekana. Mwanamke aliyekuwa anatokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili alifikiria kiuwezekano. Chunga namna yako ya kufikiri.

“Kwa maana alijiambia, ‘Nikigusa mavazi yake tu, nitapona” (Marko 5: 28). Mwanamke huyu kabla ya kuligusa vazi la Yesu aliligusa kimawazo. “Sio pindo la vazi, bali namna yake ya kufikiri iliyomfanya apone,” alisema Mt. Yohane Krisostomu.

Kuna mainjinia waliopewa mtihani wa kufungua mlango bila ufunguo. Walikuwa watatu. Wawili walianza kukokotoa mahesabu.

Mmoja baada ya kupumzika na kutulia dakika tano, alienda na kufungua mlango. Ulikuwa haujafungwa. Alifikiria kiuwezekano.

Tunasoma katika kitabu cha Ufunuo 3:8, “Nayajua matendo yako. Tazama nimekupa mlango uliofunguliwa mbele yako ambao hapana awezaye kuufunga. Kwa kuwa unazo nguvu kidogo, nawe umelitunza neno langu wala hukuzika jina langu.”

Katika maisha, kuna milango ya kazi imefunguliwa, ingia. Kuna mlango wa uchumba umefunguliwa ingia.

“Anayetegemea mazuri yatokee anabadili lisilowezekana liwe liwezekanalo; anayetegemea mabaya yatokee anabadili linalowezekana liwe lisilowezekana,” alisema William Arthur Ward.

Mwanamke tunayemuongelea alikuwa na ugonjwa ambao ulikuwa wa kawaida kwa wayahudi. Tiba yake ilikuwa si rahisi.

Lakini palikuwepo na tiba za kishirikina ambazo zilikuwa ni danganya toto: kubeba majivu kwenye yai la mbuni kwenye nguo ya kitani wakati wa kiangazi na kwenye nguo ya pamba wakati wa kipindi cha baridi; kubeba punje ya shayiri ambayo imekutwa kwenye samadi ya punda mweupe.

Matabibu wengine walitumia toniki na kunyasi (kitu kinachosababisha tishu laini kujikunyata na kubana mishipa ya damu).

Mali yake yote ilimpotea. Kuna methali isemayo: Familia inayoenda kwa mganga wa kienyeji kupiga ramli unenepesha watoto wa mganga. Bila shaka mwanamke huyu alilinenepesha watoto wa waganga wa kienyeji.Pili, unapopatwa na tatizo, jiambie ni baraka katika sura ya balaa.

Mwanamke kutoka damu miaka kumi na miwili kulimkutanisha na Yesu. “Tuinuke na tuwe watu wa shukrani, kama hatukujifunza kitu leo, walau tumejifunza kitu kidogo, na kama hatukujifunza kitu kidogo, walau hatukuugua na kama tumekuwa wagonjwa walau hatukufa,” alisema Gautama Buddha (563 K.K – 483 K.K) mwanzilishi wa dini ya Buddha.

Katika balaa, tutafute jambo la kuleta furaha. Kidole kikiumia mshukuru Mungu kwa kukupa vidole, mkono bila vidole ungekuwa kama kijiko.

Kuna filamu ya Disney iliyoitwa Pollyanna iliyotoka 1960 ina The Glad Game (Mchezo wa furaha). Somo tunalolipata ni kuwa, katika shida, tafuta jambo la kuleta furaha. Katika hasi tafuta chanya.

Katika magumu tafuta jambo la kuleta furaha. Katika Chuo Kikuu kiitwacho Cornerstone University, anafunzi walicheza mchezo huitwao Mchezo wa Shukrani. Unataja ndani ya sekunde tatu jambo ambalo unashukuru bila kurudia alilolitaja mwanafunzi mwenzako.

Badala yake walilalamikia kipindi kigumu cha mitihani, ukosefu wa ada na matumizi, utafiti, tarehe za kuwasilisha kazi kutaja machache.

You can share this post!

Mabilioni ya miradi ya serikali ndiyo ‘hutafunwa’ zaidi...

KDF yaungana na GSU, Kenya Prisons na KPA fainali za...