Makala

DINI: Usipolisahihisha kosa lako la sasa wafaa ufahamu hilo ni kosa la pili

June 16th, 2019 2 min read

Na FAUSTIN KAMUGISHA

MAKOSA ni mtihani.

“Inabidi mtu awe mkubwa kiasi cha kukubali makosa yake, makini kiasi cha kuyafaidi na jasiri kiasi cha kuyasahihisha,” alisema R.B. Zuck.

Tunajifunza mambo matatu. Kwanza, yule ambaye hakubali makosa yake bado ni mdogo.

“Hakuna mtu ambaye amekuwa mkubwa bila kupitia makosa mengi na makubwa,” alisema Phyllis Bottome.

Pili, ni kujifunza kutokana na makosa yetu.

“Makosa yako ni masomo mapya ya mafanikio,” alisema Bernardo.

Uzoefu unatufundisha kwa gharama ya makosa.

Tatu, kusahihisha makosa kunahitaji ujasiri. Usiposahihisha kosa unatenda kosa jingine. Kosa kubwa ni kurudia kosa.

Tunasoma hivi katika kitabu cha mithali: “Afichaye makosa yake hafanikiwi” (Mithali 28: 13).

Makosa yetu ya zamani tusipoyaungama na kuyatubu tukiyabeba tunabeba mizigo mizito.

Mtunga zaburi alisema: “Kwani makosa yangu yamenifunika kichwa, kama mzigo mzito mno yamenilemea” (Zaburi 38: 5). Makosa ni mzigo.

Jifunze kutokana na makosa ya wengine. Huwezi kuishi muda mrefu sana kuyatenda yote ili yawe fundisho na somo kwako.

“Makosa ya wengine ni walimu wazuri” (Methali ya Estonia). Mtu mwenye busara anawasoma wengine ili ajifunze kutokana na makosa yao, kwa gharama yao.

Jifunze kutokana na makosa ya wengine bila kuyanyoshea kidole, huenda kidole chako ni kichafu.

“Usiyanyoshee makosa ya wengine kidole kichafu” (Methali ya Italia).

Makosa yanatunyenyekesha. Makosa yanatuweka katika makundi. Kuna kundi la watu ambao hawakubali makosa yao na kuna kundi ambalo linayaita makosa uzoefu, linayakubali.

Makosa yetu ni furaha ya baadhi ya watu. Makosa ni dokezo kuwa tunafanya kitu fulani.

“Ni wale tu ambao hawafanyi chochote ambao hawafanyi makosa,” alisema Harry S. Truman. Makosa yanatufanya tuvumbue mambo ambayo hayawezekani. Lakini unyenyekevu unahitajika.

“Unyenyekevu unapelekea kwenye nguvu na si udhaifu. Ni umbo la juu kabisa la kujiheshimu kukiri makosa na kujirekebisha” alisema John J. Mccloy.

Makosa ni mtihani. Kuna mwanamke ambaye alisafiri kwenda Paris, Ufaransa bila mume wake. Dukani aliona mkufu wenye thamani sana ambao alikuwa anautafuta. Alituma ujumbe kwa mume wake wenye maneno yafuatayo.

“Nimeona mkufu mzuri sana ambao nilikuwa nautafuta bei yake ni Sh1 milioni. Unafikiri naweza kuununua?” Mume wake alituma ujumbe usemao, “Hakuna gharama iliyo juu.” Alisahau kuweka alama ya mkato ili ujumbe usomeke, “Hakuna, gharama iliyo juu.”

Mwanamke alifurahi sana.

Kutoweka koma kulimweka mwanaume huyo kwenye koma.

Kosa liwe hata dogo ni mtihani.

Bila shaka mwanaume alijifunza kuwa makinifu.

Makosa hayana kauli ya mwisho, kukosa njia ni kujua njia.

Norman Vincent alisema, “Haijalishi umetenda kosa gani – haijalishi umeharibu mambo kiasi gani – bado unaweza kufanya mwanzo mpya.Mtu ambaye anatambua jambo hili kabisa haumii sana kutokana na mshtuko na maumivu ya kushindwa na muda mfupi ataanza safari ya kuendea mwanzo mpya.”

Ukurasa mpya

Baada ya kosa, anza ukurasa mpya. Kosa si mwisho wa kitabu bali mwisho wa sura, anza sura mpya.

“Usiombe ukamilifu katika kila ufanyacho, bali hekima ya kutorudia makosa,” alisema Brenda Sloat.

Hekima inaongea hata katika makosa kwa kuwa giza linatufundisha umuhimu wa mwanga.

Kuwa makinifu na mambo matatu kutoyachezea maana majina yanabadilika yakichezewa: roho, afya njema, na akili.

Roho ikitoka mtu anaitwa marehemu. Mtu akiugua anaitwa mgonjwa.

Akili ikipata kasoro au shida ya kiakili mtu anaitwa kichaa.

Makosa katika mambo hayo matatu ni mtihani mkubwa. Lakini tukumbuke kosa kubwa ni kila mara kukaa mkao wa kuogopa kukosea.