DINI: Usitishwe na wanaokusema vibaya,vumilia, huwezi kuridhisha kila mtu

DINI: Usitishwe na wanaokusema vibaya,vumilia, huwezi kuridhisha kila mtu

NA PADRE FAUSTIN KAMUGISHA

WATU milioni 50 wakisema jambo la kipumbavu bado ni jambo la kipumbavu,” alisema Anatole France (1844-1924).

Kusingiziwa na kusemwa vibaya ni mtihani. Ukifanya jambo zuri, utasemwa. Ukifanya jambo baya, utasemwa. Usipofanya lolote, utasemwa. Ukiwa na pesa kama njugu, utasemwa.

Usipokuwa na pesa, utasemwa. Ukipandishwa cheo, utasemwa, usipopandishwa cheo utasemwa. Ukipata mchumba, utasemwa. Usipopata mchumba, utasemwa.

Aliyevumbua mwavuli walimsema vibaya. Walimuita mchawi na kusema hanyeshewi na mvua. Wengine wanasemwa vibaya mpaka wanajiambia, “nina damu ya kunguni.”

Mtu akiwa mkarimu, wanasema anajitangaza. Asipokuwa mkarimu wanasema ana gundi kwenye vidole, ni mnyimi, ni bahili. Mtu akitoa hotuba fupi sana wanasema hakujiandaa.

Akitoa hotuba ndefu wanasema hatunzi muda. Akiwa mtoto mchanga wanasema ni malaika. Akiwa mtu mzima wanasema achana na yule shetani. Akiwa mcha Mungu wanasema ni mkatoliki zaidi ya Papa.

Asipokuwa mcha Mungu wanasema shetani amemweka mfukoni. Akiaga dunia katika umri wa ujana wanasema angefanya mengi mazuri. Akifariki umri wa uzeeni wanasema miaka yake aliiharibu tu bila kufanya chochote. Watu watakusema tu.Bwana wetu Yesu Kristu alisemwa vibaya na baadhi ya watu.

Yohane Mbatizaji alisemwa vibaya na baadhi ya watu. “Kwa kuwaYohane Mbatizaji alikuja, hali mkate wala hanywi divai,nanyi mwasema, ‘ana pepo’.Akaja mwana wa mtu; yeye anakula na kunywa, mkasema “Mwangalieni huyu mlafi na mlevi, rafiki ya watoza ushuru na wenye dhambi” (Luka 7: 33-34).

Yesu alikutana na watu ambao walimsema vibaya kama watu wazuri wanavyosemwa vibaya. Yesu alitetwa, alinung’unikiwa, alikataliwa, alinenwa. Kama alivoagua Nabii Simeoni, “Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi walio katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa.”

Kama unafanya mambo mazuri na watu wanakusema vibaya, fanya mambo yafuatayo hutaumia sana. Kwanza, usimridhishe kila mtu. Usimpendezeshe kila mtu. Binadamu si pesa ambayo hupendwa na kila mtu. Yesu Kristu hakupendwa na kila mtu. Naye hakuwa bendera ya kufuata upepo wa maneno ya watu.

Alikuwa na msimamo. Huwezi ukampendeza na kumridhisha kila mtu. Baba mmoja na mtoto wake wa kiume walimpeleka punda sokoni. Baba huyo alikaa juu ya mnyama na mtoto alitembea. Watu waliokutana nao njiani walilalamika, “Ni jambo baya sana: Pande la mtu, limekaa mgongoni mwa punda wakati mtoto mdogo anatembea”.

Kusikia hivyo baba huyo aliteremka toka mgongo wa punda mtoto alichukua nafasi yake. Watazamaji walitoa maoni yao. “Ni jambo baya sana: mzee anatembea, na mtoto amekaa”.

Kusikia hivyo wote wakawa wamempanda punda – wakawasikia wengine wakisema, “Ni ukatili ulioje: watu wawili wamekaa juu ya punda”. Kusikia hivyo wote waliteremka. Lakini watazamaji wengine walitoa maoni, “Ni ujinga ulioje: punda hana kitu chochote mgongoni na watu wawili wanatembea”.

Mwishowe, wote wawili walimbeba punda na hawakufika sokoni. Yesu hakuyumbishwa na maneno ya watu kama mzee huyo na mtoto wake.Pili, zingatia ukweli huu: watu hawautupii mwembe mawe usiokuwa na maembe. Watu hawapigi teke mbwa aliyekufa bali aliye hai. Watu hawautupii mawe mwembe usio na maembe.

Ukiwa na “matunda” watu watakutupia mawe ya maneno ya kukukatisha tamaa. Vumilia. Mvumilivu hula mbivu. Mama hupenda mtoto wake acheze ashangiliwe badala ya kuzomewa. Yesu alitukanwa.

Matusi hayo ni upanga uliochoma moyo wa Maria. Lakini alivumilia. Usiogope upinzani, kumbuka tiara huruka angani dhidi ya upepo na si pamoja na upepo.

Tatu, cheka tu. Kucheka ni dawa ya msongo wa mawazo. Kucheka ni dawa ya msongo wa mawazo unaosababishwa na kusemwa. Ukweli huo unabainishwa na mtunga kitabu cha Methali: “Moyo mchangamfu ni dawa,bali moyo wenye huzuni hudhoofisha mwili” (Methali 17:22).

Wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe huko Marekani aliyekuwa Rais wa Marekani wakati huo Abraham Lincoln alisema, “Pamoja na uchovu wa kuogopesha nilionao usiku na mchana, kama sitacheka nitakufa.”

Mtu akikusema vibaya, cheka tu. Ukisemwa na mtu cheka tu, mwambie, “kicheko hiki ningeshinda nacho,ningelala nacho, nimekitoa.” Cheka tu na ondoka mahali hapo.

You can share this post!

Mwili wa Magufuli kuwasili Dodoma Jumapili jioni

JAMVI: Changamoto tele kwa Kenyatta akijaribu kuzima ndoto...