Makala

DINI: Wakati wa Mungu kukujalia mema ukifika hakuna awezaye kuzuia, lako ni kuamini tu

January 25th, 2020 2 min read

Na WYCLIFFE OTIENO

MUNGU hutenda mambo na majira.

Kuna wakati mambo yanakuwa magumu sana, lakini kipindi hicho hakiwezi kudumu milele. Mwisho wa jambo ni mwanzo wa jingine. Mwisho wa siku ni mwanzo wa nyingine. Mwaka huanza Januari na mwisho wake ni Desemba.

Mwanzo hutupatia nafasi nzuri ya kutathmini yaliyopita, kusuka mawazo yetu vyema kuambatana na tunayotarajia. Mwanzo hutupa nguvu mpya ya kutenda jambo. Januari ni wakati wa kuweka mambo vizuri ili tuweze kusafiri vyema mwaka nzima.

Mwaka huu wa 2020 tuna sababu ya kumwamini Mungu kututendea makuu. Kwa kweli Mungu amekuwa mwaminifu na yafaa tumwamini hata katika yale hatujaona. Huenda ikawa hukuanza mwaka vizuri, lakini yafaa uamini kuwa huu utakuwa bora kuliko miaka iliyopita.

Katika Biblia kuna mambo mengi yamenakiliwa kufanyika baada ya miaka 20. Baadhi ya wasomi wa Biblia wanaamini kuwa 20 inaashiria ukamilifu wa wakati, haswa kusubiri jambo fulani katika hali ngumu. Wakati unapokamilika, jambo hilo lazima litendeke.

Kama vile mwanamke mjamzito husubiri wakati wake wa kujifungua kwa hamu, hata akipitia hali ngumu hatimaye siku hufika. Ujauzito huleta mabadiliko mengi. Kuna vyakula vitakataliwa, vingine vikipendwa. Kuna watu watakataliwa, wengine wakipendwa. Kuna vitu vitapendwa vingine vikikataliwa. Lakini ni kwa kipindi hicho tu.

Hatimaye mwana akishapatikana mambo hurudi kawaida na mama kusahau uchungu aliopitia sasa akiiingia kipindi cha kufurahia na kusherehekea.

Kuna mambo mengi labda umepitia katika miaka iliyopita, lakini huu ni wakati wako wa kumwamini Mungu kuwa mwisho umefika na unaingia kipindi cha kumfurahia Bwana.

Wakati wa kujifungua haijalishi mama yuko wapi, mtoto atatoka tu. Ndio maana wengine wamezaliwa njiani, hospitalini, nyumbani, darasani na popote pale, maana wakati ukifika hakuna awezaye kuzuia.

Yakobo alikaa katika utumwa chini ya mjomba wake Labani, hata malipo yake yakabadilishwa mara kumi.

Alimtaka Raheli ila akapewa Lea. Lakini kipindi chake cha miaka 20 kilipoisha alipata uhuru wake (Mwanzo 31). Nakuombea chochote kimekuweka katika utumwa, mwaka huu kikuachilie katika jina la Yesu!

Suleimani alikamilisha kazi yake ya ujenzi baada ya miaka 20 (1 Wafalme 6:38). Na katika mwaka wa kumi na moja, katika mwezi wa Buli (yaani mwezi wa nane) nyumba ikaisha.

Kwa muda wa miaka saba alikuwa katika ujenzi. “Sulemani alijenga nyumba yake mwenyewe kwa miaka 13, mpaka alipoikamilisha nyumba yake yote.” (1 Wafalme 7:1)

Siri ni kuwa alianza kwa kumjengea Mungu. Hatimaye alifaulu kujijengea. Mwaka huu ukitaka kufaulu katika miradi uliyo nayo, moyoni kwanza waza kuhusu mradi wa Bwana. Je, ni kazi gani utakayomfanyia Mungu mwaka huu.

Ukitaka Bwana aingilie mambo yako na kupigana vita vyako lazima uwe mkarimu. Ukipanda ukarimu, utavuna ukarimu.

Yabini mfalme wa Kanaani aliwatesa Waisraeli, lakini baada ya miaka 20 Mungu alimtumia Debora kuwaweka huru.

“Mfalme Yabini alikuwa na magari ya vita 900 ya chuma. Aliwakandamiza sana Waisraeli kwa miaka ishirini; nao wakamlilia Mwenyezi Mungu awasaidie.” (Waamuzi 4:3).

Siri ni, Waisraeli walipochoka walimlilia Bwana naye akasikia akawaokoa. Kinywa kilichofungwa ni hatima iliyofungwa. Ukitaka kuona ukombozi, lazima umlilie Bwana.

Maombi ni nguzo ya ushindi wako. Chochote kilichokuwa kikikutesa, nakuombea katika jina la Yesu kikuachilie mwaka huu ili ufurahie wema wa Bwana.

Mwaka huu unadhihirisha ukamilifu wa ukarimu na upendo wa Mungu. Kuwa tayari kupokea mambo ambayo hujawahi kuyaona.

Tengeneza uhusiano wako na Mungu kwa kumwamini Yesu aliyetufia msalabani. Amini neno lake, amini kuwa ana uwezo wa kubadilisha hali yoyote. Tembea na upange mambo ukiwa na imani kuwa Mungu aliyekufikisha umbali huu ana mpango mwema nawe.

Kumbuka bila imani huwezi kumpendeza Mungu. Usiogope kupanga mambo makubwa. Huenda ikawa hujachukua hatua yoyote ya maana tangu Januari ianze; usihofu kwani hujachelewa. Waweza kumuamini Mungu kwa mambo makuu sasa hivi na ukafaulu.