Makala

'Dini ya Akorino yajiuza kama inayoelewa maana halisi ya usasa'

September 10th, 2019 3 min read

Na MWANGI MUIRURI

KWA muda sasa, dini ya Akorino imekuwa ikihusishwa na dhana nyingi ambazo zingine ni za kutamausha.

“Kuna wale ambao wamekuwa wakituhusisha na umaskini na itikadi kali za kupinga usasa unaoletwa na mataifa ya Kimagharibi. Tumehusishwa hata na makundi haramu na pia kudhaniwa kama wasio na elimu kwa kuwa ni nadra sana upate Mkorino katika ajira ya serikali au katika kampuni kuu hapa nchini,” asema Hezekiah Ng’ang’a ambaye ni muumini wa dini hii.

Anakiri kuwa historia ya dini hii ndiyo imekuwa ikichangia kusambaa kwa dhana potovu kwa kuwa “ndio, kwa muda tumekuwa na shida kubwa ya kupanua mawazo yetu kama waumini.”

Anasema kuwa “tulianza na wale Akorino wa mwanzo waliojumuika katika itikadi kali za Kiratina (kiasili) na ambapo hatukuwa tunaabiri magari ya uchukuzi, hatukua tukiamini kuhusu madawa ya kizungu na pia, tuliamini hata wadudu kama funza hutumwa kuishi ndani ya miili yetu na Maulana.”

Lakini hiyo ni nembo ambayo tumejiondolea na leo hii tuko na mbunge wa Runyenjes akiwa ni wa imani yetu na ambapo hujitokeza bungeni akiwa na kilemba, tuko na madiwani kadhaa na katika afisi za kiserikali, utatupata.

Anasema kuwa “ule umaskini tumebakisha miongoni mwetu ni ule tu wa kawaida ambao huwakumba wengine wengi.”

Aidha, anasema kuwa leo hii watoto wa Akorino wanajiunga na vyuo vikuu na pia katika taasisi za juu za elimu kama watoto wa wengine na pia kwa pesa, “tuna mabwanyenye wetu na ambao umeona hata wakitusaidia kukutana na rais Uhuru Kenyatta na naibu wake, William Ruto.”

Anauliza: “Ni watu gani ambao ni hivihivi ambao watakutana na kiongozi wa taifa?”

Ni katika hali hiyo ambapo wengi wa Akorino wameungama kuwa kuna haja ya dini hii kuwaandama wote ambao wanaendelea kuwavuta katika tope la aibu kupitia mienendo potovu wakiwa na vilemba kwa vichwa vyao.

“Ndio tuko nao ambao hata sio wa imani yetu lakini hujifanya ni waumini wetu kwa kuvalia vilemba. Wanaingia hata ndani ya baa na kubugia pombe, wanaonekana ndani ya lojing’i wakiwa kwa maisha ya uzinifu na wanahusishwa na fini hii yetu tukufu,” ateta Askofu Wachira wa Rukemi ambaye huwa na kanisa lake mtaani Nyamakima jijini Nairobi.

Anasema kuwa waumini wa dini hiyo wamekuwa wakikongamana mara kwa mara na kwa kwa kauli moja wanasema hawatavumilia visa hivyo na watakuwa wakifadhili watakaonaswa kufikishwa mahakamani.

“Aidha, alisema kuwa kuna baadhi ya mapasta ambao wameandamwa na pepo kali la kushiriki mahaba na waumini hata wale ambao tayari wako kwa ndoa zao. Wengine wanatapeli waumini kwa ukora wa kawaidana kuwaacha wamesononeka kiuchumi. Kanisa sio danguro la matapeli na wahalifu wengine. Tunafaa kuwa mfano bora wa kuwa kiunganishi cha wafuasi wetu na Mwenyezi Mungu,” akasema.

Ubinafsi

Alisema baadhi ya madhehebu yanayochipuka kila kuchao yanaendeshwa na viongozi ambao wana ubinafsi na ambao hutumia madoido ya miujiza bandia na utabiri wautapeli kuwalaghai waumini wao.

Lakini waumini hawa bado wanateta kuwa baadhi ya idara za serikali kuu na zile za kaunti huwabagua katika utoaji wa nafasi za kazi hapa nchini kwa misingi ya dini.

Kuna tetesi kuwa kwa miaka mingi wao huwa ni wapiga kura pekee huku ikifika wakati wa kutoa nafasi za kula keki ya kitaifa wao husukumwa pembeni.

Walisema shughuli ya kusajili makurutu katika idara za usalama huwa hazihusishi dini hiyo, na wakati wafuasi wao hujitokeza katika mchakato huo kuomba kazi, huwa wanabaguliwa hadharani.

Kasisi James Mburu ambaye ndiye mwenyekiti wa dini hiyo katika eneo la Mlima Kenya na anasema serikali haitambui kwa undani kuwa dini hiyo iko na wafuasi zaidi ya 50,000 ambao wamesoma hadi vyuo vikuu lakini wengi ama ni madereva wa magari ya umma, vibarua katika mijengo au wanaongoza makanisa yao pamoja na kujitafutia riziki katika sekta ya utumbuizaji wa muziki.

Waumini hawa wanafurahia sensa wakisema kuwa huenda serikali ipate takwimu za uhakika kuwahusu na ipate habari za maana kuhusu uwezo wao wa kuwa wanahisa ambao sio wa kuiga katika ujenzi wa taifa hili.