Makala

DINI: Kusitasita ni uzembe unaofanya mambo rahisi kuonekana mazito mno, ni kama hayawezekani

February 23rd, 2020 2 min read

Na FAUSTIN KAMUGISHA

MANENO “Ningejua,” na “kusitasita” yakipandwa hayaoteshi chochote.

Kusitasita ni kutamani jana iendelee. Kusitasita ni kuzika “fursa” katika kaburi la sahau. Kusitasita ni mauaji ya neema. Kusitasita ni nukta katikati ya sentensi.

“Anza kushona na Mungu atakupa uzi” (Methali ya Ujerumani). Unapoanza, mambo mengine yanajipanga vizuri.

Ukisema, “nitafanya jambo siku fulani” kumbuka hakuna siku inaitwa fulani. Siku mojawapo, sio mojawapo ya siku za wiki.

Maneno haya husikika toka midomo ya watu wanaositasita: nitaanza kesho; sina kila kitu ninachohitaji; mazingira si sawa; ngoja nijipange; kesho ipo; haraka ya nini; haraka haraka haina baraka; nangoja wakati muafaka.

Kusitasita ni falsafa ya “siku fulani nitafanya.” Bila shaka mtunzi wa kitabu cha Zaburi cha Biblia alisikia maneno kama hayo ndiposa akasema, “Watu wa kusitasita nawachukia” (Zaburi 119:113).

Kusitasita kunafanya mambo mepesi kuwa magumu. Kusitasita kunafanya mambo rahisi kuwa mazito na mambo magumu kuwa hayawezekani.

Kuna methali ya Tanzania inayokariri kwamba, “Asemaye ngoja mnyama ajitokeze kabisa, huchoma mkia.”

Ukisitasita utaponyokwa na fursa.

Unapolala, nayo biashara yako inalala. Kusitasita ni kulala. Unaposimama, ndoto zako zinasimama. Kusitasita ni kuacha kutenda jambo baada ya kuonesha nia ya kutenda au baada ya kulianza. Acha kusimama, anza kutembea!

Kusitasita ni kujichelewesha, ila muda hauchelewi. Chelewa chelewa utamkuta mwana si wako.

“Unajua kinachotokea unapopendekeza wazo zuri kwa mtu anayesitasita? Hakuna chochote,” alisema Donald Gardener.

Ukingoja kujua kila kitu hutafanya lolote. Ukingoja wakati muafaka hutafanya lolote. Kusitasita ni kuingiwa na wasiwasi. Kusitasita ni binamu mvivu wa hofu. “Tunapokuwa na wasiwasi juu ya shughuli fulani, tunaiahirisha,” alisema Noelle Hancock.

Kesho ni siku ya wiki yenye shughuli nyingi sana. Unaposema utafanya jambo hiyo kesho, itakuwa imejaa shughuli zake. Huku kusema utalishughulikia jambo siku za usoni ni ishara ya uvivu, kutojipanga, kutojiamini, kutojithamini, kutokuwa na nidhamu ya kazi, kutojitambua na kutotambuliwa na wengine.

Kusitasita mara nyingi kunasababishwa na hofu ya kushindwa au hofu ya kushinda. Kushinda kunabeba kifurushi cha kuwajibika, kunaki kwenye mstari na kutegemewa na wengi.

Mambo yanayokupeleka juu huenda sio yatakufanya kubaki juu. “Kama una malengo lakini wasitasita, huna chochote. Kama una malengo na kuyafanyia kazi, una kila kitu unachotaka,” alisema Thomas J. Vilord.

Huwezi kulima shamba kwa kulilima kichwani tu. Lazima lionekane kwa macho ya mwili baada ya kuliona kwa macho ya akili.

Napoleon Hill ni mfano wa kuigwa wa mtu ambaye hakusitasita. “Kusitasita ni mazoea mabaya ya kuahirisha hadi kesho jambo ambalo lingefanyika juzi,” alisema Mwamerika huyu.

Amewabadili watu wengi kupitia kitabu chake cha Think and Grow Rich. Alizaliwa mahali ambapo umaskini ulikuwa unatawala. Akiwa na umri wa mika 10 mamake aliaga dunia. Baada ya miaka miwili baba alioa mke mwingine.

Tangia utotoni alikuwa na ndoto ya kuwa mwandishi. Aliweka akiba kidogo kidogo na kununua kamusi. Katika kamusi yake alinyofoa kipande cha karatasi kilichokuwa na neno, “impossible – haiwezekani” kwa kutumia mkasi.

Aliyajenga maisha yake kwa misingi kwamba: hakuna lisilowezekana. Akiwa na umri wa mika 13 alikuwa analiandikia gazeti la mahalia akijipatia fedha kidogo za kusoma.

Andrew Carnegie, ambaye alikuwa tajiri mkubwa sana wakati huo, alimpa kazi ya kuwahoji milionea 500 kugundua kanuni ya mafanikio ambayo ingetumiwa na mtu wa kawaida.

Baada ya kazi ya miaka 25 alitunga kitabu chake cha Think and Grow Rich. Kwa kifupi alichogundua ni kuwa, unavyofikiria ndivyo utakavyokuwa. Kuna saikolojia ya utajiri na mafanikio. Lazima unachokifikiria ukifanyie kazi ili ufanikiwe.

Yote tisa, nahitimisha kwa kumuunga mkono mtunzi wa Zaburi kwamba, “Watu wa kusitasita nawachukia”.