Michezo

Diogo Jota kusalia mkekani kwa wiki sita kuuguza jeraha la goti

December 14th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

SAJIILI mpya wa Liverpool, Diogo Jota, 24, sasa atasalia mkekani kwa kipindi cha wiki sita zijazo kuuguza jeraha baya la goti.

Fowadi huyo raia wa Ureno alipata jeraha hilo wakati wa mchuano wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) uliowakutanisha Liverpool na Midtjylland ya Denmark mnamo Disemba 9, 2020.

“Ni jeraha baya kuliko jinsi tulivyodhania awali. Japo hatahitaji kufanyiwa upasuaji, atakuwa nje kwa muda mrefu – pengine wiki sita au zaidi,” akasema kocha Jurgen Klopp.

Tangu aingie katika sajili rasmi ya Liverpool baada ya kuagana na Wolves mnamo Septemba 2020, Jota amefungia waajiri wake wapya mabao tisa.

Anaungana sasa na orodha ndefu ya wanasoka wa Liverpool wanaouguza majeraha wakiwemo Virgil van Dijk, Joe Gomez, Konstantinos Tsimikas, James Milner, Thiago Alcantara, Xherdan Shaqiri na Joel Matip.

Jota anaingia mkekani kuuguza jeraha baada ya kipa Alisson Becker na kiungo Alex Oxlade-Chamberlain kupona na kurejea katika kikosi kilichotegemewa na Liverpool dhidi ya Fulham katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Disemba 13, 2020 uwanjani Craven Cottage. Mechi hiyo ilimalizika kwa sare ya 1-1.