Bambika

Director Trevor, Mungai Eve waendelea kuwapa mashabiki sinema ya bure

February 20th, 2024 1 min read

NA FRIDAH OKACHI

UTATA unaozingira akaunti ya YouTube ya Director Trevor na mwigizaji Mungai Eve umefanya wengi kutafakari na kutoa maoni yao kuhusu athari za kuchanganya mapenzi na biashara.

Kabla ya kufarakana, wawili hao waliwahi kufichua kwamba akaunti hiyo ilikuwa ikiwaingizia Sh700,000 kila mwezi.

Lakini sasa hali ya suitofahamu inakumba akaunti hiyo baada ya Bonaventure Monyancha almaarufu Director Trevor kutangaza mabadiliko kwenye mtandao wa Mungai Eve Media akisema utafahamika kama Kenya Online Media.

Director Trevor alitoa tangazo hilo Jumatatu jioni, mwenye umri wa miaka 24 alichapisha jumbe kadhaa kwenye mitandao ya kijamii akidai Kampuni ya Kenya Online Media hahitaji huduma za Eve Mungai.

“Je, uko tayari? Taarifa rasmi itashuka kesho,” alitangaza Director Trevor.

“Hapana! Huduma zake hazihitajiki tena kwenye mifumo ifuatayo, YouTube yenye wafuatiliaji 754k, Insta Fame 104k, Facebook 874k,” akasema Director Trevor akijibu baadhi ya mashabiki waliomwelekezea maswali mitandaoni.

Katika taarifa nyingine, mtaalamu huyo wa mitandao ya kijamii alionekana kumrushia vijembe Mungai Eve, akidokeza kuwa mrembo huyo mwenye umri wa miaka 23 anafurahia matunda ya mti alioupanda muda mrefu uliopita.

“Kuna mtu ameketi kivulini leo kwa sababu mtu alipanda mti muda mrefu uliopita,” akarusha vijembe.

Hatua ya hivi punde imechochea hisia mbalimbali kuhusu biashara na mapenzi.

Wanawake wapendwa, msichanganye mapenzi na biashara,” akashauri Diana Kamande akimtaka Mungai Eve kuelekea mahakamani.

Alishauri wanawake kuepuka kuweka zingatio la maisha karibu na mwanamume, la sivyo “itakula kwako.”

“Kama haya yote ni kweli, nasimama na Mungai Eve kwa sababu amejituma sana kujenga chapa yake,” akaongeza.

Kwa upande wake Scola Shiru, alichangia akiwa na imani Mungai Eve atasimama tena na kuibuka mshindi.

Naye Liliyan Nyambu ni miongoni mwa wale wanafahamu yanayofanyika baada ya kuhusisha mume wake kwenye biashara.

“Kuanza biashara pamoja ni porojo… Nilijua hilo baada ya kuwekeza na mchumba….Wueh! Acha ninyamaze. Kile kitu ambacho nahusika naye ni watoto tu!” akasema Liliyan Nyambu.