Michezo

Dirisha la uhamisho EPL kufunguliwa Julai 25

July 21st, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

VINARA wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) wamethibitisha kwamba kipindi cha uhamisho wa wachezaji kwa minajili ya kampeni za muhula ujao sasa kitakuwa kati ya Julai 25 na Oktoba 5, 2020.

“Washikadau wa EPL wameafikiana kuhusu tarehe mpya zitakazowapa washiriki wa kipute hicho muda wa kujishughulisha sokoni kwa minajili ya kujisuka upya kwa ajili ya kampeni za muhula ujao. Kipindi cha muhula huu kitakuwa cha wiki 10, kuanzia Julai 27 na Oktoba 5,” ikasema sehemu ya taarifa iliyotolewa na wasimamizi wa EPL.

Tarehe hizo zinaafikiana pia na ratiba ya Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga), Uhispania (La Liga) na Italia (Serie) ambazo zimefichua kwamba Oktoba 5, 2020 itakuwa siku ya mwisho ya uhamisho kwa wanasoka wote wanaopania kuondoka au kujiunga na vikosi vinavyonogesha soka ya mataifa hayo.

Ina maana kwamba klabu zitakazoshiriki kivumbi cha EPL msimu ujao zitakuwa na wiki 10 pekee kujishughulisha sokoni kabla ya kipenga cha kuashiria mwanzo wa muhula ujao wa 2020-21 kupulizwa.

“Baada ya kushauriana na vinara wengine wa soka ya Uingereza, usajili wa ndani kwa ndani miongoni mwa wachezaji wa ligi za madaraja ya chini pekee nchini Uingereza ndio utakaoruhisiwa kufanyika kati ya Oktoba 5 hadi Oktoba 16. Vikosi vitakuwa na uwezo wa kurasimisha mikataba ya kudumu au ya mikopo kutoka ligi za chini za EPL wakati huo. Itakuwa haramu kwa vikosi kusajili wanasoka wa kutoka klabu nyinginezo za EPL,” ikaongeza taarifa hiyo.

Mapendekezo hayo ya EPL hata hivyo, yatasubiri hadi Julai 18, 2020 kuidhinishwa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).