Habari Mseto

Diwani adai maafisa wa utawala Malindi ni wazembe

February 20th, 2024 2 min read

NA ALEX KALAMA

HUKU visa vya uhalifu vikizidi kuongezeka katika baadhi ya maeneo ya mji wa Malindi, mwakilishi wa wadi ya Shella mjini Malindi Twahir Abdhulkarim sasa anawalaumu baadhi ya maafisa wa utawala eneo hilo, akidai kuwa wamezembea huku uhalifu ukishamiri.

Diwani alitoa kauli yake baada ya chifu wa eneo hilo la Shella Nichodemus Mwayele kukiri kuwa eneo hilo limekuwa na magenge ya uhalifu yanayotatiza usalama kutokana na uraibu wa mihadarati.

Chifu wa Shella Nicodemus Mwayele (mbele kulia) akiwa katika kikao cha mkutano wa baraza mapema kabla ya kuondoka baada ya majibizano makali. PICHA | ALEX KALAMA

Bw Abdhulkarim amesema kuwa ni sharti vitengo vya usalama kufanya uchunguzi wa kina kuhusu swala hilo kabla ya kutoa kauli hizo kwa umma huku akiilaumu idara ya usalama kwa kuzembea katika utekelezaji wa majukumu yake.

“Nataka kumwambia Msaidizi wa Naibu Kamishna wa Malindi kwamba sisi hatuzuii polisi kufanya uchunguzi au kudharau kitengo cha ujasusi katika nchi hii. Mihadarati ambayo vijana wanauziwa ndio inawafanya washikie watu mapanga. Hazitengenezwi hapa bali zinafanya kuletwa na zinauzwa hata kwenye maduka ya kuuza dawa,” akasema Bw Abdhulkarim.

Aidha, diwani huyo wa Shella ambaye pia ni naibu kiongozi wa wengi katika bunge la Kilifi anasisitiza kuwa sharti maafisa wa utawala pamoja na idara ya usalama eneo hilo kuwajibika kikamilifu.

“Tatizo kubwa kuzorota kwa usalama limechangiwa na utumizi na uuzaji wa mihadarati. Suluhisho ni walanguzi wa dawa za kulevya kukomeshwa. Machifu hawataki kuwataja majina walanguzi ilhali wanajulikana. Machifu msiogope kwa sababu polisi wanaenda pale wapewe chao waende na hii ndio shida,” akaongeza.

Aidha diwani huyo alidokeza kuwa maafisa wa usalama katika mji wa Malindi wamegeuka kuwa kero kwa wananchi kwani baadhi yao wamekuwa wakorofi kiasi cha kwamba wanahangaisha wananchi bila sababu.

“Polisi wamekuwa wakorofi wa kuwawinda watu wanaoenda msikitini kuswali,” akadai.

Badala yake akashauri, “Zunguka hapa Malindi saa sita, saa saba za usiku utaona wakora wako tele wamejaa. Hatuoni polisi hapa usiku, polisi hawazunguki kazi yao ni kuenda huko kulinda wadosi. Tunataka polisi wazunguke usiku washike wahalifu sio saa mbili za usiku mtu anaenda kuchukua mkate kwa duka anashikwa na kupelekwa kituoni ukienda kusema huyu muachilieni sio mhalifu unaambiwa hatoki mpaka Sh2,000 au Sh3,000 ndipo aachiliwe.”

Kauli yake diwani huyo ilipingwa vikali na msaidizi wa naibu kamishna eneo la Malindi Irene Munyoki (Acc) pamoja na Bw Mwayele ambao walisisitiza kuwa eneo hilo limegeuka kuwa pango la wahalifu.

“Hatuwezi kukubali watoto waharibike, hatuwezi kukubali mangweni kuwa karibu na makazi ya watu. Na tumewapatia njia mbadala juzi tulikuwa na kikao kama hiki kule Muyeye eneo linaitwa Mkanju wa Nyege na tukawaelezea wale ambao wanauza mnazi pale ya kwamba hatutaki kuona mangweni hapo na tuliwaonyesha sehemu nyingine mbadala ambayo wanaweza kupeleka biashara yao huko na wateja wao wakawafuata huko lakini sio pale,” alisema Bi Munyoki.

Majibizano hayo yalishuhudiwa katika mkutano wa baraza uliowaleta pamoja viongozi wa serikali ya kitaifa na wale wa kaunti ya Kilifi mjini humo ili kujadiliana jinsi ambavyo wataweza kushirikiana katika kufanya miradi ya maendeleo pamoja na kuimarisha usalama katika eneo hilo.

Bi Munyoki na Bw Mwayele waliondoka kabla mkutano huo kutamatika.

Kutofautiana kwa viongozi hao kumejiri wiki chache baada ya baadhi ya vyombo vya habari kutoa orodha ya majina ya makundi ya kihalifu ambayo yamekuwa yakihangaisha jamii kwa kuwavamia watu na kuwakatakata mapanga na kisha kuwanyang’anya mali zao.