Habari Mseto

Diwani akanusha mashtaka 6 ya ulaghai Murang'a

March 28th, 2018 1 min read

Diwani kutoka kaunti ya Murang’a Peter Mburu Muthoni almaarufu Soloman Kamau Nyingi akiwa kizimbani aliposhtakiwa kwa kumlaghai mfanyabiashara Sh2.2 milioni. Picha/ Richard Munguti

Na RICHARD MUNGUTI

MWAKILISHI wa wadi katika kaunti ya Murang’a (MCA) aliachiliwa huru katika kesi inayomkabili ya kumlaghai mfanyabiashara Sh2.2milioni akidai angemuuzia Lori la kubebea bidhaa.

Bw Peter Mburu Muthoni almaarufu Solomon Kamau Nyingi  alifikishwa mbele ya hakimu mwandamizi Kennedy Cheruiyot.

MCA huyo alikamatwa na afisa wa idara ya kupambana na makosa ya jinai alipomwona mahakamani katika kesi nyingine inayomkabili.

Bw Muthoni amekanusha mashtaka sita ya kumlaghai Bi Alice Penninah Wangui Guchu Sh2,295,000, kughushi agizo la korti iliyoruhusu kuuzwa kwa lori hilo, kujifanya Bw Solomon Kamau Nyingi na kughushi kitambulishi cha Nyingi.

Kibali cha kumtia nguvuni MCA Muthoni kilitolewa mnamo Machi 12, 2018.

Hakimu alimwachilia  kwa dhamana na kurodhesha kesi kusikizwa Mei 30.