Diwani ang’olewa uongozini kutokana na hongo

Diwani ang’olewa uongozini kutokana na hongo

Na RICHARD MUNGUTI

DIWANI (MCA) wa Wadi ya Karen kaunti ya Nairobi Bw David Njilithia Mberia Alhamisi alipoteza kiti chake baada ya kusukumwa jela miaka mitatu kwa ufisadi wa ulaji rushwa ya Sh0.2m.

Bw Mberia alipokea adhabu hiyo baada ya kupatikana na hatia ya kudai hongo ya Sh1milioni na kupokea Sh200,000 kutoka kwa Bw Samuel Maina

Bw Mberia alidai hongo hiyo kushawishi kamati ya utamaduni na huduma za jamii katika kaunti ya Nairobi yenye wanachama 20 wasivuruge umiliki wa ardhi ambayo Bw Maina amejenga shule za kibinafsi.

Bw Mberia alikuwa ameshtakiwa pamoja na Madiwani Jared Okoth (Wadi ya Mathare Kaskazini) na Abraham Mwangi Njihia (wadi ya Woodley-Kenyatta) ambao waliachiliwa.

Wote watatu walikuwa wameshtakiwa kwa kula njama za kudai hongo ya Sh1milioni kutoka kwa Bw Kiragu.

Akipitisha hukumu hakimu mwandamizi Bw Thomas Nzioki alisema , Bw Mberia ni afisa wa Umma na sheria za kuangamiza ufisadi zahitaji mmoja akipatikana na hatia ang’atuliwe katika wadhifa wake.

“Wewe Bw Mberia ni afisa wa umma na chini ya Kifungu cha sheria nambari 18 za sheria za kupambana na ufisadi vile umepatikana na hatia na kuhukumiwa sasa utapoteza wadhifa wako wa MCA wa Karen. Hii mahakama itawasilisha nakala ya uamuzi huu kwa Spika wa Bunge ya Kaunti ya Nairobi akitangaze wazi kiti cha Wadi ya Karen,” aliamuru Bw Nzioki.

You can share this post!

Video za ngono zihalalishwe mitandaoni – AKS

Mkuu wa hospitali aamriwa amfikishe Sonko kortini