Habari Mseto

Diwani na mgonjwa washangaza kutoroka matibabu

June 4th, 2020 1 min read

Na IAN BYRON

DIWANI mmoja katika Kaunti ya Migori pamoja na mgonjwa wa Covid-19 wanasakwa baada ya kutoweka kwa kituo cha matibabu.

Maafisa wa kushughulikia wagonjwa wa virusi vya corona kwa sasa wanashirikiana na polisi kuwatafuta wawili hao waliotoroka kutoka kituo cha Macalder hapo Jumatano.

Waziri wa Afya katika kaunti hiyo Isca Oluoch alisema diwani huyo, ambaye alikuwa ametangamana na mgonjwa huyo alitorokea nchini Tanzania hapo wikendi baada ya kung’amua kuwa alikuwa atatafutwa ili kutengwa.

Kulingana na DkT Oluoch, MCA huyo alienda mafichoni baada ya kutangamana an wagonjwa watatu wa corona Jumamosi.

Afisa huyo aliambia Taifa Leo kuwa mgonjwa huyo alihepa kutoka kituo hicho saa kumi na mbili unusu alfajiri na hajulikani alikoelekea.

“Tumewaita maafisa wa polisi kutusaidia kumpata mgonjwa huyo ili arudishwe kwa kituo cha matibabu,” alisema.

“Hii ni mara ya kwanza kwa mgonjwa kutoroka kutoka kituoni baada ya kupatikana na virusi hivyo. Inasikitisha mno.”