Habari

Diwani wa chama tawala aaibika wakazi wa Kariobangi Sewage kufurushwa katika kipindi kigumu

May 3rd, 2020 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

ZAIDI ya wakazi 12, 000 kutoka mtaa wa mabanda wa Kariobangi Sewage wanakodolea macho kupoteza makao baada ya serikali kuwatangazia makataa ya saa 24 wawe wamehama eneo hilo linalopakana na eneo kuu la kusafisha majitaka la Kariobangi jijini Nairobi ama watolewe kwa nguvu.

Baadhi ya wenyeji wanasema wako tayari kuhama, ingawa wanalalamika kuwa hawakupewa muda wa kuondoka wala notisi na kuongeza kuwa hawana pa kuenda wakati huu mgumu wa janga la virusi vya corona.

“Sio eti tumekataa kuhama, lakini kuambiwa kwa ghafla tuondoke chini ya saa 24 zijazo na hata hatujalipa kodi ya nyumba hapa kwa sababu hatuna kitu wakati huu, si haki. Tutapata wapi fedha za kukodisha nyumba wakati huu tunapohitai kusaidiwa. Hali yetu ya kiuchumi ni mbaya sana,” mkazi mmoja alisikika akisema.

Mama mmoja kwa jina Georgina Wanjiru aliambia ‘Taifa Leo’ kuwa Baraza la Jiji la Nairobi liliwapatia eneo hilo mwaka wa 1996 kupitia kikundi cha Kariobangi Sewage Farmers, ambacho walikuwa wameanzisha miaka ya ’70 na kuwekeza fedha zao, baada ya kukufanyiwa usoroveya.

“Tulipewa hata hatimiliki na sisi ni tofauti kabisa na eneo la kusafisha maji taka la Kariobangi,” alisema.

Saa chache baada ya chifu wa eneo hilo kusisitizia wakazi wa eneo hilo wanafaa kuondoka haraka iwezekanavyo, diwani wao Julius Maina alifika mahali hapo na kuwahutubia akisema kuwa anaibika kuwa katika chama cha Jubilee kinachoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta.

“Naaibika kuwa MCA wa Jubilee kwa sababu inakuwaje kinafurusha watu wangu wa Kariobangi Sewage wakati huu wanapitia changomoto nyingi. Pia, kuna janga la virusi vya corona. Badala ya kuwaletea chakula na kuwasaidia wakati huu mgumu, inataka kuwaondoa kwa lazima. Hakuna notisi tumepewa. Kitendo hiki ni cha aibu sana,” alisema kiongozi huyo mbele ya maelfu ya wakazi wa eneo hilo.

Diwani Julius Maina (Jubilee) ahutubia wakzi wa Kariobangi Sewage waliofurushwa Mei 3, 2020. Picha/ Geoffrey Anene

Kabla ya kuondoka, Bw Maina aliwataka wakazi wasikubali hatua ya kuondolewa wakati huu.

Mtaa huo unapakana na soko la Korogocho, eneo la kusafisha majitaka, barabara ya Komarock na viwanda vya Kariobangi North.

‘Taifa Leo’ ilishuhudia baadhi ya wakazi wakiamua kuhama wakitumia pikipiki na mikokoteni, huku wengi wakisubiri kuona kitakachotokea baadaye Jumapili (Mei 3).

Kuna fununu kuwa maafisa wa polisi watatumwa katika eneo hilo Jumapili usiku kutekeleza amri ya kubomoa nyumba hizo za mabati na kuondoa wakazi, ambao hatawakuwa wamehama.