Diwani wa Korogocho kujua hatma yake kesho Jumatano

Diwani wa Korogocho kujua hatma yake kesho Jumatano

NA RICHARD MUNGUTI

DIWANI wa wadi ya Korogocho (MCA) Absalom Odhiambo Onyango almaarufu Matakwey au Mobimba atajua hatma yake kesho Jumatano mahakama itakapoamua ikiwa atazuiliwa kwa siku saba kuchunguzwa madai ya kuchochea ghasia na hujuma nyinginezo dhidi ya Serikali.

Huku Bw Onyango akifikishwa kortini madiwani wa muungano wa Azimio “waliitaka serikali ikome kuwahangaisha wanasiasa wasio na tajriba ya juu bali iwatie nguvuni vinara wa Azimio Raila Odinga, Martha Karua, Stephen Kalonzo Musyoka na Wycliffe Oparanya.”

Mawakili Danstan Omari na Samson Nyaberi waliomwakilisha MCA huyo waliikejeli serikali wakisema “imeanza kutekeleza dhuluma dhidi ya wananchi wasio na hatia.”

Wakimsihi hakimu mwandamizi Bw Gilbert Shikwe amwachilie kwa dhamana Bw Onyango.

Mabw Omari na Nyaberi walipinga vikali hatua ya idara ya uchunguzi wa jinai (DCI) wakisema “hawana sababu za kumzuilia MCA.”

Mawakili hao walimweleza hakimu “hakuna ushahidi wowote uliowasilishwa kortini kumwezesha amnyime MCA dhamana na kuagiza azuiliwe korokoroni.”

Wakili Omari alidai kortini kutiwa nguvuni kwa Onyango kunatokana na sababu za kisiasa.

“Leo ni siku ya kwanza ya serikali ya Kenya Kwanza kutumia vibaya mamlaka yake. Tunaomba hii mahakama isimame kidete na kukataa kutumiwa vibaya na wanasiasa ama kutweza haki kwa misingi ya kisiasa,” alisema Bw Omari.

“Tunaomba idara ya mahakama isimame kidete na kudumisha haki na mahakama hazipasi kutumika kusuluhisha tofauti za kisiasa. Tunaomba mahakama imwachilie Onyango kwa dhamana,” Bw Omari alimrai hakimu.

Mahakama ilielezwa ifutilie mbali madai ya polisi kwamba MCA Onyango atatoroka.

Akasema Nyaberi: “Huyu mshukiwa ni MCA wa wadi ya Korogocho. Yuko na makazi jijini Nairobi na polisi wakimtaka wanajua kule watampata. Polisi watampata katika bunge la kaunti ya Nairobi. Huyu mshukiwa ni Mheshimiwa na kiongozi aliyechaguliwa na wananchi.”

Mawakili hao walipuuzilia mbali madai Onyango anashirikiana na watu wengine kula njama za kuvuruga amani na biashara.

“Madai ya polisi eti MCA Onyango atavuruga amani ni mbwembwe tu zisizo na msingi wowote. Mwachilie kwa dhamana. Atatii maagizo ya hii mahakama,” Bw Nyaberi alisema.

Bw Onyango alidaiwa alitoa matamshi ya uchochezi wakati wa mkutano katika jumba la Chungwa House lililoko Capitol Hill.

Afisa anayechunguza kesi hiyo Sajini Francis Mwita alieleza hakimu wanachunguza kesi ya uchochezi na matamshi ya kuzua hisia za kikabila kwa lengo la kuvuruga amani.

Bw Onyango adaiwa alitoa matamshi hayo mnamo Januari 25, 2023 katika eneo la Capitol Hill.

Anadaiwa alisema: “Kwa siasa ya Taifa tunataka tutoke kwenda ikulu tutoe huyu mwizi, nataka tuingie town tufunge biashara, hakuna biashara itaendelea hii town ya Nairobi, ndio William Ruto (the President) aheshimu Raila Odinga (Azimio la Umoja leader). Lazima tufunge biashara hii town.”

Mahakama iliombwa iamuru azuiliwe na polisi kwa siku saba wachunguze simu yake na kutambua aliowapigia na kile walichopanga.

  • Tags

You can share this post!

Jinsi alivyoanzisha kituo cha michezo kuzuia watoto kuwa...

Real Madrid wakabwa koo na Sociedad katika La Liga ugani...

T L