Habari Mseto

Diwani wa Shimo la Tewa mashakani kufuatia tukio la mwanamume kupigwa mawe hadi akafa

June 3rd, 2024 2 min read

NA MAUREEN ONGALA

DIWANI katika Bunge la Kaunti ya Kilifi yuko matatani kutokana na madai ya kumpiga mwanamume kwa mawe hadi akafa wakati wa mzozo wa umiliki wa ardhi.

Mnamo Jumamosi, MCA wa wadi ya Shimo la Tewa, Bw Haron Thethe, alibahatika baada ya Naibu Gavana wa Kilifi Flora Chibule na Spika wa Bunge la Kaunti Teddy Mwambire kuwasihi maafisa kutoka kwa Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) kutomkamata hadharani ili kulinda heshima yake.

Viongozi hao wawili walipata habari kuhusu mpango wa kukamatwa kwa diwani huyo na wakaahidi kumwasilisha kwa wachunguzi baadaye.

Jaribio la kumkamata Bw Thethe lilizua hali ya wasiwasi wakati wa sherehe za Madaraka huku wenyeji na viongozi wakiongozwa na Seneta wa Kilifi Stewart Madzayo wakishutumu serikali ya kitaifa na mashirika ya usalama kwa madai ya kuwalinda matajiri huku wakihangaisha jamii wanaopigania haki za kumiliki ardhi.

“Bw Kamishna wa Kaunti, kwa sasa, Gavana hayupo na ninamwakilisha. Ikiwa kuna jambo lolote linalomlenga kiongozi yeyote hapa nataka kuambiwa, na iwapo kuna tatizo lolote kwa kiongozi yeyote nitamwasilisha kwenu,” Bi Chibule alisema.

Polisi walithibitisha kuwa, MCA huyo atafunguliwa mashtaka ya kuua bila kukusudia baada ya kuhusishwa na kifo cha mwendesha bodaboda wa Mtwapa ambaye alipigwa jiwe wakati wa mzozo wa ardhi ya umma inayozozaniwa Mtwapa.

Afisa Mkuu wa Upelelezi wa Uhalifu katika Kaunti ya Kilifi, Bw David Siele, alisema walikubaliana kuwa, viongozi wa kaunti watamwasilisha diwani huyo katika kituo cha polisi cha Mtwapa ifikapo Jumatatu.

“Tulimpigia simu MCA na kumfahamisha kuwa faili yake ilikuwa tayari na angejisalimisha na kujiwasilisha kwa polisi ili kurekodi taarifa na kwenda mahakamani,” alisema.

Tukio hilo lilitokea Machi 27, wakati Katibu katika Idara ya Utamaduni ya Kitaifa, Bi Ummi Bashir, Mwenyekiti wa Bodi ya Makavazi ya Kitaifa ya Kenya Edwin Abonyo, Mkurugenzi wa Makavazi ya Kitaifa nchini Prof Mary Gikungu, na wengine walipotembelea eneo la kihistoria la Jumba Ruins ili kubainisha ukweli kuhusu madai ya unyakuzi wa ardhi.

Umiliki wa sehemu ya ardhi hiyo unazozaniwa kati ya mwekezaji wa kibinafsi na Makavazi ya Kitaifa ya Kenya.

Shahidi ambaye hakutaka kutajwa jina alidokeza kuwa mwendesha bodaboda alikuwa akiwasafirisha baadhi ya vijana kwenda eneo hilo.

Wakati huo, MCA alikuwa na kikundi kingine cha vijana wakipinga madai ya unyakuzi. Makabiliano yalizuka kati ya makundi hayo mawili hasimu ya vijana.

“Makundi hayo mawili yalikabiliana na kuanza kurushiana mawe. Katika fujo hizo jiwe lilimpiga mwendesha bodaboda aliyelazwa hospitalini na kufariki siku mbili baadaye,” akasema.