Makala

DJ CUTS: Namshukuru Mola kunifungulia njia ya kuwatumbuiza Wamarekaniusanii

November 14th, 2020 2 min read

Na JOHN KIMWERE

ALIANZA kama mzaha lakini sasa ni kati ya madijei wanaotikisa anga la muziki wa burudani jijini Washington DC, Marekani. Lenny Muthama maarufu DJ Cuts anasema katika kazi ya U-DJ amepania kukuza talanta yake kufikia upeo wa DJ Puff mzawa wa Barbados Amerika Kusini.

Ingawa alipendelea kucheza mpira wa wavu na soka akiwa shuleni baadaye alipata msukumo wa hisia za mapenzi yake katika muziki bila kuzingatia hajawahi kutunga wimbo wowote.

Hata hivyo bado ni mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha California, Marekani anakosomea kuhitimu kwa shahada ya msanifishaji maumbo (Graphic Designer). Kando na hayo anamiliki brandi yake inayofahamika kama ‘Sherehesheria’ aliyoanzisha mwaka 2013 lakini aliisajili rasmi mwaka uliyopita.

“Nikianza kazi ya U-DJ nilikuwa nikitoa mixtape (nyimbo) na kuziuza kwenye magari za matatu jijini Nairobi ambapo kamwe haikuwa mteremko,” alisema na kuongeza kuwa penye nia pana njia maana mwaka 2013 alianza kucheza miziki mbali mbali katika kumbi za burudani jijini Nairobi. Anasema alikuwa akitoa santuri za miziki ya Dancehall, Reggae, Bongo, Hiphop na RnB.

Kipindi hicho anajivunia kufanya kazi ya U-DJ kwenye kumbi kadhaa ikiwamo Tajmall Sports Bar, Sizzling Grills na Blak Diamond kati ya zingine.

Msanii huyu anadokeza kuwa kama DJ anajivunia kufanya kazi na Serikali kupitia wizara mbalimbali katika ukumbi wa KICC. ”Kando na kufanya kazi na idara za serikali pia nimefanya kazi na brandi zingine nyingi kama Kampuni ya EABL, Barclays Bank na Sweppes katika ukumbi wa Uhuru Gardens, Nairobi.”

REDIO DALSAN

Nyota yake ilianza kumwangazia mwaka 2016 pale mteja mmoja alipomuuliza kama angependa kufanya kazi na redio moja nchini Somalia.

”Ilikuwa kama miujiza maana baada ya kuzungumza na mteja huyo aliyenipata katika ukumbi wa Tajmall Sports baadaye nilijiunga na Redio Dalsan jijini Mogadishu nchini Somalia nilikofanya kwa kipindi cha mwaka mmoja na nusu.” Baadaya mkataba huo kukaamilika ndio milango alianza kupata shoo za nje ya bara Afrika.

Nchini Marekani hupiga shoo zake katika maeneo tofauti ikiwamo Washington DC, NorthCarolina, Maryland, Virginia, Boston na Puerto Rico.

Msanii huyu hucheza nyimbo za mitindo tofauti ikiwamo ‘Hiphop’, na ‘RnB’, anaposema kuwa ndizo zinafahamika na wengi eneo hilo. Anasema eneo hilo wafuasi wa shoo zake ni wazawa kutoka mataifa ya Kenya, Jamaica, Caribeans, Marekani na Hispania.

KUSAJILI WAKENYA

Anasema ndani ya miaka mitano ijayo anataka kuona madj wengi kutoka Kenya waliopiga hatua pia wanaokuja wakipiga shoo za muziki wa burudani Marekani.

”Chini ya brandi yangu tayari tumeanza kusajili madj wa Kenya ili kuweka mikakati ya kuhakikisha wanapata nafasi kuendeleza taaluma yao nchini Marekani,” akasema. Anashauri madj chipukizi kuwa ili kufikia kiwango cha kimataifa wanahitaji kuonyesha nidhamu ya hali ya juu. Kadhalika lazima wajiepushe kuchanganya masuala ya kazi na mapenzi.