Habari za Kitaifa

DJ Mfalme aondolewa lawama ya mauaji ya polisi

April 8th, 2024 1 min read

NA RICHARD MUNGUTI

MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma (DPP) Renson Igonga amemwondelea kesi ya mauaji ya afisa wa polisi Felix Kintosi mcheza santuri Joseph Mwenda Munoru almaarufu DJ Joe Mfalme.

DPP Igonga alieleza mahakama ya Kibra, Nairobi kwamba ushahidi uliowasilishwa katika afisi yake na DPP na wachunguzi “hauna mashiko kisheria kuwezesha afisi yake kumfungulia mashtaka ya mauaji DJ Joes Mfalme.”

Badala yake, DPP alieleza hakimu mkuu Margaret Murage kwamba “DJ Joes Mfalme atakuwa shahidi katika kesi atakayoshtakiwa baonsa wake Allan Ochieng.”

Wakati DJ huyo alipofikishwa kortini mnamo Aprili 8, 2024 ili afisi ya DPP itoe mwanga kuhusu kilichosababisha kifo cha afisa wa polisi Kintosi, hakimu alifahamishwa “uchunguzi uliofanywa na kukamilishwa ulimlenga Allan Ochieng peke yake atakayeshtakiwa kwa mauaji.”

Ochieng atapelekwa katika Mahakama Kuu Kiambu atakaposhtakiwa kwa mauaji.

“Naomba hii mahakama ifunge faili ya uchunguzi dhidi ya DJ Mfalme na washukiwa wengine watano. Hakuna ushahidi wa kuwezesha DPP kumfungulia shtaka la mauaji DJ Mfalme,” kiongozi wa mashtaka alimweleza Bi Murage.

Hata hivyo, baonSa wake Allan Ochieng atafunguliwa shtaka la kumuua afisa wa polisi Felix Kintosi mnamo Machi 16, 2024.

Bw Kintosi alikuwa akihudumu kama afisa katika Kitengo cha Uchunguzi wa Uhalifu na Jinai (DCI).

Ochieng atafikishwa katika Mahakama Kuu ya Kiambu kujibu shtaka la mauaji linalomuandama.

DJ Mfalme aliachiliwa pamoja na washukiwa wengine watano, miongoni mwao maafisa watatu wa polisi.

DJ Mfalme aliyekamatwa pamoja na watu wengine sita kwa mauaji ya afisa wa polisi Inspekta Kintosi walizuiliwa korokoroni kwa siku 14 ili makachero wakamilishe uchunguzi.

DJ Mfalme alifikishwa mbele ya Bi Murage pamoja na Ochieng, Simon Wambungu na Eric Gathua.

Mbali na DJ Mfalme, maafisa watatu wa polisi Khadija Abdi Wako, Sammy Rotich na Agnes Mogoi pia walifikishwa kortini.