DKT FLO: Homa ya mapafu inavyosambaa mwilini, dalili na jinsi ya kuibaini

DKT FLO: Homa ya mapafu inavyosambaa mwilini, dalili na jinsi ya kuibaini

Mpendwa Daktari,

Homa ya mapafu (Nimonia) husambaa vipi?

Irene, Nairobi

Mpendwa Irene,

Nimonia ni ugonjwa unaoathiri moja au mapafu yote na husababishwa na bakteria, virusi au ukuvu.

Kuna aina ya nimonia inayosambazwa kupitia matone yaliyo viumbehai vinavyosababisha ugonjwa huu. Viumbehai hivi huingia kwenye hewa wakati mtu aliyeambukizwa anapopiga chafya au kukohoa.

Wakati mwingine maradhi haya hutokea wakati baadhi ya bakteria na virusi vinavyopatikana mdomoni, kooni na puani, vinapoingia kwenye mapafu.

Ni kawaida kwa mtu kuondoa uowevu ulio na virusi hivi kutoka mdomoni, puani na kooni lakini kama kawaida mfumo wa kinga mwilini huwa na uwezo wa kupigana navyo.

Lakini, iwapo hali ya kiafya ya mhusika imedhoofika kutokana na maradhi mengine, basi huenda akashambuliwa na aina kali ya ugonjwa huu.

Watu ambao hapo awali walishambuliwa na virusi, ugonjwa wa mapafu, maradhi ya moyo na kooni vilevile wanaotumia pombe na dawa za kulevya, wamo katika hatari ya kuambukizwa ugonjwa huu.

Ishara za Nimonia

 • Mafua yanayoambatana na kuchafya, maumivu ya koo na kukohoa
 • Homa kali, kutetemeka na kutoa kikohozi kilichochangamana na damu
 • Kushindwa kupumua
 • Wakati mwingine rangi ya ngozi hubadilika na kuwa rangi ya zambarau kutokana na kiwango cha chini cha oksijeni kwenye damu.
 • Maumivu ya kifua yanayoongezeka mhusika anapopumua.
 • Kuumwa na kichwa na maumivu ya misuli

Ugonjwa huu huthibitishwa vipi?

 • Maradhi haya hutambuliwa baada ya daktari kumfanyia mgonjwa uchunguzi wa kiafya na kugundua kupumua kusiko kwa kawaida kunakoambatana na sauti ya kukwaruza.
 • Uchunguzi wa eksirei unaweza fanywa katika sehemu ya kifua ili kuthibitisha kuwepo kwa maradhi haya.
 • Pia, sampuli ya kikohozi huchukuliwa na kuchunguzwa chini ya hadubini ambapo bakteria zinazosababisha homa ya mapafu hutambuliwa.
 • Damu kupimwa ambapo kiwango cha seli nyeupe za damu hutumika kutambua jinsi ugonjwa huu ulivyosambaa.
 • Tags

You can share this post!

TIBA NA TABIBU: Wanasayansi watahadharisha kuhusu uraibu wa...

DKT FLO: Nini husababisha kinyesi kuchanganyika na damu?

T L