DKT FLO: Kiharusi cha joto ni maradhi gani?

DKT FLO: Kiharusi cha joto ni maradhi gani?

Hivi majuzi kuna rafiki yangu alianza kuumwa na kichwa kisha baadaye kuzimia, ambapo baada ya kupelekwa hospitalini aligundulika kukumbwa na tatizo la kiharusi cha joto (heatstroke). Haya ni maradhi yapi?

Peris, Nairobi

Mpendwa Peris,

Hii ni mojawapo ya hali hatari zinazosababishwa na joto.

Mgonjwa huanza kuonyesha dalili kama vile kuumwa na kichwa, ugumu wa kuzungumza, kisunzi, kuzimia na hata wakati mwingine kupoteza fahamu.

Wakati huu halijoto ya mgonjwa yaweza fika nyuzi 40 na hata zaidi huku akikaukiwa na maji mwilini.

Hali hii huambatana na ishara kama vile kichefuchefu, kutapika, udhaifu, uchovu, kuumwa na kichwa, maumivu ya misuli na kuchanganyikiwa.

Ishara kamili za hali hii ni pamoja na halijoto ya mwili kuwa juu, kutokwa na jasho jingi, moyo kupiga kwa kasi, kushindwa kupumua.

Aina za kiharusi cha joto

•‘Classical heatstroke’: Aina hii huwakumba watu ambao huwa hawatokwi na jasho kwa urahisi. Iwapo mtu hana uwezo wa kutokwa na jasho kama kawaida, itakuwa jambo ngumu kwake kukabiliana na hali ya anga ya joto. Wengi wanaokumbwa na aina hii ya kiharusi cha joto huwa wazee na wanaougua maradhi hatari kama vile kisukari.

•‘Effort heatstroke’: Hali hii humkumba mgonjwa muda mfupi baada ya kujihusisha na shughuli katika eneo lenye joto.

Chanzo

Hali ya anga ya joto, kufanya mazoezi katika mazingira ya joto kupindukia, nyumba zilizo kwenye orofa za juu kabisa na ambazo hazina vifaa vya kudhibiti halijoto, kuvalia nguo za joto wakati wa joto, kunywa pombe kupindukia, uchovu, umri wa zaidi ya miaka 65, halijoto ya juu na baadhi ya maradhi kama vile ugonjwa wa moyo, ngozi, kisukari.

Kuzuia

•Walio na zaidi ya umri wa miaka 65 hasa wanaougua maradhi ya moyo wanapaswa kuwa waangalifu na hali ya anga ya joto.

•Mwili unapaswa kuzoeshwa na hali ya anga ya joto.

•Kunywa maji kwa wingi.

‘Breast abscess’ ni nini?

Ningependa kufahamishwa kuhusu hali inayofahamika kama ‘breast abscess’.

Lucy, Nairobi

Mpendwa Lucy,

Huu ni uvimbe unaoota kwenye matiti na kusababisha matatizo wakati wa kunyonyesha. Hata hivyo sio hali inayowakumba wanawake wengi. Hali hii hutokea wakati maambukizi ya mastitis yameachwa bila kutibiwa.

Ishara za hali hii

•Uchungu kwenye matiti huku sehemu hii pia ikivimba. Uvimbe huu huwa mwekundu na wenye maumivu mengi hasa unapoguswa.

•Mgonjwa huwa na joto jingi huku akionyesha ishara za kuwa na homa kali.

•Usaha kutoka kwenye chuchu za matiti.Hali hii hutokea chuchu zinapokumbwa na jeraha linalopelekea bakteria kuingia kwenye matiti na kusababisha maambukizi yanayofahamika kama staphylococcus aereus.

Wanaogua kisukari, wana uwezekano mkubwa wa kukumbwa na hali hii. Kadhalika waliowahi kufanyiwa upasuaji kwenye matiti, wako hatarini zaidi. Hali hii pia huwakumba sana wanawake wanaovuta sigara kwa wingi.

Kutokana na sababu kuwa kwa mara nyingi uvimbe huu huota karibu na sehemu ya juu ya ngozi, waweza ondolewa bila kufanyiwa upasuaji kupitia mbinu inayofahamika kama aspiration (kuondoa majimaji yaliyo katika uvimbe huu). Hata hivyo kuna wale ambao huathirika kila mara hasa ikiwa uvimbe huu hautaondolewa kupitia upasuaji.

Jinsi ya kuzuia hali hii

•Akina mama wanaonyonyesha na ambao wana maradhi ya mastitis, engorgement (maziwa kujaa kwenye matiti), wanapaswa kuhakikisha kuwa wanakamua maziwa yote kutoka kwenye matiti kila mara.

•Kabla ya kunyonyesha, ondoa maziwa kwenye matiti ukiyafinya kwa kutumia kitambaa kilichotumbukizwa kwenye maji yaliyopashwa moto kidogo.

• Nyonyesha mtoto vizuri kwa kuingiza sehemu nyeusi inayozunguka matiti mdomoni mwa mtoto ili kuzuia chuchu kukumbwa na majeraha na hivyo kuzima bakteria kuingia kwenye matiti.

  • Tags

You can share this post!

Shikanda ashukuru Ingwe kumwamini

ZARAA: Mashine za kisasa kuifanya kazi ya upanzi wa mboga...

T L