Habari

Dkt Mogusu atawagusa?

December 9th, 2020 3 min read

BENSON MATHEKA na LEON LIDIGU

“TUKO kwenye vita na lazima tushinde,” alisema Rais Uhuru Kenyatta mnamo Aprili 6, 2020, kwenye hotuba yake kwa taifa kuhusu virusi vya corona.

Lakini sasa imejitokeza kuwa ‘wanajeshi’ walio mstari wa mbele kupigana na adui wa Covid-19 wamepuuzwa na kuachwa kupigana bila silaha, yunifomu na hata pesa za chakula.

“Madaktari wengi wanahisi kupuuzwa, wana njaa, wamefilisika na baadhi wamelazwa hospitalini baada ya kuambukizwa virusi vya corona wakiwa kazini,” Dkt Stephen Mogusu aliambia Taifa Leo mnamo Jumanne wiki iliyopita kabla ya kuzidiwa na kulazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi.

Aliaga dunia mnamo Jumatatu wiki hii kutokana na corona.

Alikuwa mmoja wa madaktari 200 waliotumwa kuhudumu katika kaunti mbalimbali, ambapo alifanya kazi katika hospitali ya Machakos Level 5 alikohudumu katika chumba walimotengwa wanaogua corona.

Lakini kwa muda huo wote hakulipwa hata shilingi moja na hakuwa na bima ya afya.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo mnamo Jumanne wiki iliyopita, Dkt Mogusu alisema kwa uchungu: “Ninafanya kazi ya serikali katika mstari wa mbele kukabiliana na corona, lakini sina hata pesa za kununulia mtoto wangu nepi. Hii inanivunja moyo. Wakati mwingine najiuliza mke wangu ananiona nikiwa mwanamume wa aina gani!”

Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo wiki iliyopita ulionyesha kuwa madaktari na wahudumu wengine wanaohudumia wagonjwa wa corona katika kaunti zote 47 isipokuwa Makueni na Kakamega hawana nguo za kujikinga (PPE) na wanafanyishwa kazi kwa masaa mengi.

Baadhi walisema wameacha kazi kwa hofu ya kuambukizwa corona na kukosa pesa za kukidhi mahitaji ya familia zao.

Kwenye mahojiano, marehemu Dkt Mogusu alisema juhudi zao za kutaka kulipwa ziliambulia patupu huku Wizara ya Afya ikiwapuuza.

Hali ya kusikitisha ya madaktari, wauguzi na wahudumu wengine wakikabiliana na janga la Covid-19 imeanika uozo katika sekta ya afya.

Ingawa maafisa wa serikali wamekuwa wakiwasifu wahudumu wa afya kwa kujitolea kwao kukabiliana na janga hili na kuahidi kuwapa vifaa vya kazi, vifo vyao kutokana na maradhi wanayotegemewa kukabili vimeweka wazi uongo ambao serikali imekuwa ikieneza.

Kufikia sasa, madaktari 14 wameangamizwa na virusi vya corona huku kilio cha wenzao kwamba maslahi yao yamepuuzwa kikikosa kushughulikiwa.

Badala ya kushughulikia maslahi ya madaktari wakati huu wa janga la corona, viongozi wakuu wa serikali wamewaacha kuteseka huku wakielekeza nguvu na rasilmali kwa BBI.

Kwenye ujumbe alioandikia wenzake alipokuwa amelazwa hospitali, Dkt Mogusu aliyefariki akiwa na umri wa miaka 28, aliwashauri wenzake wanaofanya kazi katika hospitali za umma “kujiokoa” kabla hawajaambukizwa corona kama yeye.

“Ninachotaka kusema ni jiokoeni kutoka taasisi hizo (hospitali za umma). Mko na nafasi ya kufanya kazi siku zijazo. Mimi ni dhaifu sana kuweza kuandika mengi, jiokoeni!” alisema.

Ingawa Dkt Mogusu alikufa kabla ya kulipwa malimbikizi ya mshahara kwa miezi mitano, serikali imekuwa ikiwalipa madaktari wa Cuba wapatao 100 mamilioni ya pesa kila mwezi.

Licha ya madaktari na wahudumu wa afya kugoma kutetea maslahi yao hasa baada ya wenzao kufariki, viongozi na maafisa wa serikali wanachukulia matatizo yao kwa mzaha na kuwataka waendelee kuhudumu.

Akiwa Kisumu mnamo Jumatatu, Kiongozi wa ODM Raila Odinga alisema wahudumu hawafai kugoma Wakenya wanapouawa na corona.

“Wakenya wanakufa na haifai madaktari kuweka serikali mateka hasa wakati huu kuna changamoto za kiuchumi. Waliapa kulinda maisha ya watu na hawafai kugoma,” alisema Bw Odinga.

Kauli yake iliudhi Wakenya waliomlaumu kwa kufurahia masaibu ya madaktari ilhali miezi mitano iliyopita alienda ng’ambo kutibiwa.

Baadhi walishangaa zitakapotoka Sh14 bilioni za kuandaa kura ya maamuzi ya BBI ambayo Bw Odinga amekuwa akipigia debe kila uchao.

“Wakati Raila Odinga alikuwa mgonjwa alisafiri kwa ndege ya kibinafsi hadi Dubai kutibiwa katika hospitali ya Wajerumani. Kama wanasiasa wengine, ana bima na hutibiwa katika hospitali bora za kibinafsi nchini na ng’ambo. Kwa Raila na wanasiasa wenzake, BBI ndio muhimu kuliko maisha ya Wakenya,” mwanaharakati Bonface Mwangi alisema.

Kulingana na Gavana wa Busia Sospeter Ojaamong, madaktari wanafaa kusubiri kura ya BBI iishe ndipo maslahi yao yashughulikiwe.

Kulingana na Gavana huyo, hata wakigoma hawatapata chochote.

“Waambieni hao watu wa afya waache kugoma. Hata wakigoma hawatapata chochote. Wasubiri hii BBI ipite tuone kama itakuwa na mazuri,” alisema Gavana Ojaamong.