Habari za Kaunti

Dkt Monda ajitetea vikali kuchunga unga

February 29th, 2024 1 min read

NA WYCLIFFE NYABERI

NAIBU Gavana wa Kaunti ya Kisii Dkt Robert Monda ametoa majibu kwa kila mojawapo ya shutuma tatu ambazo madiwani wanadai ni makosa tosha ya kumtimua.

Dkt Monda mnamo Alhamisi alijitetea katika Bunge la Kaunti ya Kisii lilipokuwa likijadili hoja ya kumwondoa afisini.

Kuhusu ikiwa alipokea hongo ya Sh800,000 kutoka kwa mkazi mmoja wa Kisii ili amsaidie kupata kazi katika Kampuni ya Maji na Majitaka ya Gusii (GWASCO), Dkt Monda alisema pesa hizo zilikuwa za deni alilokuwa amekopesha babake mlalamishi.

Kuhusu ikiwa alimtumia Meneja Mkurugenzi wa GWASCO hongo ya Sh100,000 ili meneja huyo amsaidie ‘mtu wa Dkt Monda’ apate kazi ya Meneja wa Mauzo wa kampuni hiyo ya GWASCO, Naibu Gavana huyo alisema alimtumia Meneja Mkurugenzi wa GWASCO Sh100, 000 lakini ‘kimakosa’.

“Pesa hizo zilikuwa zimwendee afisa mmojawapo wa kaunti kwa kazi aliyonifanyia ya kusafirisha bidhaa za ujenzi nyumbani kwangu. Nilifikiri pesa hizo zilimwendea aliyefaa kuzipokea kumbe haikuwa hivyo. Nilibaini hilo wakati aliniuliza ni za nini,” akajitetea Dkt Monda.

Shtaka la tatu lilikuwa ikiwa aliwatumia vibaya maafisa wa kutekeleza amri za kaunti kwa kuwafanya vibarua katika shamba lake. Lakini akijitetea, Dkt Momda alisema hafanyi ukulima wowote wala ufugaji wowote wa ng’ombe katika kipande cha ardhi alichorithi kutoka kwa babake.

“Hakuna afisa yeyote wa kaunti ninayetumia vibaya wakiwemo wale niliopewa kisheria,” akajitetea.

Aidha, kiongozi huyo ambaye Gavana Simba Arati alijaribu kumtetea Jumatano, alijitetea akisema “sijamtishia mlalamishi anayedai kunipa hongo”.

Hata hivyo, Dkt Monda alichekesha wakati wa kusikilizwa kwa hoja dhidi yake alipokiri kuwa aliamuru ndugu yake akamatwe na polisi baada ya “kuikata miti yangu bila idhini”.

Aliwakilishwa na wakili Katwa Kigen.

Soma Pia: Madiwani Kisii wamkaidi Arati, waendelea na hoja ya kumng’atua Dkt Monda

Naibu Gavana wa Kisii Dkt Robert Monda (kushoto) akihojiwa na wakili wake Katwa Kigen katika Bunge la Kaunti ya Kisii mnamo Februari 29, 2024. PICHA | WYCLIFFE NYABERI