Habari za Kitaifa

Dkt Mutua afichua siri ya ongezeko la fisi nchini

February 7th, 2024 1 min read

NA MAUREEN ONGALA

WAZIRI wa Utalii Alfred Mutua ametangaza hali ya hatari kufuatia ongezeko la visa vya fisi kuwavamia wakazi katika maeneo mbalimbali nchini.

Kulingana na Dkt Mutua ni kuwa hali hii imesababishwa na ongezeko la idadi ya fisi nchini baada ya kuzaana kwa wingi.

Waziri alisema pia wameongezeka kwa sababu wanakula mizoga ya wanyama waliokufa kufuatia kiangazi kikali kilichokumba nchi mwaka 2023.

Akihutubia wanahabari wakati wa kuzindua shughuli ya kuwatafuta makurutu watakaojiunga na Shirika la Huduma kwa Vijana Nchini (NYS) katika uwanja wa Karisa Maitha mjini Kilifi, Dkt  Mutua alisema fisi hao wamekuwa kero katika maeneo ya jiji la Nairobi, Juja, Machakos, Makueni, Shimba Hills na maeneo mengine.

“Tuko na fisi wengi na kila mtu anauliza wametoka wapi. Lakini tunafahamu kuwa wanyama wengi wa porini waliaga dunia wakati wa kiangazi kilichoshuhudiwa nchini na fisi walisherekea kwa kula mizoga na hivyo kuzaana kwa wingi,” akasema Dkt Mutua.

Fisi akiwa katika mbuga ya Maasai Mara mnamo Aprili 20, 2020. PICHA | MAKTABA

Dkt Mutua alisema kuwa fisi hao wamekuwa wengi sana na kwa sasa wanazurura vijijini na kuwataka wananchi kuwa waangalifu ili kuepuka kuvamiwa.

“Tunatoa wito kwa wananchi kutotembea usiku katika maeneo hayo yasiyo salama kwa sababu ya tatizo hili la fisi,” akatahadharisha.

Alisema Shirika la Huduma kwa Wanyamapori Nchini (KWS) limepokea ripoti kuhusu watu waliovamiwa na kujeruhiwa na fisi na wengine kuuawa.

“Tayari tumetuma kikosi cha maafisa kuwatafuta fisi hao huku tukiendelea kuhamasisha jamii kuhusu jinsi wanavyoweza kuishi bila mgogoro na wanyama hao,” akasema.

Wakati wa shughuli hiyo, Dkt Mutua aliwashauri vijana kufahamu kwamba NYS itakuwa ngazi ya kuwawezesha kujiunga na jeshi, polisi na NYS.