Dkt Ruto adokeza uwezekano wa kuungana na Raila katika uwaniaji 2022

Dkt Ruto adokeza uwezekano wa kuungana na Raila katika uwaniaji 2022

Na MWANGI MUIRURI

NAIBU Rais Dkt William Ruto ametangaza Alhamisi kuwa kuna uwezekano wa yeye kuungana kisiasa na kiongozi wa ODM Bw Raila Odinga kuwania urais wa 2022 japo kwa masharti.

Akiwa katika mahojiano na kituo cha redio cha Citizen, Dkt Ruto amesema kuwa Bw Odinga hujiangazia kama aliye na maono ya kitaifa na “ingawa tunatofautiana naye mara kwa mara kuhusu masuala mengi haimaanishi hatuwezi kuwa na mpango.”

Kwa sasa, Dkt Ruto na Bw Odinga wako katika mirengo hasi kuhusu mswada wa marekebisho ya Katiba kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI), akisema kuwa kila mtu ana haki ya kuwa na msimamo kinzani.

“Haimaanishi hizi tofauti haziwezi zikasuluhishwa na tukawa na umoja. Hii BBI iachiwe wabunge sasa waipige msasa na wapendekeze pa kubadilishwa ndipo kila mmoja awe mshindi. Wanaonisukuma niongoze mrengo wa upinzani kuhusu BBI wamekosa mwelekeo. Ukiwa unataka mrengo huo wa kupinga uwe na kiongozi, wewe chukua jukumu hilo upinge na uache kunishurutisha… Hapo sipo,” akasema Dkt Ruto.

Kuhusu kuungana na Bw Odinga, Dkt Ruto amesema: “Sio sisi katika mrengo wa Hasla tutakuwa wa kuenda kumtafuta tuungane bali ni yeye wa kuja pamoja na wengine ambao wataona kuwa mipango yetu ya 2022 iko shwari.”

Amesema kuwa ni lazima yeyote au chama chochote cha kisiasa katika kusaka kuungana na Hasla kuwa tayari kubadilisha mjadala wa kitaifa kutoka uwaniaji nyadhifa, kabila au eneo na badala yake “tuwe na zile siasa za kulenga kuinua wale walio chini kiuchumi.”

Dkt Ruto amesema kuwa hawezi kamwe akajiunga na mrengo wa kisiasa ambao umekuja pamoja kwa msingi wa kuunganisha vigogo wa kisiasa wa kikabila wakiwa na vyama vyao vya vijiji vya kwao na kuishia kujiita “muungano mtakatifu”.

Ameonekana kulenga muungano wa kisiasa kati ya kiongozi wa ANC Bw Musalia Mudavadi, kiongozi wa Wiper Bw Kalonzo Musyoka, mwenzao wa Ford Kenya Bw Moses Wetang’ula na mwenyekiti wa Kanu, Gideon Moi.

Dkt Ruto aidha amekashifu uchambuzi wa Bw Mudavadi kuhusu jinsi ya kufufua uchumi wa taifa hasa kutokana na mzigo mkubwa wa madeni kutoka mataifa na taasisi ng’ambo.

“Tunajua kwamba shida yetu kama taifa kwa sasa ni mzigo wa madeni ambapo katika mwaka huu pekee wa kifedha, tutahitajika kulipa Shilingi Trilioni moja kwa wanaotudai. Mzigo huo unaendelea kuwa na uzito kwa kuwa bado tunaendelea kukopa. Suluhu letu sio jinsi ambavyo Bw Mudavadi amekuwa akisema eti tuombe muda zaidi wa kulipa madeni hayo,” akasema.

Kubuni nafasi za ajira

Alisema kuwa dawa ya uchumi wa taifa kwa sasa ni kusaka mbinu za kuwasaidia watu 16 milioni ambao kwa sasa hawana ajira ili wapate nafasi ya kuwa na pato ambalo litalipiwa ushuru ndio uchumi upanuke na kuwe na pesa za kulipa madeni hayo.

“Uchumi wetu hauhitaji hadaa kuwa Wakenya wengine watapewa likizo ya kulipia ushuru. Wakenya hawana shida na ulipaji ushuru na wako tayari kuanza kwa wakati wowote ule kutozwa ushuru. Ukiwapa mbinu ya kuunda mapato watakuwa tayari kiulipa ushuru. Hao ndio tunafaa tuwainue ili wakishaunda faida zao, walipe mikopo ambayo wametwikwa mabegani mwao na mikopo kiholela,” akasema.

Amesema kuwa vuguvugu lake la Hasla liko tayari kuunda hazina ya Sh60 bilioni ya kuinua uchumi wa walio chini ambapo Sh30 bilioni zitafadhili uendelezaji maeneo bunge huku kitita sawa na hicho kikiundwa cha kuwapa mikopo bila riba wote ambao hawana ajira na wangetaka kuijingiza katika biashara.

Dkt Ruto alisema kuwa kwa sasa ako ngangari, bado ako na imani ya kuibuka rais wa tano wa taifa hili baada ya uchaguzi wa 2022 na kuwa wale wanaopanga njama ya kumfungia nje wajipange kwa kuwa ako na maono na hatalegeza Kamba liwe liwalo.

Alisema kuwa taifa hili lilikuwa katika mkondo sawa kisiasa “kabla ya wageni waliokuja katika nyumba ya Jubilee (Handisheki) na tukaishia kukorofishana ndani ya boma kiasi wengine walianza kutimuliwa eti kwa kuwa wananiunga mkono kisiasa na kutangaza kwamba wao ni marafiki zangu wakaadhibiwa kwa kupigwa teke kutoka vyeo.”

Amesema hizo ni siasa za kipuzi, akiongeza kuwa bado yuko ndani ya chama tawala cha Jubilee “lakini kwa wakati tu unaofaa kwa kuwa chama cha United Democratic Alliance (UDA) bado ni mradi wetu wa Hasla na ambao utakuwa kimbilio letu iwapo joto litazidi kuelekezewa sisi ndani ya chama tawala cha Jubilee.”

You can share this post!

Mtaalamu aelezea kiini cha stroberi zako kukosa kuzaa...

Kanda ya Ziwa yapata fursa ya kumuaga Dkt Magufuli