Habari

Dkt Ruto ashauri maombolezo na mazishi ya Moi yasiingizwe siasa chafu

February 7th, 2020 2 min read

Na SAMMY WAWERU

NAIBU Rais Dkt William Ruto amesema safari ya kumpumzisha Rais Mstaafu Daniel Toroitich Arap Moi inafaa iwe tulivu na isihusishwe siasa chafu, “kwa kuwa ni baba yetu aliyetufanyia makuu”.

Dkt Ruto amesema wengi wa viongozi walio serikalini na pia wanasiasa walipitia mikononi mwa Mzee Moi, na kujumuisha siasa zisizo na mwelekeo katika harakati za kumpungia mkono wa buriani ni kumkosea heshima.

“Wengi wa viongozi tulioko serikalini na wanasiasa, karibu asilimia 60 tulipitia mikononi mwa Mzee Moi. Ametulea kisiasa. Moi alilea familia yake; wavulana na wasichana, pamoja na watoto wake kisiasa,” akasema Naibu wa Rais Alhamisi usiku kwenye mahojiano na kituo kimoja cha runinga.

Akionekana kushangazwa na tetesi kuwa hahusishwi katika maandalizi ya Rais huyo Mstaafu, Dkt Ruto alisema Mzee Moi ni kiongozi aliyefanyia Kenya mengi hususan maendeleo, akitaja sekta ya elimu kama aliyoipa kipau mbele katika utawala wake wa miaka 24.

“Anahitaji mapumziko ya hadhi, tuepuke siasa duni,” akasema.

Mzee Moi aliaga dunia mapema wiki hii, wakati akipokea matibabu katika Nairobi Hospital.

Saa chache baada ya kifo cha Rais huyo mstaafu kutangazwa, Dkt Ruto alihutubia taifa katika ofisi yake ya Harambee House Annex, jijini Nairobi, ambapo hakuwa ameandamana na afisa yeyote wa ngazi ya juu serikalini.

Baadaye, alifululiza hadi katika hifadhi ya maiti ya Lee Funeral, ambapo hakuna kiongozi aliyempokea.

Ni taswira ambayo Ruto amesalia kimya.

Waziri wa Usalama wa Ndani na Mikakati ya Serikali Dkt Fred Matiang’i, Mkuu wa Majeshi Samson Mwathethe na Inspekta Mkuu wa Polisi, IG, Hillary Mutyambai, waliandamana pamoja katika hifadhi ya Lee Funeral, na pia kuonekana kutoa mipangilio ya maombolezi ya Moi na mazishi yake, ambayo yatakuwa ya kitaifa.

Dkt Ruto na ambaye amewahi kuhudumu kwa karibu na Mzee Moi, alisema matamanio yake ni kuona marehemu amezikwa kwa njia ya heshima.

Alisema mara ya mwisho kuonana na Mzee Moi ilikuwa kati ya 2016 – 2017.

Rais Moi atazikwa Jumatano wiki ijayo, nyumbani kwake Kabarak, Kaunti ya Nakuru.