KIPWANI: Dogo anayetikisa visiwa vya Lamu

KIPWANI: Dogo anayetikisa visiwa vya Lamu

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

KUNA dhana kuwa wasanii wa kiume wakioa umaarufu wao hupungua hasa kutokana na kushindwa kutangamana na mashabiki wa kike kama zamani.

Lakini kwa Abbas Ali al-maarufu Man Azzer, hali imekuwa tofauti kabisa. Toka apate mwenza Desemba 2019, umaarufu wake umezidi kupanda.

“Wazo kwamba kuoa mapema kungezima nyota yangu halikuwahi kunijia akilini. Kwangu mambo yamekuwa shwari kabisa kwani nimemakinika zaidi na kazi zangu sababu moyo umetulia,” asema Man Azzer ambaye tangu aanze kuimba mwaka 2010, amesharekodi video tano na nyimbo 25.

Anasema kuwa nyimbo zilizomletea umaarufu zaidi ni ‘Utamu’, ‘Risala’, ‘Freestyle’, ‘Mapenzi’ na ‘Tosha’ huku video za Utamu, Macho na Tosha zikitizamwa zaidi kwenye YouTube.

Mtindo wake ni Bongo Flava ila pia kachanganya biti za kiarabu na kihindi zinazoshabikiwa sana kwao Lamu.

“Wajua natoka Lamu na huku kwetu mila na desturi za kihindi na kiarabu zimekolea hivyo nimeamua kuwapa mafans wakipendacho,” afunguka.

Anasifia mojawapo ya kete spesheli, alioachia 2017 kumhakikishia mpenziwe kuwa ni yeye tu na anashukuru lengo lake lilitimia kwani sasa ni mkewe na mpenzi wa moyo wake.

“Nilitoa kibao cha Sifa kumhakikisha mpenzi wangu kwamba nampenda kwa dhati na kwa kuwa hilo limetimia, nina imani tutakuwa pamoja daima dawamu,” afichua.

Aidha anamshukuru mno Yahya Ahmed Shee al-maarufu Basode, diwani wa wadi ya Mkomani, Lamu kwa kumpa sapoti kimawazo na kifedha ili kuendelea kukuza kipaji chake.

Dogo alianza kutambulika 2017 pale alipowakilisha Kaunti ya Lamu kwenye mashindano ya muziki mjini Mombasa na kutwaa nafasi ya tatu.

Baadaye, alipewa mkataba wa kurekodi albamu tatu mjini Kisumu.Isitoshe, ana mpango wa kusafiri Dubai na sehemu zingine za Arabuni kunoa makali yake ya ngoma za Kiarabu endapo atapata mdhamini.

Analalamika pia kuwa serikali ya Kaunti haijawapa wasanii wa nyumbani sapoti ipasavyo hasa wakati wa sherehe maalum na badala yake huwaalika wageni kutumbuiza.

“Tunastahili kupewa motisha kwa kuimba siku za sherehe ili nasi tupate vipato vitusaidie kunogesha vipaji vyetu,” amwaga.

Mbali na kuendelea na muziki, Man Azzer ameamua kuwashika mkono vipaji ibuka kwa kuanzisha studio yake ili kuwapa fursa ya kunoa talanta zao na kujipatia pato pia.

You can share this post!

DOMO: Ni kama ndrama, ni kama vindeo!

Yazamia kustawisha akademia ya soka kwa vizazi vijavyo

T L