DOMO: Kagundua followers sio wapigakura

DOMO: Kagundua followers sio wapigakura

NA MWANAMIPASHO

KUNA kujiamini halafu kuna kujichocha. Nataka kuamini mchekeshaji MC Jessy anajutia ile fursa aliyopewa na Naibu Rais William Ruto alipomshauri asigombee ubunge eneo la Imenti Kusini.

Badala yake aliahidi kumpa kazi kwenye serikali atakayounda akishinda uchaguzi. Alitaka MC Jessy amwachie mpinzani wake kwenye tiketi ya UDA.

Mwisho wa siku aliipiga chini na kuamua kugombea kama mwaniaji huru.

Sasa yeye pamoja na yule mwaniaji wa tiketi ya UDA wote wamepoteza baada ya kubwagwa na mgombea wa Jubilee.

Nahisi kucheka sababu nakumbuka jomba akisema alikaa na wazee na wakamsisitizia kuwa asithubutu kung’atuka kwenye kinyang’anyiro hicho.

Sasa hapa nipo najiuliza hivi, hao wazee sasa wapo wapi sababu hapa walimchocha tu? Lakini tena kwa nini asingefuata ushauri wa Naibu Rais? Sasa atalazimika kurudi kuwachekesha watu.

Ile chaneli yake ya YouTube sasa atarudi kuendelea na mishemishe sababu alikuwa ameitelekeza. Ndio sababu nasema huku ni kujiamini kupitiliza.

Hata kama aliamua kuendelea na kampeni, angesaka mbinu ya kuendelea na chaneli yake. Lakini pia ni kwa nini asingeanza na kugombea MCA kisha taratibu apande? Au ni baada ya kumwona Jalas akifanya yake kule Langata naye akaamua kupambana?

Asisahau Jalas amepita kwa bahati kubwa. Nina uhakika kama sio mkono wa Baba, jamaa angechimba. Angechimba kama yeye na yule mtoto wa mama aliyechimba kule Mathare North.

Mtoto wa mama, kazi yake ni kulialia tu. Alijitanusha kifua kuwa angeshinda ubunge, sasa sijui yupo wapi. Diana wake natumai anamshughulikia maana kimbunga kilichomkuta, wewe acha tu!

Sijawahi kuwaamini wasanii wanaojitosa kwenye siasa kuwa watu wenye nia njema. Kwa miaka zaidi ya kumi nimekuwa nikiwaangazia wasanii kwenye makala za burudani. Nimefanikiwa kutangamana nao mara kwa mara na nitasema hivi, wengi wa watu hawa ni wabinafsi, wanajipenda, wanajiona miungu hivyo mimi kuona wakishushiwa viboko na wananchi kwa kutochaguliwa bungeni, nafsi yangu inaridhika sana.

Kwa MC Jessy, nafikiri yupo vizuri zaidi akiendelea kutuvunja mbavu. Naelewa maisha yamekuwa magumu toka shoo ya Churchill iliyokuwa ikimbeba kubuma. Michongo ya Umcee pia imepungua kutokana na ushindani uliopo. Hivyo kubwa aliloachwa nalo ni kusaka pesa kwa kutengeneza content.

Naamini kabisa nia yake ya kutaka kuwa mbunge ilikuwa ni kujipunguzia presha ya kimaisha wala siamini kama jamaa anazo sifa za uongozi. Ila najua ana sifa zote za mburudishaji. Nawacheka sana sababu walichanganywa na umati wa mitandaoni.

Umaarufu wa kuwashobokea watu mitandaoni ni tofauti. Sasa wamebaki wakililia chooni. Wameelewa kuwa wao sio sukari kama walivyotegemea. Kwenye ground wapiga kura ni kina mama, bibi zetu, baba na babu zetu.

Hawa wanajali zaidi maisha yao na wala sio maisha ya wana Insta.

Wawili hawa bora waitane kijiweni wanywe mtori wa moto kutuliza joto halafu baada ya hapo, waambatane moja kwa moja hadi kwenye ile shoo ya Diana au shoo aliyokuwa akifanya MC Jessy waendelee kutengeneza content.

  • Tags

You can share this post!

ODM walemea Kenya Kwanza ubunge Pwani

Serena abanduliwa Canadian Open

T L