Makala

DOMO KAYA: Ama kweli ustaa una kazi

June 28th, 2019 2 min read

Na MWANAMIPASHO

AISEE! Kwa siku chache hizi zilizopita showbiz ya +254 na +255 imebamba kinoma.

Leo ya kwangu nitakuwa tu ni kugusia matukio ya Showbiz yaliyoniacha hoi.

Nitaanza na P-Unit.

Sijui kama mumesikia mapya kutoka kwa hawa makaka watatu? Majamaa wanadai fidia ya mkwanja mrefu kutoka kwa benki ya KCB.

P-Unit inayoundwa na Frasha, Gabu na Bon-eye wametishia kwenda mahakama kudai fidia ya kile wanachodai kuibiwa kwa wazo lao la msemo ‘Weka Weka’ na KCB.

Weka Weka’ ilikuwa wimbo walioachia 2015 na kuwa bonge la ‘hit’. Sasa wiki chache zilizopita KCB walianzisha promoshoni yao mpya ya kibiashara ‘Weka Weka Promotion’, nao P-Unit kwa uzumbukuku wakadai kuibiwa msemo huo.

Inashangaza ni jinsi gani walivyokosa hekima kwa madai haya. Lakini hata zaidi kwa mawakili wao kushindwa kuwachanua.

Mwanzo wanachodai sio matumizi ya wimbo wao Weka Weka bali ni msemo huo. Sijawahi kumwona mwenye hati miliki ya lugha mpaka walipotokea hawa majuha watatu.

Naaamini waliamua kuzusha wakitumai KCB itaogopa kuharibu jina na ikubali kuwafidia. Lakini kwa bahati mbaya ikala kwao. KCB wameganda kwa kusisitiza maneno hayo sio hati miliki ya mtu kwa kuwa ni lugha ya Kiswahili.

Sijui anayewashauri P-Unit katika hili ila naye pia ni mpuzi kama tu wao. Ningetaka kuamini wanaamini wanapaswa kufidiwa jinsi ilivyomtokea mshikaji wao Nonini alipozusha Safaricom ilipoiba kauli aliyodai kubuni ‘Gigagaga’ japo ni neno la kitaaa.

Tofauti ya Nonini na wao ni kwamba, Safaricom ilitumia kabisa kipande cha wimbo wake Manzi wa Nairobi ambapo yapo maneno hayo pasi na idhini yake.

Safaricom walifanya kweli na kuingia naye kwenye mkataba wa kimatangazo. Pengine ndicho hawa masela wanachowazia, ila ndio imekula kwao.

Nikiachana na o natua kwake Wema Sepetu.

Kichuna wa mtu bado anahangaishwa na kesi ya ule mkanda akipigana mate na mpenzi wake wa zamani PCK. Mapema wiki hii ndio aliachiliwa kutoka seli baada ya kuwa kule kwa siku saba kwa kukiuka masharti ya dhamana aliyokuwa nayo.

Kikweli namwonea huruma, maisha yake siku hizi asilimia 70 anatumia kuzunguka kwenye mahakama mbalimbali kujibu mashtaka. Ukiachana na hii kesi pia ana nyingine anakoshtakiwa kwa kupatikana na bangi.

Maisha ya Wema yamekuwa ya vikwazo tupu. Kama sio utata wa kikazi, basi ni utata wa kimapenzi. Mwenyewe hajihurumii, ila juzi nilipomwona akihepa kutoka mahakamani baada ya kuachiliwa, nilihisi kachoka na drama hizi. Ila Wema huyu ni mkorofi tu. Acha nisubiri kusikia ni kipi ataibua kipya.

Nikikanyagia ya Wema, namwibukia mwehu Ringtone. Kwa kweli bado sijui tatizo la huyu jamaa ni nini. Amekuwa akimsaka mke kwa kutembea na bango jijini liloandikwa sifa za mwanamke anayemsaka. Alipeleka upuzi huo katika kanisa lake Bishop Kiuna- JCC, kanisa la watu wenye pesa, kilichofuatia ni kutimuliwa na polisi. Sijui anachojaribu kukifanya ni kipi ila kiki hii yake kwa sasa imekataa. Kachosha kila mtu.

Nashangaa kwa hela alizonazo ni vipi bado hajasumbuliwa na maslay queen. Kama kuna wa kumshauri, bora amwelezee kiki hiyo sasa imeisha nguvu. Kailazimisha kwa zaidi ya miezi miwili, ni wakati atafute kiki nyingine na safari hii ajitahidi kuwa mbunifu kidogo na kiki hizo.

Labda kwa kumalizia ni kitu alichojaribu kukifanya Eric Omondi akiwa na matumaini itatrendi. Kuna video iliyovuja inayomwonyesha akiwa kitandani na slay queen mmoja hivi. Eric anajifanya kusisinzia baada ya ‘shughuli’ nzito eti huku slay queen akiwa anachukua selfie.

Kwa bahati mbaya Erico hapa alianguka mtihani. Wajanja tulishaiona zamani kiki aliyokuwa akijaribu kuibua. Eti baada ya kuachana na Chantal toto la Kiitaliano, maisha yameendelea.

Kosa walilofanya ni kusahau kumwambia slay queen aoshe uso angalau zile kilo kadhaa za vipodozi usoni mwake zipungue.

Inawezekanaje kama wote walikuwa usingizini baada ya mechi chumbani, kwa yule slay queen kuamka akiwa kakoleza vipodozi tena huku akiwa amevalia pajama nyeupe za hotelini? Huu usanii bwana, kweli una kazi.